MTATURU ACHANGIA MILIONI 3 MRADI WA MAJI


MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amehudhuria mahafali ya 11 ya darasa la saba ya shule ya Msingi Aghida iliyopo kijiji cha Tumaini katika Kata ya Issuna na kuwapongeza walimu na wazazi kwa malezi mema ya wanafunzi.

Aidha,amechangia Shilingi Milioni tatu kwa ajili ya kukarabati kisima cha maji ili kiweze kutoa huduma wakati wanaandaa mkakati wa kudumu wa kuchimba kisima kirefu ili kukidhi mahitaji ya maji kwenye kijiji hicho.

Mbunge Mtaturu amechangia kiasi hicho cha fedha baada ya risala iliyosomwa kuonyesha uwepo wa changamoto ya maji kutokana na kisima kilichokuwa kinatumika kinahitaji ukarabati.

Akizungumza katika mahafali hayo Octoba 3,2023,Mtaturu ametoa pongezi kwa uongozi wa shule na wazazi kwa kuanza kutoa lishe kwa watoto shuleni kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya kuongeza ufaulu.

“Serikali inajenga miundombinu,inaleta walimu hivyo ni wajibu wa wazazi kuwaandaa watoto kwak uwanunulia sare za shule na chakula ili waweze kuzingatia masomo yao,”amesema.

Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzie wa darasa la saba mwanafunzi Hamida Mayunga amempongeza mbunge kwak ushirikiana nao katika mahafali hayo na kueleza changamoto ya upungufu wa walimu.

“Tunafahamu na tunaona serikali imefanya mambo mengi ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo yaliyoondoa kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo lakini bado tuna upungufu wa walimu,

“Hapa shuleni walimu waliopo ni saba na ikama inataka wawe 11,lakini pia kuna changamoto ya umeme na maji kwani kisima kilichokuwa kinatumika kinahitaji ukarabati,”amesema.

Awali,Mbunge Mtaturu amekagua ujenzi wa daraja kwenye barabara ya Msui hadi Tumaini inayoendelea kujengwa na mkandarasi ili kuimarisha mawasiliano ya Kijiji cha Tumaini na Nkuhi kwenye Kata ya Issuna ambayo kipindi cha mvua husababisha adha kubwa kwa wananchi na wanafunzi wanapoenda shule.

Akizungumza mwananchi wa Kijiji cha Tumaini Swalehe Nkwimba amempongeza Mbunge Mtaturu kwak uendelea kuwa sauti yao kwenye kero wanazompatia.

“Tunaomba utufikishie salamu zetu za shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya,kila tukitembea tunaona maendeleo aliyoyafanya kwa ajili yetu,tunshukuru sana,”amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post