MRADI KITUO CHA KUPOZA UMEME CHALINZE WAFIKIA ASILIMIA 84.3


Na Mwandishi wetu,Pwani.

*Asisitiza Watanzania wanataka umeme*

*Atoa Pongezi kwa wafanyakazi kwenye mradi huo

*TANESCO wapongezwa kwa hatua ya ujenzi*

Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme wa Msongo wa kilovoti 400/220/132/33 wa kituo cha Chalinze umefikia asilimia 84.3 na hivyo kuleta matumaini ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme. 

Hayo yameelezwa leo Oktoba 12, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa  kituo hicho cha Chalinze Mkoani Pwani, kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo. 

"kwa sasa  ujenzi umefikia asilimia. 84.3 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 31 Disemba, 2023. Mradi huu unakwenda kupunguza changamoto ya umeme kwa kiasi kikubwa hususan katika mkoa huu wa Pwani," amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, mara baada ya Mradi huo kukamilika, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea Megawatt 2115 kutoka katika Bwawa la kuzalisha Umeme wa Maji la Julius Nyerere na kitasambaza Megawati 850 kwenye mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani na kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa hiyo. 

Akizungumza na wafanyakazi wanaofanya kazi katika mradi huo amewataka wafanye kazi kwa bidii kwa kuwa Serikali imewapa ushirikiano ili mradi huo ukamilike kwa wakati. 

Meneja wa Mradi wa kituo hicho Mhandisi Newton Livingstone Mwakifwamba amesema kuwa Serikali imetoa ushirikiano mkubwa katika utekelezaji hususan katika mazingira mazuri ya wafanyakazi. Amesema mradi huo utakamilika kwa muda uliopangwa ifikapo mwezi Desemba 2023.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema toka kuanza kwa mradi huo hakuna changamoto iliyojitokeza kukwamisha mradi huo. Amempongeza Dkt. Biteko kwa kutembelea mradi huo kujionea maendeleo yake.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa mradi utakapokamilika utakua ni msaada mkubwa wa mkoa wa Pwani.

Mradi huo ulianza rasmi tarehe 6 Septemba, 2021 ambapo kazi za ujenzi zilianza tarehe  11 Oktoba, 2021 na unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze pamoja na kituo cha kupoza umeme na kusafirisha umeme kuelekea mikoa ya kaskazini kwa kuingizwa Kenya Gridi ya Taifa.

Ziara hiyo ilihudhuriwa na  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango na Uwekezaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Decklan Mhaiki, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash na Viongozi Mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani na Watumishi wa mradi huo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post