MILIONI 710 KUIMARISHA UTOAJI HUDUMA ZA AFYA MBINGA
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Afya Kindimbachini kilichopo katika Kata ya Muungano Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma

Na. WAF, Mbinga- Ruvuma
 Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema kuwa Kituo cha Afya Kindimbachini kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kitapokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Milioni 710 ndani ya mwezi mmoja ili kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma za afya kituoni hapo

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel katika uzinduzi wa Kituo cha Afya Kindimbachini kilichopo katika Kata ya Muungano Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma

Dkt. Mollel ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha utoaji wa Huduma za afya nchini kwa kuhakikisha vituo vya kutolea Huduma za afya vinakuwa na miundombinu bora, vifaa tiba na vitendanishi, dawa pamoja na uwepo wa wataalamu wa Afya.

Aidha amewapongeza wananchi wa Kata hiyo kwa kuchangia shilingi Millioni 22 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya pamoja na shilingi Millioni 9 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa Afya.

"Niwapongeze sana wananchi wa kata ya Muungano kwa kuunga mkono serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo ili kuhakikisha afya zenu na watanzania kwa ujumla zinakuwa salama”, Amepongeza Dkt. Mollel

Pia ametoa wito kwa wananchi hao kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo nchini ili kuweka mazingira rafiki kwa vizazi vya baadae.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Muungano, Mhe. Paulo Kayombo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi makini wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi kwakua wananchi hao walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vituo vingine jirani hususani wakina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post