MATUMIZI SAHIHI YA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI SULUHISHO LA UPOTEVU WA RASILIMALI ZA SERIKALI

Waziri wa Fedha Dr. mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa uzinduzi Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama ‘GPSA.


Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kieletroniki Serikalini, yametajwa kuwa suluhisho la kudumu katika kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za serikali ikiwemo mapato yatokanayo na vyanzo mbalimbali nchini.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Waziri  wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba, wakati akipokea na kuzindua Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama ‘GPSA Intergrated Management Information System’ (GIMIS), kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene.

Amesema kuwa, matumizi ya mifumo imara ya kielektroniki yanasaidia kuondoa mianya ya upotevu wa rasilimali za Serikali na kudhibiti watumishi  wasio waadilifu, kwakuwa malipo yote ya serikali yatalipwa kupitia njia sahihi na salama katika taasisi husika.

“Tukifanya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki tunapunguza makosa mengi ya kibinadamu, hivyo matumizi sahihi ya mifumo hii yatatuwezesha kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu ikiwa ni pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya serikali”, anafafanua Dkt.Mwigulu.

Ameeleza kuhusu mfumo huo Dkt. Mwigulu alisema kuwa, mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), ambapo kwa sasa  majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa kupitia  mfumo huo ambao umesaida kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Dkt. Mwigulu ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha inaunganisha mfumo wa Manunuzi Kielektroni (NeST) na mfumo wa GIMIS kwa kuwa, mfumo huo unatumiwa na Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala, Ofisi za Mikoa na Halmashauri za Wilaya nchini katika kupata huduma za GPSA. 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  George Simbachawene amesema kuwa, lengo la mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), katika uuzaji wa mafuta Serikalini, ili kuweka uwazi na kutunza kumbukumbu za matumizi ya mafuta katika kila taasisi ya umma.

Amesema kuwa, hadi sasa zaidi ya taasisi nunuzi 7070 zinatumia mfumo huo ambapo, taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila taasisi zinatunzwa katika mfumo huo na kusaidia katika uandaaji na usimamizi wa mipango ya bajeti ya ofisi, pamoja na udhibiti wa matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma.

“Lengo la mfumo huu ni kuhakikisha matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma na kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kutokana na kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi za matumizi ya mafuta”, anasisitiza.

Ameongeza kuwa, kupitia mfumo huo, Serikali inaweza kufahamu kiasi cha mafuta yaliyotumika na yaliyobaki, magari yaliyopatiwa mafuta, muda, mahali na tarehe na hivyo kuziwezesha taasisi husika kuweza kudhibiti matumizi ya mafuta ikiwa ni pamoja na kuondoa udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu.

Aidha, katika utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuunganisha mifumo ya TEHAMA Serikalini, Simbachawene alisema kuwa, Mfumo huo umekwisha unganishwa kwenye mfumo mkuu wa Serikali wa kuwezesha mifumo kubadilishana taarifa (GovESB).

Aidha tayari umeshaanza kubadilishana taarifa na mifumo ya baadhi ya Taasisi za Umma kama vile mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali (GePG) pamoja na mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Taasisi (ERMS).

Mfumo wa GIMIS umesanifiwa na kujengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post