CHONGOLO AANZA NA UMEME AKITUA KATAVI ZIARA YA SIKU 5

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akizungumza wanachama, viongozi wa CCM na wananchi wa Mpanda Mjini, Jumatatu Oktoba 2, 2023 katika ofisi za chama hicho Mkoa wa Katavi, mara baada ya kuwasili mkoani humo, kuanza ziara ya kikazi,

************

Na mwandishi Wetu, Katavi


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Godfrey Chongolo amewahakikisha wananchi wa Mkoa wa Katavi kuwa Chama hicho kitasimamia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maeneo ya mkoa huo, utakaopatikana kwa kuunganishwa na gridi ya taifa.

Akizungumza na wanachama, viongozi wa CCM na wananchi wa Mpanda Mjini, Jumatatu Oktoba 2, 2023 katika ofisi za chama hicho Mkoa wa Katavi, mara baada ya kuwasili mkoani humo, kuanza ziara ya kikazi, Ndugu Chongolo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia changamoto ya kukosekana kwa umeme wa kutosha katika mkoa huo kutokana na kutounganishwa na gridi ya taifa.

“Suala la kuunganisha laini ya umeme wa gridi ya taifa kutoka Tabora kuja Mpanda, ujenzi wa vituo va kupoza umeme tayari vimeshamilika. Lakini umeme wa kupokelewa ili upozwe ndiyo haupo. Subira imekuwa ndefu.Nimeambiwa viongozi kadhaa wamekuja kuelezea hilo na kutoa maelekezo kadhaa na maagizo ili Mpanda na Nkasi wapate umeme wa uhakika.

“Sisi tuliahidi mikoa hii yote ambayo haijaunganishwa na gridi ya taifa tuhakikishe inaunganishwa katika kipindi cha miaka hii mitano ya utekelezaji wa Ilani.

“Kigoma wameshaunganisha kwa sehemu kubwa ya mkoa, Rukwa tayari bado Mkoa wa Katavi. Niwaahidi ninatamani kuchaguliwa kwa kishindo katika mkoa huu Chama Cha Mapinduzi , ni matamanio yangu hayo ni kutokuwa na ahadi hewa itakayotusumbua au kutupatia maswali huko mbele.” amesema Chongolo.

Amewaambia wananchi atazungumza na Waziri wa Nishati ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo.“Nitawaita wanaohusika na hili jambo , huu mradi unafanywa na TANESCO.

“Hivyo niachieni nitaenda kukaa na Waziri anayehusika na TANESCO bahati nzuri amepewa mamlaka makubwa kwa hiyo hana sababu ya kujitetea.Nitakwenda kumwambia aje kuangalia uhalisia wa utekelezaji wa huu mradi.

“Pili ahakikishe anaweka nguvu zake hapo ili wananchi wa Mkoa wa katavi sasa na wao wapate umeme wa gridi wa taifa na sio vinginevyo.”

Akieleza zaidi amesema ameambiwa na Mkuu wa Mkoa kwamba watu wengi wanataka kuwekeza katika viwanda vikiwemo vya kuchakata alizeti na tumbaku lakini changamoto ni umeme wa uhakika.

“Sisi lazima tuwe mbele ya wananchi , sio wananchi watangulie hatutawatendea haki.Ni lazima tuhakikishe tunalifanyia kazi.Kazi yangu ni rahisi kwenda kusimamia kuhakikisha tuliyokubaliana tunatekeleza.

“Naenda kusuma mradi huu, hatuwezi kuwa na barabara nzuri kutoka Tabora kuja hapa halafu umeme tu wa kuunganisha nguzo ukatushinda.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post