WAZIRI MBARAWA AFUNGUA MKUTANO WA KWANZA WA KIMATAIFA WA USAFIRISHAJI NA USAMBAZAJI


WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amekipongeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kuendelea kufanya tafiti zinazoboresha sekta hiyo kwani mpaka sasa Serikali imewekeza miradi mbalimbali ambayo inaendana na tafiti kutoka kwa wataalamu.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa Usafirishaji na Usambazaji ulioandaliwa na NIT, Waziri Prof.Mbarawa amesema sekta ya usafirishaji inahitaji wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kufanya kazi katika miradi ya kimkakati inayoendelea nchini.

"Nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea kama haina sekta mahiri ya usafirishaji kwa mfano, mizigo itakuja hapa Dar es Salaam lazima iwafikie Watanzania mbalimbali,’’ amesema


Aidha amesema kuendeleza miradi hiyo inahitaji wafanyakazi na wataalam hivyo basi NIT kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi, watayarishe wataalam wazuri ambao wataitoa nchi kutoka mahali ilipo na kukuza uchumi kwa wananchi wetu ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea sekta ya usafirishaji.

‘’Tumesaini mkataba wa Sh bilioni 630 kwa ajili ya kujenga karakana ya meli katika bandari ya Kigoma, kwa kujenga meli mbili kwa ajili ya kusafirisha mizigo na meli moja itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3,500 ambayo itasafiri kupitia Ziwa Tanganyika na meli ya pili itasafiri Ziwa Victoria ikiwa na uwezo wa kubeba tani 3,000,’’ alisema.

Pamoja na hayo amesema ni mara ya kwanza katika historia kuwahi kujenga kiwanda kamili chenye vifaa vyote vya kisasa vinavyohusika na ujenzi wa meli.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof. Zacharia Mganilwa amesema kuwa taasisi za elimu ya juu zina majukumu matatu ikiwemo kufundisha, kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu hivyo kupitia mkutano huo, watafiti watatoa matokeo ya tafiti walizozifanya kwa kushirikiana na nchi zilizoendelea.

”Mkutano huu unakwenda kutoa majibu au takwimu zitakazowafanya wanaoendesha mashirika mbalimbali ya uchukuzi hapa nchini kama vile Shirika la Reli Tanzania (TRC), Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambao wataifanya sekta yetu ya uchukuzi na usafirishaji iweze kufanya utendaji wenye tija kwa matumaini makubwa ya serikali ilivyowekeza na matumaini kwa wananchi waweze kupata huduma nzuri katika usafirishaji,”amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post