WADAU WATAKIWA KUSAIDIA UTEKELEZAJI WA MWONGOZO WA UTAMBUZI WATOTO WENYE ULEMAVUMkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Rasheed Maftah akifungua Kongamano la Afya kwa Viziwi leo Septemba 29, 2023 lililofanyika jijini Mbeya, katika kuelekea kilele cha wiki ya Viziwi Duniani itakayofanyika kesho jijini humo.


Washiriki wa Kongamano la Afya kwa Viziwi lililofanyika jijini Mbeya Septemba 29, 2023 wakisikiliza mada.

Na Mwandishi Wetu, MbeyaSerikali imetoa rai kwa wadau kusaidia kuwajengea uwezo Waratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto na Maofisa Lishe ngazi ya mikoa katika kutekeleza Mwongozo wa Taifa wa utambuzi wa mapema na afua stahiki kwa watoto wenye ulemavu.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ndio yenye dhamana ya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo.

Akifungua kongamano la afya kwa Viziwi leo Septemba 29, 2023 jijini Mbeya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu kutoka ofisi hiyo, Rasheed Maftah amesema Maofisa Ustawi wa Jamii na Maofisa Maendeleo ya Jamii wa mikoa nchini tayari wamepatiwa mafunzo ya utekelezaji mwongozo huo.

“Wizara ya Afya na wadau wetu Shirika la Afya Duniani (WHO) tunaomba mbebe jukumu la kuwajengea uwezo waratibu wa afya ya uzazi wa mama na mtoto namna ya kuweza kutekeleza mwongozo huu ili mtoto anapozaliwa apate na vipimo vya usikivu ili kuona hali yake ya kiwango cha usikivu na kama kuna dosari zozote afua stahiki ziweze kufanyika,”amesema.

Amesema Machi 16, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na watu wenye ulemavu Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na kuelekeza kuimarishwa kwa mfumo wa utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu na kuwaunganisha na afua stahiki ili kuzuia au kupunguza makali ya ulemavu.

Aidha, ameomba moja ya maazimio ya kongamano hilo iwe ni kuweka mikakati ya kusambaza mwongozo wa El-nino uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa ili kuwafikia watu wenye ulemavu kama ilivyokuwa wakati wa kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

“Tunashukuru wenzetu wa Ofisi ya Waziri Mkuu idara ya Maafa tayari wameshatoa mwongozo wa maafa kuelekea kipindi cha El-nino, kama mnavyofahamu kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa tayari tumeshaelezwa kwamba kwa mwaka huu na ujao huenda tukawa na mvua nyingi ambazo kitaalamu zinaitwa El-nino,”amesema.

Ameongeza kuwa “Sisi kama sekta ya watu wenye ulemavu hatujabaki nyuma tutumie mwongozo huu wa maafa ili kuiandaa jamii yenye uziwi kama ilivyofanyika wakati wa ugonjwa wa Corona ambapo jamii hii ilivuka salama.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post