SHILINGI 300 INAVYO HATARISHA AFYA ZA WAFANYABIASHA SOKO LA SABASABA


 
Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.
 Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeshauriwa kuwachukulia hatua za haraka wafanyabiasha wa soko la Sabasaba wanaokiuka kanuni za utunzaji wa mazingira kwa kumwaga haja ndogo kwenye maeneo yao na kusababisha harufu mbaya inayotishia afya za wateja.

Wafanyabiasha hao wamekuwa wakitumia chupa na makopo kukojolea badala ya kutumia Choo kisha kumwaga kwenye maeneo ya wazi na kusababisha uharibufu wa mazingira na kutaja sababu ya kufanya hivyo ni gharama kubwa ya huduma hiyo ambayo ni shilingi 300 kwa huduma moja.

Baadhi ya Wateja wanaopata huduma za kijamii katika soko hilo Jijini hapa wametoa ushauri huo wakati wakizungumza na Mwandishi wa habari hii na kueleza kuwa wamechoshwa na tabia hiyo ambayo imezoeleka ya kuchafua  soko hilo ambalo ni muhimu kwa wakazi wa Jiji la Dodoma.

Herriet Thomas ameeleza kuwa wafanyabiasha wengi wamekuwa wakitumia makopo na chupa za maji kama choo kisha kumwaga nje kama njia ya kukwepa gharama za huduma ya choo ambayo ni shilingi 300.

"Ukipita kwenye maendeleo ya Saluni na maduka ya nguo kuna harufu mbaya kwa sababu wanamwaga haja ndogo,kuna wale wa Saluni wanachanganya maji machafu na mikojo kisha kuyamwaga nje,unaweza kudhani wanamwaga maji kupunguza vumbi kumbe ni njia ya kumwaga haja ndogo kuepuka gharama,"amesema

Hayo yanatokea wakati Serikali ikiendelea kupigia kelele suala la utunzaji na usafi wa mazingira sambamba na kuahidi kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiasha ndogo ndogo nchini(wamachinga) .

Hali hii imesababisha maeneo ya soko hilo hususani kwenye vibanda kuwa machafu yenye harufu mbaya jambo linaloweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ikiwemo kipindupindu na kuhara.

Sufiani Moses Mfanya biashara wa matunda Katika soko hilo anasema kutokana na umuhimu wa eneo hilo Serikali inapaswa kuwashawishi wawekezaji wa huduma hizo za vyoo kuweka bei wezeshi ili kumudu gharama hizo .

"Hakuna asiyefahamu umuhimu wa soko hili,linaingiza mapato makubwa kwenye  Halmashauri ya Jiji ,jambo la kushangaza ni kwamba hakuna choo kinachoendana na hali ya wafanyabiashara nadhani kwa sababu vinamilikiwa na wawekezaji huru jambo linalopelekea bei ya huduma kuwa kubwa,"amesisitiza 

Kutokana na hayo Malunde Blog imeshuhudia maeneo ya  mabanda ya nguo na vibanda vya Saluni kwenye eneo hilo kukiwa na harufu ya haja ndogo  na kusababisha baadhi ya wateja kushindwa kupata huduma za kijamii kwenye eneo hilo.

Mmoja wa wafanyabiasha wa eneo hilo Edna Mahembaa amesema kwa siku moja mtu anatakiwa kutumia shilingi 1200 Kwa ajili ya Malipo ya huduma ya choo jambo analodai kuwa ni gumu kutekelezeka kutokana na ugumu wa maisha.

Hata hivyo anashauri kuwa uwepo utaratibu maalum wa kuwasaidia kupunguza gharama za huduma hiyo hadi kufikia shilingi 100 au 200 badala ya shilingi 300 kuendana na hali ya wafanyabiashara hao.

Anasema,"Mtu mmoja anatakiwa kutumia gharama ya shilingi 1200 Kwa siku Kwa sababu huwezi kwenda chooni mara moja Kwa siku,Kwa ujumla mtu aliyekamilika analazimika kwenda zaidi ya mara tatu kwa siku,huwezi kujizuia,"amesema

Naye Khamis Seganje amesema kuwa gharama hiyo ni kubwa kubwa mno Kwa wafanyabiasha wa kawaida na kufafanua kuwa wengi wao wanapigia hesabu zaidi kwenye chakula na mahitaji mengine.

"Hii shilingi 300 ukiizidisha mara tatu tayari unapata 1200,hapo tayari unapata sahani ya chakula,hela hiyo hiyo ukiipigia hesabu kwa mwezi unapata shilingi elfu  36000 ambayo unaweza kulipia pango,ndo Mana tunashindwa kwenda chooni,"Amesema Balozi wa Mazingira,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Oliver Nyeriga  ameshauri jitahada za mapema kufanyika ikiwa ni pamoja na uongozi wa soko hilo kuweka faini kubwa kukomesha tabia hiyo.

"Wanaotupa makopo yenye haja ndogo wakigundulika watozwe faini  ya elfu 50000 hadi 100000,hii ikichukuliwa Kwa umakini Kila mtu ataheshimu kanuni na taratibu zote za uhifadhi wa mazingira ikiwemo matumizi sahihi ya vyoo,kutupa taka kwenye vyombo maalum na kujizuia kabisa kutupa taka ngumu ovyo,"amesema

Nyeriga amesema ikiwa tabia hiyo itaendelea itahatarisha usalama wa afya za wanafunzi wa shule ya Sekondari Viwandani ambayo ipo jirani kabisa na eneo la Sabasaba.

"Eneo hili lipo jirani na wanafunzi,ambao mara nyingi hupita kununua mahitaji ikiwemo chakula,kuna wakati wanaokota chupa ambazo zimetumika kuhifadhi haja ndogo wananunulia juisi ni hatari lazima suala hili litafutiwe ufumbuzi la sivyo watoto wetu watapata magonjwa,"amesisitiza


Naye Katibu wa Soko hilo Nyamsuka Nyamsuka amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kwamba kama uongozi wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali kukomesha tabia hiyo ikiwemo kuwaelimisha wafanyabiasha hao namna ya usalama wa matumizi ya vyoo.

Amesema gharama zinazotozwa kwenye huduma za vyoo haziwezi kuwafanya wafanyabiasha hao kichukua hatua ya kujisaidia kwenye makopo na hivyo kuwashauri kuwa wastaarabu ili kuwaokoa wengine.

"Bei ya huduma za vyoo ni kubwa sababu vyote vinamilikiwa na watu binafsi,watu hawa wanatumia gharama kubwa za uendeshaji kupitia maji na huduma ya kunyonyaaji taka ambayo hufanyika kila mwezi,nashauri Serikali ingethubutu kuweka huduma hiyo ili kunusuru hii hali ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma za mitaro ya maji taka kwenye soko letu,"amesisitiza 
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post