RAIS SAMIA AZIDI KUONESHA HURUMA YAKE KWA WANANCHI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza na wananchi wa eneo la Pombe Shop Chamwino Morogoro usiku alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi tarehe 22 Sept 2023.

**********************

· Aelekeza wananchi waliovamia Bwawa la Mindu kupatiwa viwanja

· Waziri Slaa ahitimisha migogoro ya ardhi Morogoro usiku

Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza wananchi 357 wa kata ya Mindu mkoani Morogoro waliovamia eneo la hifadhi ya bwawa la Mindu mita 500 kupatiwa viwanja.

Uamuzi huo unafuatia mgogoro wa muda mrefu baina ya wananchi na serikali kufuatia Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kutaka wananchi hao kuondolewa ili kulinda chanzo hicho cha maji.

Akizungumza na wananchi hao tarehe 22 Septemba 2023 wakati wa akifuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Silaa amesema, madai ya wananchi kuwa umbali wa mita 500 ulioanishwa kulinda eneo la bwawa la Mindu hayana ukweli kwa kuwa lengo la serikali si kujipatia eneo bali kulinda chanzo hicho cha maji.

‘’Ingelikuwa tunapima halafu tunawaondosha wananchi na kugawana viwanja, kimoja RC, kingine DC na kamishna tungesema tunawabana ili tupate maeneo, tunapima kulinda bwawa ambalo mimi si mkazi wa eneo hili tunalinda bwawa hili kwa faida wa wana morogoro mkiwemo ninyi’’ alisema.

Akielezea zoezi la uthamini lililofanyika, Waziri Silaa amesema hilo lilikuwa zoezi maalum ambalo lilibaini wananchi walioko ndani ya mita 500 wako kwenye eneo la hifadhi la bwawa la Mindu na kubainisha kuwa hapo ndipo linapokuja suala la haki halali na ile haramu.

‘’Fidia ya hapa si fidia ya compasation iliyotokana na mtu aliyechukuliwa ardhi yake yenye mali ndani yake bali ni fidia iliyotokana na busara, hekima na huruma ya Rais. Tungelifuata Maamuzi ya Baraza la Mawaziri la tarehe 23 Sept 2019 maana yake mkuu wa wilaya angeagizwa kufikia tarehe fulani kila mtu aondoke’’ alisema Silaa.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, fidia kwa wananchi waliovamia eneo la hifadhi ya bwawa la Mindu haipo lakini kwa mujibu wa wataalamu wa ardhi wananchi 357 ndiyo wanaopaswa kulipwa kifuta jacho ikiwa ni huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kama mkono wa heri kuwasaidia kuhamisha mali zao.

Hata hivyo, alisema baada ya kufanya mawasiliano na Rais Samia Suluhu Hassan alimuelekeza amuambie Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro awapatie viwanja wananchi wanaopisha uhifadhi wa eneo la bwawa ili waweze kujenga nyumba za kuishi.

Awali Diwani wa Kata ya Mindu mkoani Morogoro Zuberi Mkalaboko alimueleza Waziri wa Ardhi kuwa, wananchi wa eneo hilo hawana tatizo la kupisha uhifadhi wa bwawa isipokuwa kero zao kubwa ni tatu alizozitaja kuwa, ni ushirikishwaji, vipimo vilivyofanywa na wataalamu wa ardhi pamoja na fidia wanayotaka kulipwa wananchi hao.

‘’Mhe Waziri, kero za wananchi wa Mindu ni maeneo matatu, kwanza ushirikishwaji, pili fidia inayolipwa na tatu vipimo vilivyofanywa na wataalamu hawa’’ alisema Diwani Mkalaboko.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mbali na kutembelea eneo la Mindu na CCT-Forest alihitimisha ziara yake ya siku moja mkoani Morogoro kwa kutembelea kata ya Chamwino eneo lenye mgogoro la Pombe Shop ambapo ilimlazimu kuutatua mgogoro wa eneo hilo usiku ambapo aliuhitimisha kwa kumuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro kuwatafutia viwanja wananchi 57 kuondoka kwa hiari kupisha ujenzi wa shule.

‘’Tumekaa hapa mpaka usiku kuhangaikia watoto wenu, eneo hili lilikuwa la umma na litaendelea kuwa la umma’’ alisema Silaa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akimsikiliza mmoja wa akina mama alipokwenda kusikiliza na kutatua mgogoro katika eneo la uhifadhi wa bwawa la Mindu Morogoro tarehe 22 Sept 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (anayenyoosha mkono) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima (wa tatu kulia) eneo la Pombe Shop alipokwenda kusikiliza na kutatua mgogoro wa ardhi tarehe 22 Sept 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akimsikiliza mwananchi katika eneo la Pombe Shop alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi tarehe 22 Sept 2023.
Sehemu ya wananchi wa eneo la Pombe Shop Chamwino Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Mhe Jerry Silaa usiku alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi katika eneo hilo tarehe 22 Sept 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akiangalia moja ya nyaraka za mwananchi alipotembelea ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro tarehe 22 Sept 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post