PROF.KUSILUKA ASHAURI JAMII KUONA UMUHIMU WA KUTUNZA MAARIFA ASILIA KWA VIZAZI VIJAVYONa Dotto Kwilasa, DODOMA

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)Prof.Lughano Kusiluka  ameishauri Jamii kuona umuhimu wa kuhifadhi maarifa asili kwa kuweka kumbukumbu za mila na desturi za Kiafrika kwa faida ya vizazi vijavyo hali itayosaidia kukuza utalii wa kitamaduni kwa kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya bara la Afrika. 

Prof.Kusiluka ameeleza hayo leo September 4,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye Warsha ya watafiti wataalam wa kuhifadhi maarifa asili kutoka nchi tisa yenye lengo la kubadilishana uzoefu wa kuhifadhi kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Miongoni mwa nchi hizo ni pamoja na Ujerumani, Ethiopia,Msumbiji,Kongo, Tanzania,Kenya na Zimbabwe..

Amesema ikiwa jamii itaweka kumbukumbu za mila na desturi za Kiafrika kwa njia ya hadithi, nyimbo, na ngonjera,kumbukumbu hizo zitasaidia vizazi vijavyo kuelewa na kuheshimu urithi wa mwafrika na kujifunza  kuelewa kalenda za Kiafrika na matukio ya kihistoria yaliyotokea katika bara letu.

"Vijana watanzania wanatakiwa kujua kuwa wanaishi katika bara tajiri lenye historia ndefu, na ni muhimu kuelimisha na kuenzi historia hii,ni muhimu vijana wetu wakajifunza kuhifadhi kumbukumbu,na ndiyo maana UDOM kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cologne kilichopo Ujerumani tumewakutanisha watafiti hawa kutoka nchi tisa duniani kuona namna ya kubadilishana uzoefu na uhifadhi kumbukumbu,"amesema.

Akizungumza kuhusu warsha hiyo Prof.Lughano Kusiluka amesema Warsha hiyo ina matarajio makubwa katika kusaidia kuhifadhi maarifa asilia ambayo kwa namna moja au nyingine yameanza kusahaulika kutokana na jamii kujikita zaidi katika elimu ya magharibi.

"Warsha hii itasaidia kuibua hisia za wataalam katika uhifadhi wa tamaduni na urithi wa Kiafrika,tunajua kuwa tamaduni na urithi wetu ni muhimu sana katika kujenga utambulisho wetu na kukuza maendeleo yetu kama bara hivyo ni muhimu kuelewa na kuhifadhi maarifa ya asili ya Kiafrika ili tuweze kuendeleza urithi wetu kwa vizazi vijavyo,"amefafanua

Prof.Kusiluka ametaja  mikakati ya kufanikisha hilo kuwa ni pamoja na kufanya utafiti na kukusanya maarifa ya asili ya Kiafrika kutoka kwa wazee  na jamii za asili na kwamba hiyo itasaidia kuhifadhi maarifa na desturi ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu.

Aidha ameeleza maono ya UDOM kwa miaka ijayo kuwa  Chuo hicho kinatarajia kulitumia Jengo la Chimwaga kama hifadhi ya lugha asili za Tanzania na tamaduni mbalimbali jambo litakalo wavutia wengi na kuwa kivutio cha utalii ikiwa ni pamoja na kutumika kufundishia watafiti wa PhD kuhusu maarifa na elimu ya asili.

Amesema Jengo hilo la Chimwaga ambalo lilianza kutumika kama chuo limebeba historia ya UDOM hivyo uhifadhi wake utategemea teknolojia ya kisasa kama vile video na mitandao ya kijamii kueneza maarifa ya tamaduni na urithi wa watanzania na kuwafikia watu wengi zaidi na kujenga ufahamu kuhusu asili.

"Kupitia uhifadhi huu tunategemea kuwashirikisha vijana wetu katika shughuli za kijamii ambazo zinahusisha tamaduni na urithi wa Kiafrika na Kuwafundisha na kuwahusisha vijana wetu kutahakikisha kuwa maarifa haya hayapotei,"amesisitiza Prof.Kusiluka.

Naye mmoja wa washiriki katika warsha hiyo ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu(PhD)Adriano Utenga amesema maarifa ya watu yanatunzwa na watu wenyewe hivyo kutoa wito kwa watanzania kuungana na nchi nyingine za Kiafrika kwa njia ya ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa ili kudumisha umoja  na kulinda tamaduni zetu. 

"Tunapaswa kuwa wamoja na kuweka maslahi ya bara letu mbele,asili yetu ni utajiri,sisi wataalam tunapaswa kutumia nguvu zetu kuamsha ari ya jamii kutunza maarifa asilia,"amesema.

Huku akitumia mfano wa nchi za Ghana na Senegal ambazo zimefanya jitihada kubwa za kuhifadhi tamaduni na urithi wao, Utenga amesema Tanzania inawezĂ  kujifunza kutoka kwao na kutekeleza mikakati sawa nchini ikiwa ni pamoja na kukuza utalii wa kitamaduni kwa kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya bara la Afrika. 

"Utalii huu utasaidia kuongeza mapato na kukuza ufahamu kuhusu tamaduni zetu na urithi wetu,Kwa ujumla tuna jukumu la kuwafundisha na kuwahamasisha watu wetu ili waweze kuchukua hatua,tuwaelimishe watu wetu juu ya thamani ya tamaduni na urithi wa Kiafrika,tuwahimize wawe na fahamu na kuenzi tamaduni zetu kwa kujifunza lugha zetu, kuvaa mavazi yetu ya asili, na kushiriki katika shughuli za kitamaduni,"amesisitiza.


Mwishoo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post