LATRA YAASWA KUSHIRIKISHA WADAU ZAIDI MATUMIZI YA MFUMO WA KUFUATILIA MWENENDO WA MABASI-VTS


Na Mwandishi wetu - Dar es Salaama


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe Suleiman Kakoso ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini-LATRA kushirikisha wadau zaidi juu ya matumizi ya Mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa mabasi (VTS)
Mhe kakoso ameyasema hayo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea , kukagua na kujifunza jinsi mfumo wa ufuatliaji wa mwenendo wa mabasi (VTS) uliopo kwenye ofisi ndogo za LATRA Mikocheni Jijini Dar es salaam unavyofanya kazi ambao kwa sasa unawashirikisha Jeshi la Polisi na wamiliki wa mabasi.

Mwenyekiti Kakoso ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Latra kushirikisha zaidi Wizara na taasisi ambazo ni mtambuka kwenye jambo hili kama vile Wizara ya katiba na Sheria,Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Mawasiliano naTeknolojia ya Habari na taasisi za TCRA, Mamlaka ya Serikali Mtandao(EGA) na wamiliki wa mabasi na malori kupitia vyama vyao vya TABOA na TATOA ili kujenga uelewa wa pamoja na kuanza kutumia mfumo huu.


“Uwekezaji uliofanyika hapa ni mkubwa,ili mfumo huu uweze kuwa na ufanisi na kuleta tija kwa Taifa inabidi wadau wote wa usafiri na usafirishaji, teknolojia na usalama waanze kutumia mfumo huu uliobuniwa na LATRA ili kuweza kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa urahisi maana ni mfumo mzuri na tangu uanze kutumika umeweza kupunguza sana ajali zilizokuwa zinatokea mara kwa mara” amesisitiza kakoso


Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua tena na sasa kuwa Waziri wa Wizara ya Uchukuzi ambayo inategemewa sana kuinua uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa madhumunu makubwa ya ziara ya kamati ya miundombinu kwenye ofisi za latra ni kuja kujifunza shughuli zinazofanyika hapo zikiwemo za udhibiti wa usafiri wa nchi kavu kwa njia ya barabara na reli ili kuhakikisha usalama wa vyombo vinavyosafiri na abiria kwa masaa 24.


“Tumepokea maoni na mapendekezo yote ya kamati na Serikali inakwenda kuyafanyia kazi kwa wakati ili kuhakikisha tunadhibiti kwa lengo la kuongeza uchumi kwenye sekta ya usafirishaji wa nchi kavu, kama kuna kanuni au sheria zozote zinazohitaji mabadiliko au maboresho Latra waniandikie na mimi niko tayari nitazipitisha na kuziwasilisha Bungeni kwa ushauri na mapendekezo zaidi ili zianze kutumika mara moja ili kuhakikisha usalama wa vyombo vyetu, wananchi na mali zao na hii itasaidia kuvuta uwekezaji zaidi kwenye sekta ya usafirishaji na kuongeza pato la Taifa”, amesisitiza prof Mbarawa.


Awali Mkurugenzi Mkuu wa Latra CPA Habibu Suluo ameishukuru Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kufanya Ziara ya kujifunza kwenye ofisi za Latra na kusema kuwa mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa mabasi-vts ulianza toka mwaka 2010 na kupitia mabadiliko mbalimbali mpaka sasa wameanza rasmi kutumia VTS ambapo mfumo huo umeonesha ufanisi mkubwa licha ya kuwepo kwa changamoto za rasilimali watu, baadhi ya wadau kufanya hujuma na changamoto za ukusanyaji wa faini pindi makosa yanapobainika kupitia mfumo huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post