USHIRIKIANO TANZANIA, MAREKANI KUIMARISHA SEKTA YA MADINI


#Marekani kuipa Kipaumbele Sekta ya Madini nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amekutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka Ubalozi wa  Marekani nchini katika ziara iliyolenga  kuzungumzia masuala mbalimbali katika shughuli za uchimbaji na maendeleo ya Sekta ya Madini,  Mji wa Serikali jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Septemba 7, 2023, Katibu Mkuu Mahimbali amesisitiza kuimarisha ushirikiano  katika uchimbaji wa madini hususan ya kimkakati, kujengewa uwezo wataalam mbalimbali wa Sekta ya Madini ili mnyororo mzima wa shughuli za madini unufaike.

Amesema kuwa Wizara ya Madini imeweka vipaumbele katika maeneo manne ili kuimarisha zaidi Sekta hiyo, maeneo hayo ni pamoja na Utafiti wa kina, maendeleo ya rasilimali watu, ushirikiano  sambamba na KanziData ya Madini.

Aidha, amesisitiza kuwa milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini ipo wazi kwa nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye kipaumbele ili nchi zote zinufaike na uwepo wa madini hayo.

Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Kiuchumi  kutoka Ubalozi wa Marekani nchini, Jonathan Howard amesisitiza kuwa, nchi yake itashirikiana na Tanzania katika shughuli za Sekta ya Madini hususan katika kujengeana uwezo na ujuzi, fedha na teknolojia.

Vile vile, Howard ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya kumteua na kumuapishwa Mhe. Antony Mavunde kuwa Waziri wa Madini. Wamesema nchi yao itampatia ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kuiongoza Sekta ya Madini.

Ameongeza kuwa wanatarajia kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika  Madini  linalotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26, 2023 jijini Dar es Salaam. 

Pia, amepongeza juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuvutia wawekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi inayochochea maendeleo na uchumi kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post