THAILAND YAFUNGUA MILANGO WATANZANIA KUJIFUNZA UONGEZAJI THAMANI MADINI



*Kampuni Kubwa Yenye Uzoefu wa Miaka 50 Yaonesha Nia Kuwekeza Nchini

*Mbibo Aielezea kuwa ni Safari Yenye Manufaa Makubwa kwa Tanzania

*TIC  Wakaribishwa Kuanzisha Tawi  Kuchochea shughuli za Uongezaji Thamani Madini

Bangkok- Thailand

Watanzania wamekaribishwa kujifunza namna ya kuongeza Thamani Madini ya Vito kwa Kuzingatia  Ubora  na Viwango  vya  Juu  vya Kimataifa  unaoweza kutumiwa na  Chapa Kubwa  Duniani.

Hayo yamebainishwa  wakati  Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Madini Msafiri Mbibo ulipotembelea kiwanda kikubwa cha Pranda Jewelry Public Company Ltd, kilichopo Bangkok nchini Thailand  chenye uzoefu wa miaka 50 katika shughuli za uongezaji thamani madini ya vito huku  kikiongozwa na kauli mbiu (motto) inayozingatia ubora  katika tasnia hiyo ndogo.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Makamu wa Rais na Mwanzilishi wa Kiwanda hicho Bibi. Ratchnee Sapranda ameeleza kuwa kutokana na uzoefu wa miaka mingi, anawakaribisha watanzania kujifunza, kupeleka madini ghafi katika kiwanda hicho kwa ajili ya kuongezwa thamani kwa ubora wa juu kufuatia ujuzi na utalaam walionao katika eneo hilo na kusisitiza kwamba, kama kampuni wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuanzisha kiwanda cha uongezaji thamani madini nchini, kuwekeza au kutuma wataalam wake ili kubadilishana ujuzi, maarifa na utaalamu.

‘’ Tuna uwezo wa kukata madini katika maumbo mazuri ya aina mbalimbali, kwa rangi nzuri za kuvutia na kuzingatia ubora unaotakiwa kimataifa kwa sababu hii ndiyo shabaha yetu kubwa tunayoisimamia katika kuongeza thamani ya madini na hii ni sababu tunasema, Thailand ni kitovu cha shughuli za uongezaji thamani,’’ amesisitiza Sapranda.

Aidha, Bibi, Sapranda amesema asilimia 75 ya bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho zinauzwa katika nchi ya Marekani na asilimia 25 nchi za Ulaya na kuongeza kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikipata maombi ya kutengeneza vito na mapambo ya aina mbalimbali kutoka chapa kubwa duniani ambapo nchi kadhaa zikiwemo za Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu, China, India, Japan, Ufaransa na nyingine ikiwemo baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa zikitumia bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda hicho.

Ameongeza kuwa, kampuni ya Pranda ni kampuni pekee miongoni mwa kampuni zinazohusika na masuala ya uongezaji thamani madini iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa  nchini humo na ikiwa  imeajiri takriban wafanyakazi 1,800.

Katika hatua nyingine, ujumbe huo umepata fursa ya kutembelea kiwanda cha Mfanyabiashara wa  Madini  na mmiliki wa kiwanda kidogo cha uongezaji thamani madini cha Sunset  Pukkapon Piantumdee. Akizungumza na ujumbe huo, ameeleza kuwa wataalam wa Tanzania wanaweza kupata uzoefu kwa kutumia mashine rahisi kama anazotumia kuongeza ubora wa madini.

 Ameongeza kwamba, yuko tayari kutoa nafasi tano kwa watanzania kujifunza kupitia teknolojia inayotumiwa na kiwanda chake ikiwa Serikali itakuwa tayari kushirikiana ili kuboresha ubora wa madini na kuongeza kwamba, amekuwa na uzoefu wa kufanya kazi na Tanzania tangu mwaka 2011 ambapo alijihusisha na ununuzi wa madini ya Tanzanite na kisha kuhamia katika Sapphire  ya Tunduru.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Mbibo akizungumza baada ya ziara hiyo, amesema kwa  Tanzania, ziara hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa kutokana na wadau mbalimbali kuonesha dhamira ya wazi ya kushirikiana na Tanzania kuendeleza sekta ndogo ya uongezaji thamani madini.

Amesema ni mapokeo mazuri  na tayari kiwanda cha Pranda tayari  kimeanza kushirikiana na Serikali  na  kina mchango katika eneo hilo baada ya kutoa nafasi kwa wakufunzi kutoka Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kujifunza ili kupata uzoefu, ujuzi, maarifa  na namna ya matumizi ya teknolojia za kisasa na kuongeza kwamba, kiwanda hicho kimeonesha tena utayari wa  kuiwezesha Tanzania kutuma wataalam wengine kujifunza .

‘’Ni watu ambao wanatumika na chapa mbalimbali kutoka Amerika, Italia, Dubai na kwingineko duniani. Hii imetufundisha hata sisi tunaweza kutengeneza bidhaa zetu kwa kutumia chapa hizi,’’ amesema Mbibo.

Ameongeza kwamba, kupitia ziara hiyo, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepata wasaa wa kuzungumza na Mwekezaji wa  kampuni ya Pranda ambapo mwekezaji huyo ameshauri TIC  kuanzisha tawi lake nchini Thailand ili kuwawezesha Watanzania kufahamu fursa za kiuwekezaji zinazopatikana nchini Thailand  vilevile raia wa Thailand na nchi nyingine za Asia kuweza kupata huduma  zinazohusu uwekezaji nchini Tanzania.

Aliongeza kwamba, hilo litachangia kufungua fursa zaidi za kiuwekezaji  na kuchochea ukuaji wa shughuli hizo nchini Tanzania.

‘’Tutakaporudi  tutaendelea kuwasiliana nao  kuona ni  jinsi gani kama watakuwa tayari waje kuwekeza Tanzania na wawaajiri Watanzania ili  kuwawezesha watanzania kujua namna ya kuongeza thamani madini  na kujua namna ya kufanya biashara ili kuongeza uchumi wa nchi na kubadili maisha ya watu,’’ amesititiza Mbibo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post