BIBI MBARONI TUHUMA ZA KUMUUA MJUKUU WAKE KWA KUMLIMA JEMBE KICHWANI


Na Joachim Nyambo, Mbeya.


MWENYEKITI wa Kijiji cha Ikoho kilichopo wilayani Mbeya, Ezekia Walonde amethibitisha kuwa mwili wa mtoto, Vision Eriki aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu aliyepoteza maisha baada ya bibi wa mama yake kumkata na jembe kichwani ulizikwa jana(Septemba 1) majira ya saa tisa alasiri.

 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mtoto Vision aliyekuwa  mkazi katika Kitongoji cha Mapinduzi kilichopo Kijiji cha  Ikoho, Kata ya Maendeleo wilayani Mbeya amezikwa katika kitongoji cha Irea kilichopo kijijini Ikoho.

 

Awali Jeshi la polisi mkoani Mbeya liliwaambia waandishi wa habari kuwa mtoto huyo alipoteza maisha baada ya kukatwa sehemu ya kichwa chake kwa jembe na bibi wa mama yake.

 

Kikongwe aliyepelekea kifo cha mtoto huyo alitajwa kwa jina la Malogi Mwaihoyo(75) mkulima na mkazi katika kijiji cha Ikoho kilichopo wilayani Mbeya mkoani hapa.

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga mauaji hayo yalitokea Agosti 31 mwaka huu majira ya saa nne na nusu asubuhi katika Kitongoji cha Mapinduzi Kijiji cha  Ikoho, Kata ya Maendeleo iliyopo kwenye Tarafa ya Tembela wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi iliyopo Mbeya Vijijini.

 

Kamanda Kuzaga alisema  asubuhi hiyo bibi huyo aliamkia kazi ya kuchimba udongo kwaajili ya maandalizi ya kukandika nyumba yake ili kuiweka katika mazingira nadhifu kama inavyofanyika kwa nyumba nyingine hususani zinazomilikiwa na watu walio na kipato cha chini kijijini hapo.

 

Alisema wakati kikongwe huyo akiendelea kusafisha eneo kwa kutumia jembe hata kabla ya kuanza kuchimba udongo ghafla alisikia sauti na mtoto mdogo akilia kwa nguvu baada ya kushusha jembe ardhini ikiwa ni mwendelezo wa kuendelea kusafisha eneo hilo.

 

Kamanda Kuzaga alisema pasipo kujua wakati kikongwe huyo akiwa anaendelea na kazi yake mjuu wake alikuwa amekwisha tambaa akimfuata hadi eneo alilokuwa akiendelea na kazi na ndipo alijikuta amemshushia jembe kichwani na kumfanya apoteze uhai wake.

 

Alifafanua kuwa uchunguzi wa awali ulionesha bibi huyo ana tatizo la uoni hafifu yani akikabiliwa na upofu hivyo kwa haraka hakuweza kujua pale chini kuna nini na ndiyo sababu hata aliposikia sauti alilazimika kuuliza watu waliokuwa jirani kuwa kulikuwa na nini na ndiyo waliomwambia amemkata mjukuu wake na amefariki.

 

Alisema kikongwe huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi  wakati taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kufanyika huku akiisihi jamii kuhakikisha inatekeleza jukumu la Ulinzi na Usalama wa watoto wadogo kama inavyoelekezwa katika Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto( PJT-MMMAM) inayoendelea kutekelezwa nchini.

 

“Tunaona kabisa kwamba huyu mtoto wa mwaka mmoja na miezi mitano ameachwa kwa bibi ambaye naye bibi huyu  ana matatizo ya macho yaani uoni hafifu. Ameachwa kwake  bila msaada wowote na mzazi  ameondoka kwenda kwenye shughuli nyingine. Nitoe wito kwa hawa wazazi wa  hawa watoto vikongwe wasiwaachie hawa vikongwe kuwalelea watoto.”

 

“Tunaona haya madhara yaliyotokea, bibi hana nguvu ya kuweza kummudu huyu mtoto kulingana na pilika zake katika haya makuzi anayopitia mtoto kwa sababu anakuwa na mambo mengi…anakwenda huku na kule…anatambaa huku na kule. Kwa hiyo bibi anashindwa hivyo wale wote ambao wanawaachia akina bibi wawalelee watoto waache.” Liongeza Kamanda Kuzaga.

 

Kamanda huyo alisema kumekuwepo na matukio mengi yatokanayo na vikongwe kuachiwa watoto wadogo kuwalea yakiwemo ya kutumbukia kwenye visima vya maji na kusisitiza kuachana na tabia hiyo kutaepusha madhara kama hayo na kuifanya jamii ya watoto wadogo kuwa salama.

 

Lakini Mwenyekiti wa Kijiji alipozungumza na mwandishi wetu alisema wakati tukio linatokea mama wa mtoto aliyemtaja kwa jina la Gwila Hamis alikuwa amefuata maji kwaajili ya kuja kupondea udongo wa kusiriba ndani ya nyumba ya bibi yake kwakuwa ilichakaa hivyo alifunga safari kutoka kwake kuja kumsaidia bibi yake kazi hiyo.

 

Walonde alisema tukio hilo ni la kwanza kuwahi kutokea kijijini hapo na kutokana na hali ya maisha ya kikongwe huyo baada ya tukio wanakijiji wote wamenahuzunika na kumhurumia bibi huyo aliyesema hana matatizo na mtu.

 

Alisema kutokana na hali yake duni ya maisha kijiji na halmashauri walimuwezesha kuwa miongoni mwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya masikini wa Tasaf na kutokana na uoni hafifu wake wakati wa ujazaji wa nyaraka mbalimbali za mpango huo ililazimika awepo mtu wa kumjazia.

 

“Hata alipolazimika kuja siku za kuja kuchukua fedha au kujaza fomu za wanufaika wa Tasaf mimi mwenyewe huwa nalazimika kumsaidia kujaza akiingia ofisini haoni kabisa.” Alisema Mwenyekiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post