VIJANA WA AFRIKA WAJIBIWA NA SAMIA MASWALI YANAYOWATATIZA

Na Nyabaganga Daudi Taraba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehutubia mkutano wa vijana wa Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere mapema hii leo tarehe 7 Septemba 2023 jijini Dar es Salaam.

Akijibu maswali ya vijana katika mkutano huo kuhusu masoko ya mazao ya kilimo, Rais amesema, serikali inafanya utafiti juu ya mambo mawili yenye utata. Moja ni kujua mahitaji ya kila mahali (soko) ili kujua nini hasa kinahitajika ili ndicho kizalishwe.

Aidha, amesema jambo la pili linalofanyiwa utafiti ni jinsi ya kuunganisha wakulima na soko, jambo ambalo amesema linatekelezwa kwa baadhi ya mazao na kuonesha mafanikio. 

Akitoa mfano wa mazao yaliyofanikiwa, alisema mazao ya korosho, ufuta na mbaazi yameuzwa kupitia ushirika na mafanikio ni mazuri ikilinganishwa na miaka 2-3 iliyopita.

 Amesema, kwa mfano, mbaazi mwaka jana kilo moja iliuzwa kwa shilingi mia tatu (300), lakini kwa mfumo huo wa ushirika na stakabadhi ghalani, mwaka huu kilo hiyo hiyo imeuzwa kwa shilingi 2,000 na zaidi.

Akijibu swali lingine kuhusu jinsi ICT itakavyosaidia vijana katika kilimo, Rais amesema teknolojia haiepukiki. Kwamba tayari inatumiwa na maafisa ugani ambao wanapata taarifa za udongo na tafiti mbalimbali kwa kutumia ICT.

 “Kilimo ni kujua taarifa zake, ndiyo sababu tunatambua taarifa za afya ya udongo”, amesema Rais Samia. Kutambua wakulima na eneo wanalolima, haya yote yanafanyika kwa mfumo wa ICT.

“Tumewekeza kwenye vituo vya utafiti na taasisi ya uzalishaji wa mbegu. Lengo likiwa ni kupata ¾ ya mbegu za mazao yanayolimwa hapa nchini zipatikane hapa nchini”.

ICT pia inatumika katika umwagiliaji wa mimea kutoka kwenye mfumo wa kupeleka maji mengi yasiyohitajika. Sasa tutapeleka kiwango tu cha maji yanayotosha tu na kutegemea aina ya udongo. Vilevile hata kwenye vihenge, vifaa vya kudhibiti unyevunyevu vimefungwa.

Akijibu swali ni kwa jinsi gani programu ya BBT inaweza kuonesha kuwa imefanikiwa, amesema:

Kwanza ni idadi ya vijana walioingia na waliovutika kwenye programu hiyo.

Pili, matumizi ya mbolea, ongezeko hilo ni dhahiri kuna mafanikio.

Tatu, uzalishaji kuongezeka ni kiashiria kuwa kuna mafanikio.

Nne, ustawi wa maisha ya vijana, ambalo ndilo lengo kuu, ni kiashiria.

Tano, bei ya chakula katika soko kuwa nzuri kwa mlaji na muuzaji ni kiashiria kingine cha mafanikio.

Akiongelea Uchumi wa Bluu, amesema ni jambo geni kwa upande wa Tanzania Bara, ila kwa Tanzania Visiwani siyo geni. Kuna mambo yanayofanyika huko. Mfano, kilimo cha mwani ambao unasafirishwa nje ya nchi na mwingine unazalisha bidhaa mbalimbali hapa nchini.

Aidha, amesema baadhi ya viumbe waliokuwa wamepotea baharini wamerejeshwa kwa kupitia chuo cha utafiti cha Marine Institute. Viumbe kama majongoo na chaza ambaye anatoa vito, wamerejeshwa.

Amesema suala la Uchumi wa Bluu ni pana na kwa sasa linaandaliwa sera ili liweze kuwa la manufaa kwa vijana na watu wengine hata upande wa bara.

Amesema nchi imeweka agenda ya kutekeleza BBT, kushawishi vijana kwa kuwawezesha mtaji na ardhi ili wawe na uzalishaji wa faida.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ya Tanzania waliohudhulia mkutano wa AGRF 2023.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post