WANAFUNZI WAHIMIZWA KUPENDA MASOMO YA SAYANSI

Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula akikabidhi majarida ya OYLA Africa kwa wawakilishi wa wanafunzi wa shule zilizopokea msaada wa majarida hayo kutoka kampuni ya Baobab Shalom Limited katika hafla fupi iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato Jijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.

****************

Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula amewahimiza wanafunzi wa kitanzania kupenda masomo ya sayansi na teknolojia kutokana na mchango wake katika kuleta maendeleo ya nchi.

Prof. Kipanyula amesema Sayansi na Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa kitaifa na kimataifa na hasa katika sekta za elimu, habari, biashara na huduma mbali mbali za kijamii.

Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika sekta ya elimu ambapo imewekeza kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hivyo kuwahamasisha wanafunzi kujifunza kwa bidii na kuwa wabunifu.

Alikuwa akizungumza katika hafla fupi ya kugawa majarida 700 yanayofahamika kama OYLA Africa ambayo yametolewa na kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam kufuatia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov katika ofisi za TEA jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.

Bw. Semikov amesema lengo la Majarida hayo ni kuwezesha wanafunzi wanaoyatumia kuwa wabunifu na wadadisi kwa lengo la kuboresha mazingira na maisha yao kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye ameshukuru kampuni ya Baobab Shalom Limited kwa kutoa msaada huo wa majarida kupitia Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na TEA na kuongeza kuwa TEA iko tayari wakati wote kushirikiana na wadau wa elimu na kuwahakikishia kuwa misaada ya elimu inayopita kwenye Mfuko wa Elimu wa Taifa inasimamiwa kikamilifu na kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov (wa pili kushoto) wakisaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa ajili ya kugawa majarida 700 ya OYLA Africa yanayohimiza wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati katika hafla fupi iliyofanyika jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov (wa pili kushoto mstari wa mbele) baada ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa ajili ya kugawa majarida 700 yanayohimiza wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati katika hafla fupi iliyofanyika jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.
Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula ( wa pili kulia mstari wa mbele) akipokea jarida la OYLA Africa kutoka kwa Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov (wa pili kushoto). Majarida hayo yanalenga kuhimiza wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato ya jijini Dodoma walioshiriki hafla ya kupokea Majarida ya OYLA Africa kwa ajili ya kuhimiza wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati yaliyotolewa na Kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi wakiwa wameshika magazeti ya OYLA Africa yaliyotolewa Kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post