WAMILIKI WA MAKAO YA WATOTO WATAKIWA KUFUATA TARATIBU ZA UENDESHAJI
Na WMJJWM, DSM

Wamiliki wa Makao ya watoto wametakiwa kuhakikisha wanatoa huduma kwa mujibu wa sheria na kanuni na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana kwa ajili ya kusaidia watoto zinatumika kikamilifu kwa maendeleo na ustawi wa watoto.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua Mkutano wa Wamiliki wa Makao ya Watoto Mkoa wa Dar es Salaam Agosti 04, 2023.

Dkt. Gwajima amebainisha kwamba, pamoja na makao mengi kufanya kazi nzuri na kwa uwazi, baadhi yamekuwa yakikusanya rasilimali na kujinufaisha wao zaidi kuliko walengwa ambao ni watoto walioko kwenye vituo hivyo huku wamiliki wa baadhi ya makao hayo wakiwazuia na kuwapa vitisho Maafisa Ustawi wa Jamii pale wanapofika kwenye makao hayo kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa utoaji wa huduma.

"Jambo hilo ni kosa kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 146 (2) (c) na adhabu yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua milioni 2 na isiyozidi milioni 10 au vyote viwili na pia ofisi ya msajili inaweza kufuta leseni ya kumiliki makao” ” Dkt. Gwajima.

Amewataka wamiliki wa makao hayo kuwaruhusu bila vipingamizi Maafisa Ustawi wa Jamii kuingia makaoni na kufanya ukaguzi wakati wowote inapohitajika.

Akisisitiza kuhusu hatma ya huduma kwa mtoto aliyeko kwenye makao, Dkt. Gwajima amesema kila mmiliki wa makao anatakiwa kuhakikisha watoto anaowalea wananufaika na huduma za makao na kuandaliwa kuunganishwa na familia au jamii kupitia Malezi ya Kambo au Kuasiliwa na au kuwezeshwa kujitegemea kwa wale waliofikia umri na kujengewa uwezo.

Aidha, Dkt. Gwajima ametoa siku 90 kwa wamiliki wa makao ya watoto kote nchini kuhakikisha wanahuisha Kamati za Makao na miezi sita kwa kila mwenye makao kuwa amekamilisha taratibu zote za umiliki na uendeshaji wa makao, vinginevyo wawasiliane Wizara moja kwa moja iwapo watakumbana na changamoto.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amewapongeza na kuwatia moyo wanaoendesha Makao ya Watoto kwa kufuata taratibu za uendeshaji na kuongeza kuwa, Wizara inakamilisha Mapitio ya Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Makao ya Watoto na inatarajia kutoa toleo jipya Septemba 2023, ili kuimarisha ulinzi wa watoto kwa kila nyanja.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesisitiza wamiliki wa vituo hivyo kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usajili na uendeshaji wa makao na kwamba, wizara itaimarisha ufuatiliaji wa makao yote nchini ambayo kwa sasa yako jumla 431 huku 58 yakiwa mkoa wa Dar es Salaam.

Nao wamiliki wa makao ya watoto mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw. Evans Tegete, wamesema wamepongeza juhudi za Serikali za kuwa na jukwaa la pamoja la mawasiliano na Serikali ambalo litawasaidia kwenda pamoja kwenye kuboresha hatua za maendeleo na ustawi wa watoto wa kwenye makao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post