TARULA KUFANYIA MATENGENEZO YA BARABARA

 

Na Dotto Kwilasa,  Dodoma 

Jumla ya barabara zenye km 21,057.06 zitafanyiwa matengenezo Kwa mwaka wa fedha 3023/2024,huku km 427 zitajengwa kwa kiwango cha lami, km 8,775.62 zitajengwa kwa kiwango cha changarawe, madaraja na makalavati 855 yatajengwa na mifereji ya mvua km 70.

Hayo yameelezwa leo Agosti 24,2023 jijini Dodoma na  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Victor Seff wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa Wakala umekwisha tangaza kazi za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara zaidi ya asilimia 60 ya mpango wa mwaka 2023/24 ambapo baadhi ya kazi utekelezaji umeanza. 

Amesema kuwa jumla ya bil. 858.517 zimeidhinishwa kwa ajili ya Ujenzi, Ukarabati na Matengenezo ya Miundombinu ya barabara za Wilaya, ambapo kati ya fedha hizo, bil. 710.31 ni fedha za ndani na bil. 148.207 ni fedha za nje kupitia miradi ya RISE, TACTIC, Bonde la mto Msimbazi na Mradi wa Agri connect.

Pamoja na hayo Injinia huyo alisema mojawapo ya kipaumbele cha TARURA ni kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi.

 Madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 92, Singida 24, Tabora 5, Kilimanjaro 10, Mbeya 2, Arusha 6, Mrorgoro 2, Rukwa 3, Pwani 1, Ruvuma 3 na Iringa 15.

Ameongeza kuwa wanaendelea kufanya majaribio ya tekinolojia mbalimbali ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka maeneo mengine ya mbali.

" Tekinologia hizo ni pamoja na ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer. Hadi sasa kwa kutumia Teknologia ya ECOROADS Katika Jiji la Dodoma imejengwa km 1 ambayo imekamilika na Katika Wilaya ya Mufindi zitajengwa km 10 na Mkandarasi yuko kwenye matayarisho ya kuanza kazi" amesema.

Kuhusu utekelezaji wa kazi za ujenzi na matengenezo kwa mwaka wa fedha 2022/23 amesema umefikia asilimia 85  hadi kufikia mwezi Juni 2023 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 743.405  sawa na asilimia 89 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 598.81 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 144.593 ni fedha za nje.

Hata hivyo Mtendaji Mkuu huyo amesema kupitia fedha za ndani, jumla ya kilomita 22,523.51 zimefanyiwa matengenezo (utunzaji wa barabara), ujenzi wa barabara  kwa kiwango cha lami kilomita 249.74, ujenzi wa barabara kwa  kiwango cha changarawe kilomita 9,761.01, Ujenzi wa madaraja na makalavati 463 pamoja na ujenzi wa mifereji ya kuondoa maji barabarani kilomita 64.47.5

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post