KAYANDABILA AMSHUKURU RAIS SAMIA KUTOA FEDHA ZA UJENZI MIUNDOMBINU YA ELIMU KIDATO CHA TANO


MKURUGENZI wa Manispaa ya Tabora Elias Mahwago Kayandabila akizungumza na mmoja wa Wanafunzi shule ya Sekondari Kazima mara baada kuwapokea wanafunzi hao wa kidato cha tano kwenye mabweni mapya yaliyojengwa kwenye shule hiyo kwa fedha za Serikali kuu.Pichani kulia kwake alieambatana nae ni Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari - TMC Mwalimu Nyahori Mang'ari.

******************

Na Alex Siriyako, TMC Tabora


MKURUGENZI wa Manispaa ya Tabora Elias Mahwago Kayandabila
amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha Sh.Bilioni 1.2 kwa ajili ya miundombinu ya elimu kwa wanafunzi wa kidato cha tano kwa shule za Sekondari Milambo na Kazima.


Kayandabila ametoa shukrani zake za dhati kwa Rais leo Agosti 15, 2023 baada ya kutembelea shule hizo katika kuhakikisha utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kuzitaka shule zote za Sekondari zenye kidato cha tano kuhakikisha kuwa zinawapokea wanafunzi wa kidato cha tano kuanzia leo.


"Ikumbukwe kuwa, wanafunzi wa kidato cha tano kwa shule nyingi nchini wamepokelewa katika miundombinu mipya kabisa na ya kisasa mathalani Mabweni, Madarasa pamoja na Vyoo. Shule ya Sekondari Milambo ni miongoni mwa shule kongwe kabisa nchini.


" Na haijapata ujenzi mkubwa wa Miundombinu mipya kama huu wa awamu hii wa mabweni manne, madarasa manne na matundu kumi ya vyoo.


"Pia Shule ya Sekondari Kazima ikiwa nayo ni miongoni mwa shule kongwe imepata fursa ya ujenzi mkubwa wa miundombinu mipya ya kisasa kwa maana ya mabweni matatu, madarasa manne pamoja na matundu 10 ya vyoo."


Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Mirambo Mwalimu Daudi Mapere ameishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule yake Sh.milioni 670 kwaajili ya ujenzi wa mabweni manne, madarasa manne pamoja na matundu 10 ya vyoo na ameahidi matokeo makubwa kwasababu miundombinu imekuwa mizuri sana.


Wakati huo huo Mwalimu Elizabethi Masanja, ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Kazima amemshukuru Rais kwa kuwaondolea adha ambayo wangeipata kama wangepokea ongezeko hili la wanafunzi bila maboresho haya ya Miundombinu.


Mwalimu Masanja amefafanua awali Shule ya Kazima ilikuwa inapokea wanafunzi 200 wa kidato cha tano , na kwa mwaka huu inatarajia kupokea wanafunzi 546


Hivyo bila maamuzi magumu, makubwa, na kuungwa mkono ya serikali koboresha miundombinu, watoto hawa wangesomea mazingira ya shida sana. Hivyo amesishukuru Serikali kwa kusimamia vyema sana Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)hususani kwenye sekta ya elimu.


Kwa upande wao wanafunzi wa Kazima Sekondari na Mirambo kwa awamu tofauti tofauti wamemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwajengea miundombinu bora ya elimu na wameahidi kufanya vizuri katika mitihani yao.

MKURUGENZI wa Manispaa ya Tabora Elias Mahwago Kayandabila akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kazima,kushoto ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Kazima, Mwalimu Elizabethi Masanja
MKURUGENZI wa Manispaa ya Tabora Elias Mahwago Kayandabila akisalimiana na mmoja wa Wanafunzi shule ya Sekondari Milambo mara baada kuwapokea wanafunzi hao wa kidato cha tano kwenye mabweni mapya yaliyojengwa kwenye hiyo kwa fedha za Serikali kuu.Pichani kulia kwake alieambatana nae ni Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari - TMC Mwalimu Nyahori Mang'ari

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post