MCHENGERWA ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI• ACHANGIA UJENZI WA MSIKITI WA JITIMAI

Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa - CCM ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa viongozi wa dini zote nchini kuendelea kuhubiri umoja na amani kwa faida ya Taifa la Tanzania.

Waziri Mchengerwa ametoa wito huo wakati alipokuwa akiwahutubia waumini wa kiislamu kwenye Msikiti wa Jitimai uliopo kwenye jimbo la Mwera- Zanzibar na kufanya changizo la ukamilishaji wa ujenzi wa msikiti huo.

Katika msikiti huo, Mhe. Mchengerwa ametoa jumla ya shilingi milioni tano, mifuko mia moja ya saruji, kujenga chumba maalum kwa ajili ya kuhifadhia maiti na jengo moja la darasa la madrasa na juzuu 500 kama mchango wake.

Aidha, amesema kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na jumuiya hiyo, ameyachukua maombi ya kupatiwa miundombinu muhimu kama barabara, maji na umeme na ameahidi kuyafikisha serikalini ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

Akitoa hotuba yake mara baada ya kupata taarifa ya kazi kubwa ya kuanzisha huduma mbalimbali za jamii inayofanywa na Jumuiya ya Jitimai Tanzania nchini kote, Mhe . Mchengerwa ameipongeza jumuiya hiyo na ameiomba iendelee kufanya kazi hiyo kwa kuwa ni kazi ambayo Mwenyezi mungu ameelekeza katika kitabu kitukufu cha Quran.

Akiwa hapo Waziri Mchengerwa amepata fursa ya kujionea ujenzi unaoendelea wa msikitiki huo, madarasa, zahanati na uwanja wa mikutano

Amesema Quran tukufu imeeleza namna ambavyo jamii inavyotakiwa kuishi ambapo aamesema imesisitiza binadamu kuishi kwa amani na upendo hivyo amesema viongozi wote wa dini wana wajibu wa kuwaongoza watanzania kiroho.

Aidha amewaomba kuendelea na jitihada za kuliombea taifa ili liendelee kuwa na amani kama maono ya waasisi wa taifa la Tanzania ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Amani Abeid Karume yaliyovyokuwa ya kuwaunganisha watanzania kuwa pamoja.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mwera Mhe. Mihayo Juma N’hunga kwa niaba ya wananchi wa Jimbo hilo amemshukuru waziri Mchengerwa kwa michango yake ambapo yeye pia amechangia mifuko 100 ya saruji.

Shehe wa Msikiti huo ndugu Amir amesema Jumuiya ya Jitimai Tanzania ni Miongoni mwa Jumuiya za Kiislam ambazo zinatoa huduma za jamii katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara na visiwani.

Miongoni mwa maeneo ambayo Jumuiya ya Jitimai Tanzania imekuwa ikifanya kazi ni pamoja na Mkuranga, Dodoma, Dar es Salaam, Pemba na Tanga ambapo katika kisiwa cha Unguja ina maeneo sita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post