KAMATI YA BUNGE YA ELIMU YAIAGIZA WIZARA YA ELIMU KUTOA FEDHA KUKAMILISHA MIRADI DUCE**************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge la Elimu, Tamaduni, Sanaa na Michezo imeiomba Serikali kuhakikisha inakamilisha kwa wakati miradi ya ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Chang'ombe pamoja na maabara kwaajili ya shule ya Sekondari Chang'ombe Inayosimamiwa na Chuo Kishiriki Cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeombwa kufikia mwezi Desemba 2023, miradi hiyo iwe imekamilika ili ifikapo Januari mwakani iweze kufanya kazi.

Hayo yamesemwa leo Augosti 8,2023 mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kutembelea Miradi mbalimbali katika Chuo Kishiriki Cha Elimu Dar es Salaam, DUCE ambapo wamepongeza juhudi ambazo zinafanywa na Chuo hicho.

Akizungumza katika ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Elimu, Tamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko amesema kuna umuhimu mkubwa Wizara kuhakikisha inatoa fedha kwaajili ya kukamilisha miradi hiyo kwani Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam, (DUCE) kimeanzisha miradi hiyo hivyo inatakiwa wapewe ushirikiano kukamilisha miradi hiyo.

Amesema miradi inakwenda vizuri na ubora wa ujenzi uko vizuri na inaonekana uhitaji ni mkubwa katika matumizi ya miradi hiyo itakapokamilika.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Omary Kipanga amesema wamepokea maagizo kutoka kwa Kamati, hivyo Wizara itatekeleza maagizo hayo ili kuhakikisha miradi ambayo inasimamiwa na DUCE inakamilika kwa muda ambao umewekwa ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu kwenye maeneo hayo.

"Wizara tutakuja kuongeza fedha ili miradi iweze kukamilika ndani ya miezi minne kama maagizo yalivyotolewa ili ifikapo mwezi Januari wanafunzi wetu waweze kuyatumia kikamilifu". Amesema Mhe. Kipanga

Pamoja na hayo Naibu Waziri Kipanga ameipongeza Menejimenti ya Chuo kwa kuibua majengo hayo na kuona umuhimu wa kukamilisha miradi hiyo ambayo itakuwa na msaada mkubwa itakapokamilika.

Nae Rasi wa Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu (DUCE), Prof.Stephen Maluka amesema wenye jengo la shule ya msingi wametumia takribani shilingi milioni 350 na ujenzi unatarajia kukamilika mwezi Novemba 2023 kwa madarasa manne na ofisi, na kwa upande wa jengo la maabara mpaka sasa wameshatumia Shilingi milioni 553 na ujenzi bado unaendelea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post