FEDHA ZA UJENZI WA ZAHANATI ZASHTUKIWA KUPIGWA NA VIONGOZI WA KITONGOJI, MBUNGE AFICHUA MADUDU


Wananchi wa Kitongoji cha Kinyika, Kata ya Mkwese, Wilayani Manyoni wamelalamikia Viongozi wa Serikali kitongoji hapo kwa ucheleweshwaji wa ujenzi wa Zahanati ikiwa walishachangishwa na kutoa michango yao.

Wananchi hao wametoa malalamiko yao mbele ya Mbunge wa Manyoni Mashariki Mhe. Dkt. Pius Chaya alipofika kufanya Ziara.

Wananchi hao wamekiri kuumizwa na kuwa na wasiwasi wa Upotevu wa Fedha ambazo zilikusanywa ikiwa ni takribani Milioni 2 katika nyakati tofauti huku Mfuko wa Jimbo ukiwa ulishatoa Milioni 6.5 ambapo mpaka sasa ujenzi upo kwenye hatua za msingi na umeshapita muda mrefu.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wakitoa kero mbele ya Mbunge wao kwa niaba ya Wananchi hao akiwemo Bwn. Christopher Shauri na Mrosha Juma , wamesema
“Baadhi ya viongozi wanajibeba, walitangaza kwamba wanahitaji kutengeneza zahanati tukaambiwa tuchange mchango tukatoa lakini mpaka Leo ujenzi upo katika hatua ya Msingi, ukuta umeanza kuchanika siku jengo likimalizika si litamwangukia mgonjwa kweli?, Unaposema sisi tutoe michango ya Zahanati Hawa viongozi ukitoka hiyo imeisha ni mpaka mwakani, viongozi wetu hawana ushirikiano na sisi”.


Kutokana na malalamiko hayo Mhe, Dkt. Chaya amewapa Siku Saba wasimamizi wa Mradi huo ambao ni Viongozi wa eneo hilo kuhakikisha jengo hilo linasimama na ikiwa vinginevyo atapendekeza wafanyiwe uchunguzi na TAKUKURU.

"Natoa maagizo kwa viongozi wanaohusika anzeni kufanya mchakato wa kutafuta mafundi wazuri na huyo fundi ambaye amelipwa laki nne na kazi hajafanya azirejeshe ndani ya siku 3 na nawapa siku saba muwe mmeshakamilisha ujenzi mpaka kufikia hatua ya lenta na kama ikibidi uchunguzi uje kufanywa na TAKUKURU utafanywa juu ya haya malalamiko yenu” ,alisema Dkt. Chaya

Hata hivyo Ziara ya Mbunge huyo inaelekea ukingoni ambayo dhima kuu ikiwa ni kusikiliza na kutatua kero za wananchi ikiambatana na mikutano ya hadhara juu ya miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita inayoendelea kutekekezwa katika Jimbo la Manyoni Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post