CMSA YATOA IDHINI YA KUUZA HATIFUNGANI YA BENKI YA CRDB YENYE THAMANI YA SH.BILIONI 780Na Mwandishi Wetu,

MTENDAJI Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA)Nicodemus Mkama amesema utoaji wa idhini ya kuuza Hatifungani ya Benki ya CRDB, yenye thamani ya Sh.bilioni 780 sawa na dola za Marekani milioni 300 inaonesha dhamira yao ya dhati ya kuunga mkono juhudi za benki ya CRDB.

Juhudi hizo ni pamoja na kupata rasilimali fedha kupitia masoko ya mitaji ili kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Mkama ameyasema hayo leo jijini Dar es Salam wakati wa hafla ya kupokea idhini ya hatifungani ya Benki ya CRDB yenye mgus na matokeo chanya kwa mazingira na jamii.

"Hafla hii ni ya kihistoria sio tu katika sekta ya fedha hapa nchini, bali katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kwani CRDB inakuwa benki ya kwanza nchini kupata idhini kutoka CMSA, kutoa hatifungani itakayowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira na yenye matokeo chanya kwa jamii yaani green, social and sustainability bond.

"Hatifungani hii pia inakuwa ya kwanza kwa ukubwa ikiwa imetolewa katika fedha za aina mbalimbali na yenye mguso kwenye mazingira, na matokeo chanya kwa jamii yaani multicurrency green, social and sustainability bond iliyotolewa kwenye masoko ya hisa, Kusini mwa Jangwa la Sahara, " amesema.

Ameongeza utoaji wa Hatifungani yenye mguso na matokeo chanya kwa mazingira na jamii ni matokeo chanya ya ushirikiano wa wadau katika sekta ya masoko ya mitaji, wenye lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha sekta ya fedha inawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia shughuli za maendeleo.

Ameongeza hatua hiyo ni muhimu, kwani inachangia katika kuchochea ukuaji wa sekta binafsi; umma na uchumi wa nchi kwa ujumla huku akifafanua utoaji wa Hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi hapa nchini.

"Kwani utachangia katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya miradi katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

"Hatifungani hii pia inawezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zitakazopatikana zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali za kimaendeleo kijamii na wananchi watakaowekeza katika hatifungani hii watalipwa riba hivyo kuinua vipato vyao, " amefafanua.

Ametumia nafasi hiyo kuipongeza Bodi na Uongozi wa Benki ya CRDB kwa juhudi zilizowezesha kukidhi matakwa ya sharia na kupata idhini kutoka CMSA huku pia akizishukuru na kuzipongeza taasisi na wataalam wote walioshiriki katika mchakato huu.

Amesema kazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na hivyo kufanikisha hatua hiyo kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa.

"Nitoe taarifa kwa umma kuwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeidhinisha Hatifungani ya Miaka 5 ya Benki ya CRDB, yenye mguso na matokeo chanya kwa Mazingira na Jamii yenye thamani ya Shilingi bilioni 780.

"Idhini imetolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani;

" Uwepo wa Muundo wa Hatifungani; Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji na kupata ithibati kutoka kwa kampuni yenye utaalam kuhusu miradi yenye mguso na matokeo chanya kwa Mazingira na Jamii.

"Fedha za mauzo ya Hatifungani hii zitatumika kuwekeza katika miradi yenye mlengo wa kuhifadhi mazingira na yenye mguso na matokeo chanya kwa Jamii, ukizingatia Dunia kwa sasa ipo katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, " amesema.

Aidha Mkama amesema sekta zitakazonufaika ni pamoja na sekta ya kilimo, nishati jadidifu, viwanda endelevu, ujenzi, maji, afya na elimu. Hatua hii ni muhimu, kwani itawezesha utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa hususan lengo namba saba la Maendeleo Endelevu (SDG) linalohimiza upatikanaji wa nishati safi kwa wote.

Pia amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala hivyo utoaji wa hatifungani hii utawezesha utekelezaji wa malengo na azma ya Serikali ya uwekezaji katika nishati safi.

Aidha, kutolewa kwa hatifungani katika fedha mbalimbali za kigeni kutatoa mchango katika jitihada za Serikali za kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni hapa nchini.

"CMSA imeidhinisha utoaji wa hatifungani ya CRDB kutokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Mh. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Serikali kupitia CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuza hisa kwa umma;

"Hatifungani za miundombinu; hatifungani rafiki wa mazingira; hatifungani za bluu (blue bonds); na hatifungani za taasisi za Serikali.Nitoe taarifa kwa umma kuwa wawekezaji wote, watanzania na wasio watanzania, watu binafsi, vikundi, kampuni, mashirika na taasisi wanaruhusiwa kuwekeza katika hatifungani hii."

Mkama ametoa rai kwa wadau wote wa sekta ya fedha kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana katika kutekeleza mikakati ya upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo kwa kutoa bidhaa mpya na bunifu .

Ameongeza bidha hizo zinalenga kuhifadhi mazingira na zenye mguso na matokeo chanya kwa jamii na hivyo kuchangia katika kuchochea maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi hapa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post