JE WAJUA SEKTA YA KILIMO ILIKOTOKA, ILIPO NA INAELEKEA WAPI

Fuatilia taarifa hizi kupitia tovuti ya Wizara ya Kilimo www.kilimo.go.tz na mitandao yote ya Wizara, upate habari za leo leo na za uhakika kuhusu sekta ya kilimo.

Kwa kipindi cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, viongozi wote walioongoza  nchi hii wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kilimo.Walihakikisha wanalipa suala la usalama wa chakula uzito mkubwa. Waliweka sera na mipango mizuri katika sekta ya kilimo, na wakati wote nchi imejitosheleza kwa chakula kwa kiasi kikubwa.

Fuatana nami katika habari hii ujikumbushe tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.

Awamu ya kwanza iliongozwa na Baba wa Taifa na Rais wa kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alikuwa mstari wa mbele na mhimili mkubwa wa kuwaongoza Watanzania katika kupata Uhuru. Mara baada ya nchi yetu kuwa huru, kipaumbele cha kwanza katika kuendeleza uchumi kilikuwa kilimo. Kilimo kilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa. Kiliajiri zaidi ya asilimia 90 ya wananchi. Mazao yaliyolimwa wakati huo yalikuwa katani, kahawa na pamba. Kahawa na pamba ni mazao yaliyoongoza kulipatia taifa fedha za kigeni. Aidha, aina mbalimbali za mazao ya chakula yalizalishwa. Mbinu mbalimbali zilitumika kuhakikisha kilimo kinahamasishwa na tija katika kilimo ilionekana.

Kati ya miaka ya 1961 na 1980, zilibuniwa kauli mbiu na maazimio mbalimbali, kama vile chakula ni uhai, siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, mvua za kwanza ni za kupandia, na kadhalika. Lengo lilikuwa ni kuhamasisha maendeleo ya kilimo na kilimo cha ujamaa, ambapo kauli mbiu hizi ziliibuliwa katika maazimio mbalimbali.

Azimio la Arusha la mwaka 1967. Azimio liliweka njia kuu za uchumi mikononi mwa umma. Mashamba makubwa yaliyokuwa yakimilikiwa na walowezi yalitaifishwa na kuwa chini ya mashirika ya umma.

Azimio la Iringa la mwaka 1972, lenye kauli mbiu ya Siasa ni Kilimo. Liliweka msukumo wa kuanzisha mashamba makubwa ya Vijiji vya Ujamaa yaliyokuwa na lengo la kuhamasisha kilimo bora, yaani kanuni za kilimo bora.

Mwaka 1974, kulikuwa na kampeni ya nchi nzima, yenye kauli mbiu Kilimo cha Kufa na Kupona. Lengo la kampeni hii lilikuwa ni kuongeza uzalishaji wa chakula katika ngazi ya kaya.

Mwaka 1982, kulikuwa na kampeni ya Kilimo ni Uti wa Mgongo wa Taifa, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kilimo katika uchumi na usalama wa chakula katika nchi ya Tanzania.

Awamu ya pili iliongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi. Tulishuhudia mageuzi ambayo yalikuwa yakichochea maendeleo ya kilimo, yakiwemo utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya mwaka 1983. Kilimo kiliendelea kuwa ni sekta namba moja katika kutoa ajira kwa Watanzania. Serikali ilifanya mageuzi ya kiuchumi yaliyokuwa kichocheo katika maendeleo ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kupunguza mkwazo katika biashara ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa ajili ya ustawi wa wanachi.

Awamu ya tatu iliongozwa na Hayati Benjamin William Mkapa. Kilimo kilipata msukumo wa kipekee na kuwa chenye mafanikio. Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kilimo na Mifugo ya mwaka 1997 na uanzishwaji wa Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo, vilikuwa ni chachu kubwa katika kilimo. Utekelezaji wake uliongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo. Kilimo kilikua kutoka chini ya asilimia 3 hadi asilimia 6 na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na hali ya usalama wa chakula nchini kuimarika.

Awamu hii iliimarisha taasisi na kusimamia utawala bora, ilibinafsisha mashirika ya umma na kuboresha bodi za mazao na kubaki na bodi za udhibiti na uendelezai mazao. Kwa kipekee, iliunda Wizara ya Masoko na Ushirika, kuimarisha ugatuaji wa madaraka kwa kuimarisha Serikali za Mitaa, ambapo huduma za ugani za kilimo na mifugo zilihamishiwa TAMISEMI.

Awamu ya nne iliongozwa na Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete. Kilimo kiliendelea kupewa msukumo mkubwa. Hapa tunaona Azimio la Kilimo Kwanza la mwaka 2009, ambalo lilizinduliwa kipindi cha sherehe za Sikukuu ya Wakulima tarehe 3.8.2009, kwenye viwanja vya Nanenane, Nzuguni, Dodoma, likiwa na azma ya kuongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo nchini.

Sera na mikakati yake zililenga kutatua changamoto zilizoko katika sekta ya kilimo na kuibua fursa zilizo katika sekta ya kilimo. Lengo kuu lilikuwa ni kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, ambayo imeweka msukumo zaidi katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 Nguzo ikiwa ni kukuza kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa wakulima wakubwa na wadogo, na kutoa mikopo kwa wakulima wadogo kwa masharti nafuu, na kuongeza vivutio kwa ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya kilimo.

Aidha, uelewa na matumizi ya teknolojia za kisasa katika ngazi zote zilikumbukwa. Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika (CRMP) zilikuwa chachu ya kuleta Mapinduzi ya Kijani. Jambo la kujivunia kwa wakati huo ni kwamba asilimia 95 ya mahitaji ya Taifa ya chakula yalizalishwa hapa hapa nchini.

Mfumo wa kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi wakati upungufu unapotokea uliwekwa na kuanzishwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula.

Tuliposherehekea miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu hapo mwaka 2011, kilimo chetu kiliendelea kuwa nguzo na mhimili katika uchumi wa Taifa, na tulithubutu kusema Kilimo Kwanza “Tumethubutu, Tumeweza na Tunazidi Kusonga Mbele”.

Awamu ya tano iliongozwa na Hayati Dkt John Pombe Magufuli. Ilifanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu mbalimbali ambayo ni muhimu katika kuchochea uzalishaji, uongezaji wa thamani usafirishaji na masoko (viwanda).

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imethibitisha kwa vitendo utashi wa kisiasa wa kuutambua sekta ya kilimo kuwa namba moja katika kukua kwa uchumi wa Taifa.

 Awamu ya sita imeipa sekta hii kipaumbele katika bajeti ya Taifa. imewekeza katika maeneo ya kimkakati ya utafiti, uzalishaji mbegu bora, uimarishaji huduma za ugani, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, uhifadhi wa mazao na uimarishaji wa upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo. Aidha, imetoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima na imelipa suala la upimaji udongo kipaumbele.

Katika Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu II (ASDPII), uwezeshaji na  hamasa zinaendelea kufanyika ili sekta binafsi iweze kuwekeza na kufanya biashara katika sekta ya kilimo.

Haya yote ndiyo yaliyotufanya tufike tulipo na tunasongambele hamasa zipo palepale, Kilimo sasa ni kibiashara na kaulimbiu ya sasa ni Agenda 10/30. Kilimo ni biahara; anzia sokoni kisha nenda shambani, zalisha kulingana na mahitaji ya soko. Katika hili vijana wamekumbukwa, wanawake pia. Progrmu ya JENGA KESHO ILIYO BORA (BBT) imewalenga wakulima wote. Wamekumbukwa katika ruzuku ya mbolea na mbegu za alizeti imetolewa na seikali kwa wakulima. Lengo ni kuhakikisha kilimo kinazalisha kwa tija na ajira nyingi zinapatikana kupitia kilimo na ifikapo 2030 malengo yote kumi yawe yametekelezwa. Ndugu msomaji wangu usikose kusoma makala inayofuata ili uyajue malengo hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post