Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa
Na Mariam Kagenda _ Kagera
Mwenge wa Uhuru unatarajia kuzindua, kutembelea, kukagua Miradi ya Maendeleo 57 yenye jumla ya thamani ya Tsh. bilioni 26.3 katika mkoa wa Kagera kuanzia Agosti 8 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo August 4 ambapo amesema kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 utawasili mkoani Kagera ukitokea Mkoa wa Geita na kupokelewa Wilaya ya Muleba, kata ya Nyakabango katika Viwanja vya shule ya Sekondari Nyakabango.
Miradi itakayokaguliwa kutembelewa na kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 ni miradi ya Afya, Maji, Barabara, Elimu, Vikundi vya Vijana na Wanawake na miradi ya Kilimo. Aidha mwenge utakagua shughuli za mapambano dhidi ya malaria, madawa ya kulevya, mapambano dhidi ya rushwa, shughuli za lishe na mazingira.
Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, “TUNZA MAZINGIRA, OKOA VYANZO VYA MAJI KWA USTAWI WA VIUMBE HAI, KWA UCHUMI WA TAIFA”
Hadi sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100, hivyo Mkoa wa Kagera upo tayari kuukimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2023.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, katika maeneo ya miradi, maeneo ya mkesha wa Mwenge wa Uhuru pamoja sambamba na kujifunza falsafa mbalimbali za Mwenge wa Uhuru.
Mkoa wa Kagera una Halmashauri 8 ambapo Mwenge ukihitimisha mbio zake mkoani Kagera utakabidhiwa mkoani Kigoma siku ya tarehe 16.08.2023.