Picha haihusiani na habari hapa chini
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Hosam Elias mkazi wa Bukondamoyo kata ya Mhungula Mjini Kahama amefariki dunia huku mwenzake (jina limehifadhiwa) akinusurika kufa baada ya kunywa dawa zilizodaiwa kuongeza nguvu za kiume kwa mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Laurent Bakuye.
Inaelezwa kuwa mwanaume huyo amefariki dunia Julai 31,2023 na mwenzake walikunywa dawa ya kuongeza nguvu za kiume hali iliyosababisha uume kusimama muda mrefu na kushindwa kupata kipozeo hivyo kusababisha kifo chake huku mwenzake akiwahishwa hospitali kupatiwa matibabu.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Laurent Bakuye mkazi wa Bukondamoyo kata ya Mhungula halmashauri ya Manispaa ya Kahama kwa tuhuma za kuwapa watu dawa idhaniwayo kuwa ni sumu na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mwingine kulazwa katika hospitali ya manispaa ya Kahama.
"Tukio limetokea Julai 31,2023 ambapo watu wawili Hosam Elias mkazi wa Bukondamoyo na mwenzake mkazi wa Lumambo walifika kwa mganga huyo kupata dawa ya kuongeza nguvu za kiume. Baada ya kupatiwa dawa hizo ambazo waliuziwa kwa shilingi 1000 na walipozitumia walianza kuzidiwa ndipo Hosam Elias akafariki dunia hapo hapo na mwenzake kukimbizwa katika hospitali kwa matibabu zaidi",amesema Kamanda Magomi.
Kamanda Magomi amesema tayari wamechukua mabaki ya dawa hizo na wametuma kwa mkemia mkuu wa serikali ili zifanyiwe uchunguzi zaidi huku akitoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia dawa ambazo hazijathibitishwa ili kuepuka matukio kama hayo.