AMEND WAELEZEA MPANGO MKAZI USALAMA BARABARANI TANGA WAFIKIA ASILIMIA 90, POLISI WATOA NENO

Dereva wa Bajaji jijini Tanga Avishai Fanuel akiandika maelezo ya kotorudia kosa la kutosimama katika kivuko cha waenda kwa miguu baada ya kukamatwa na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani na kisha kufikishwa katika Mahakama ya Watoto iliyokuwa ikiendshwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwakizaro mkoani Tanga.Katikati anayeshudia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga William Mwamasika.Mahakama ya Watoto ni sehemu ya Mpango wa Shirika la Amend kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kuwajengea uelewa wanafunzi kutambua sheria ili kujieupusha na ajali.

**************

Na Mwandishi Wetu, Tanga

SHIRIKA la Amend Tanzania limesema limetekeleza Mpango Kazi wa Usalama Barabarani kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa asilimia 90 huku Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa wakipokeza hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ajali za barabarani.

Hayo yamesemwa leo Agosti 17, 2023 na Meneja wa Amend Tanzania Simon Kalolo baada ya kumaliza kwa uendeshaji kesi katika Mahakama ya Watoto( Mahakama Kifani) kwa madereva waliovunja sheria za usalama barabarani kwa kutosimama maeneo yenye alama za watembea kwa miguu yanayotumiwa kuvuka wanafunzi.

Mahakama ya Watoto ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kazi huo sambamba na kuweka alama na michoro ya barabarani zinazopita kwenye baadhi ya Shule za msingi katika Jiji la Tanga.

Akifafanua zaidi Kalolo amesema Amend imekuwa ikijishughulisha na usalama barabarani nchini tangu mwaka 2009 na kwa ufadhili wa Shirika la Fondation Botnar jijini Tanga,wanashirikiana na Halmashauri ya Jiji hilo kuboresha miundombinu ya barabara maeneo ya shule.

Amesisitiza wamekuwa wakitoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi, kuanzisha klabu za usalama barabarani na mahakama kifani za watoto, mafunzo kwa madereva pikipiki , kuandaa makongamano ya wadau wa usalama barabarani, kufanya tafiti huhusu ajali za barabarani, na kuandaa Mpango Kazi wa usalama barabarani kwa Jiji hilo.

"Mpango Kazi huo wa usalama barabarani lengo lake kuu ni kuboresha safari salama na endelevu kwa Jiji la Tanga ulizinduliwa Novemba 11 , 2022 na tangu ulipozinduliwa kuna mambo kadha yametekelezwa.

" Baada ya uzinduzi huo tumefanikiwa kuzindua miundumbinu katika shule tatu za msingi za Shaaban Robert, Mabawa na Majengo. Pia kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi 3,501 wa shule za msingi Mabawa, Majengo na Shabaan Robert na wengine 3,247 wa shule za sekondari Toledi, Kihere and Kiomoni.

"Tumeanzisha klabu mbili za shule za usalama barabarani katika Shule ya Msingi Usagara na klabu ya usalama wa baiskeli katika Shule ya Sekondari Usagara, yenye watoto 20 katika kila klabu.

Tumetoa mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto hawa, baada ya kuhitimu kuwa mabalozi, wakipokea vyeti katika hafla ndogo.Shughuli za vilabu hivi zimejumuisha mafunzo, midahalo ya usalama barabarani," amesema.

Pia amesema wametoa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki 350 kufanya jumla ya madereva waliopata mafunzo haya kufikia 950.

Kalolo amesema Februari mwaka huu wamesambaza vifaa vya kufundishia usalama barabarani kwa maofisa maendeleo ya jamii katika kata 22 kati ya 27 za Jiji la Tanga.

Ameongeza Juni mwaka huu maofisa maendeleo ya jamii walikuwa wamezungumza kuhusu usalama barabarani katika zaidi ya mikutano au matukio 50 tofauti, na kuelimisha jumla ya takriban wananchi 6,600.

" Tumekamilisha uwekaji wa miundombinu ya waenda kwa miguu katika eneo moja lenye shule tatu za msingi na kwamba lengo kuu ilikuwa kupunguza mwendo wa vyombo vya moto hadi chini ya 30km/h na kuwapa watoto mahali salama pa kutembea na kuvuka."

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani William Mwamasika ameipongeza Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani huku akifafanua bodaboda katika Jiji la Tanga zinachangia ajali kwa kiwango kikubwa, hivyo amewaomba waendesha vyombo vya moto kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Pia ametoa rai kwa wazazi na walezi kutokubali wanafunzi kupakiwa mishikaki kwenye bodaboda aidha wakati wa kwenda shule au kurudi nyumbani kwani ikitokea ajali msiba wake utakuwa mkubwa na wenye kuumiza.

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo Mayasa Said amesema baada ya wanafunzi na walimu kupatiwa elimu ya usalama barabarani sambamba na kuwekwa kwa alama zinazowawezeha wanafunzi kuvuka kwa usalama ajali zimepungua, hivyo wanaishukuru Amend kwa kupeleka mpango huo jijini Tanga.


Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga William Mwamasika (katikati) akizungumza baada ya kumalizika kwa uendeshaji kesi za madereva waliokiuka sheria za usalama barabarani uliokuwa ukisimamiwa na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwakizaro jijini Tanga.

Meneja wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo akielezea hatua waliyofikia katika kuutekeleza Mpango Kazi wa Usalama Barabarani kwa Jiji la Tanga baada ya kufanyika kwa Mahakama ya Watoto waliokuwa wakisimamia kesi za madereva waliokiuka sheria za usalama barabarani

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwakizaro jijni Tanga ambao wamepatiwa elimu ya usalama barabarani wakisikiliza kesi katika Mahakama ya Watoto.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwakizaro wakiendesha kesi katika Mahakama ya Watoto ambayo ilikiwa ikisikiliza kesi za madereva waliovunja sheria za usalama kwa kutosimama eneo la kivuko cha waenda kwa miguu

Mahakama ya Watoto ikiendelea baada ya mmoja wa madereva katika Jiji la Tanga kufikishwa kwenye Mahakama hiyo baada ya kubainika amekiuka sheria za usalama barabarani

Mmoja wa madereva akisoma kiapo cha kutorudia tena kosa la kutosimama katika kivuko cha waenda kwa miguu baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Watoto.

Mkufunzi wa mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda akitoa ufafanuzi wa michoro mbalimbali ya usalama barabarani kwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga ( hayuko pichani)


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post