WATATU WAFARIKI AJALI YA NOAHWatu watatu wakazi wa Lugala, Kata ya Manzase mkoani Dodoma, wamefariki dunia jana Jumanne usiku baada ya gari aina ya Noah walilokuwa wamepanda kutumbukia kwenye korongo.

Imeelezwa kuwa dereva wa gari hilo alishindwa kupandisha mwinuko uliopo kwenye barabara kuu katika eneo hilo hali iliyosababisha kupoteza mwelekeo na kuingia kwenye korongo.

Akizungumza kuhusu ajali hiyo leo Agosti 2, 2023 Diwani wa Kata ya Manzase, John Mika amesema majira ya saa 2 usiku gari hiyo ilichukua abiria kutoka mnada wa Fufu na kuwarudisha kwenye maeneo yao.

“Ilikuwa usiku wakati gari hiyo inatoka mnadani na kabla ya kupanda mlima ikawa imemshinda dereva na kupelekea gari kuangukia kwenye korongo na watu wawili walikufa hapohapo na mmoja alifariki wakati anapelekwa hospitali,” amesema.

John amesema waliofariki ni Amos Matereka, John Nghambi na Nhoya Mashamba ambao familia zao zinatarajia kufanya mazishi leo na majeruhi wawili wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Aidha amesema watu wanane waliotolewa kwenye gari hilo walipatiwa matibabu kwenye zahanati ya kata na kufanya idadi ya watu waliokuwepo kwenye gari hiyo kuwa 13.

Mkazi wa kijiji hicho Anna Chihicha ameiomba Serikali kuwasaidia kusawazisha eneo hilo ambalo lina mwinuko hivyo kuhatarisha usalama wa watumiaji wa eneo hilo.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno amethibitisha kutokea ajali hiyo na kuahidi kutoa taarifa kamili baadaye.
CHANZO-MWANANCHI.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post