WAZIRI SIMBACHAWENE AIAGIZA SEKRETARIETI YA MAADILI KUTUMIA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (Mb) ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupokea matamko ya rasilimali, maslahi na madeni ya Viongozi wa Umma ili kuongeza uwazi katika utendaji kazi.

Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo tarehe 5 Julai, 2023 alipotembelea Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma zilizoko Kilimani, jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri aliambatana na Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Angalieni matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kupokea matamko ya raslimali, maslahi na madeni ya Viongozi wa Umma, hii itasaidia kuongeza urahisi wa viongozi kuwajibika, uwazi na kupunguza minongono katika umiliki wa mali kwa viongozi wa umma,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhe. Simbachawene, matumizi ya TEHAMA yanayokusudiwa yanatakiwa kufungua milango kwa kiongozi wa umma kuongeza raslimali zake wakati wowote bila kusubiri mwisho wa mwaka.

“Katika matumizi ya mifumo, hakikisheni mnawashirikisha watumiaji kwasababu wao ndio wanaojua changamoto za ujazaji wa tamko,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema, muundo wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma unatakiwa kuangaliwa upya ili kuiboresha na kuleta ufanisi katika utendaji kazi.

“Haiwezekani chombo kama hiki chenye historia kubwa kisiboreshwe mara kwa mara ili kuleta ufanisi katika kusimamia maadili ya viongozi wa umma,” amesema na kuongeza kuwa “Iangalieni upya miundo yenu ukama inaleta tija.”

Kwa upande wake Mhe. Ridhiwani amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Maadili kutovunjika moyo wakati wanapotekeleza majukumu yao.

“Naipongeza taasisi yenu kwa kazi nzuri na ngumu inayohitaji busara ya kusimamia maadili ya viongozi wa umma. Napenda kuwatia moyo katika utekelezaji wa kazi zenu,’ amesema.

Naye Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi, Kamishna wa maadili alimueleza Waziri kuwa changamoto kubwa ya Sekretarieti ya Maadili kwa sasa ni kutokamilika kwa ujenzi wa jengo la makao Makuu na Ofisi ya Kanda ya Kati ambao umetumia muda mrefu.

“Mhe. Waziri ujenzi wa jengo letu umetumia muda mrefu sana, kutokamilika kwa jengo letu kunatulazimu kuendelea kufanyia kazi katika jengo la kupanga. Kama jengo letu lingekamilika kwa wakati tungeweza kuokoa fedha za pango kutekeleza majukumu mengine.”

Mradi wa jengo la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma unasimamiwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA).

Waziri Simbachawene amewaagiza TBA kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post