Shirika la WOTESAWA latoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wafanyakazi wa nyumbani, vijana

Shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani WOTESAWA limetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wafanyakazi wa nyumbani pamoja na vijana wanaounda vikundi mbalimbali vya ujasiriamali jijini ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora.

Mafunzo hayo ya vitendo yamefanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Jumatatu Julai 17 hadi Ijumaa Julai 21, 2023 yakijumuisha washiriki 45 kutoka Kata za Mahina na Buhongwa jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuhamasisha haki za kiuchumi na kijamii kwa wafanyakazi wa nyumbani na vijana unaotekelezwa kwa miaka miwili tangu mwaka 2022 kwa ufadhili wa shirika la Foundation For Civil Society (FCS). 

Msimamizi Msaidizi wa Mradi huo kutoka Shirika la WOTESAWA, Esther Petro alisema mafunzo hayo yatawasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia bidhaa wanazotengeneza hatua itakayowasaidia kuondokana na utegemezi ambao una mahusiano ya karibu na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

"Lengo kuu la shirika la WOTESAWA ni kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani, hata hivyo bila kuwawezesha kiuchumi bado wataendelea kukabiliana na vitendo vya ukatili hivyo tunaamini kupitia mafunzo haya wataweza kujikwamua kiuchumi na kutoendelea kuvumilia vitendo vya ukatili wakiwa kwa waajiri wao" alisema Esther.

Esther aliebainisha kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kutambua umuhimu wa kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo za viungo, chakula na vinywaji ambazo zinakidhi ubora, kusajili biashara zao na kulipa kodi pindi zinapofikia hatua ya ukuaji.

Naye Afisa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa Mwanza, Giliard Abel akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo alisema wajasiriamali wengi hushindwa kurasimisha biashara zao kutokana na ukosefu wa elimu hivyo mamlaka hiyo inaendelea kuelimisha jamii kutambua taratibu za uanzishaji biashara, kupata namba ya mlipa kodi pamoja na sifa za anayepaswa kulipa kodi na anayestahili kupata msamaha wa kodi.

Kwa upande wake Mkaguzi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mkoa Mwanza, Nelson Mugema alisema ni muhimu wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kupitia TBS kwani hatua hiyo inawasaidia bidhaa zao kushindana sokoni huku akiongeza kuwa kwa sasa wajasiriamali wanaoanza uzalishaji wanayo fursa ya kujisajili kupitia SIDO ambapo wanapata msamaha wa kufanya shughuli zao kwa miaka mitatu bila kutozwa gharama zozote hatua inayolenga kuchochea vijana kukuza mitaji yao.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Martha Benjamini na Khadija Ramadhan walisema awali hawakuwa na uelewa kuhusu namna ya kurasimisha biashara zao hivyo wanatarajia kuyatumia vyema ili kuboresha zaidi shughuli zao.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Msimamizi Msaidizi wa mradi wa kuhamasisha haki za kiuchumi na kijamii kwa wafanyakazi wa nyumbani na vijana kutoka shirika la WoteSawa, Esthe Petro (kushoto) akiwa na mkufunzi wa mafunzo hayo (kulia) kwenye maandalizi ya kuandaa bidhaa ya pilipili ya kupika.
Mkufunzi akitoa ufafanuzi hatua za kufuata wakati wa kuandaa bidhaa mbalimbali ikiwemo viungo vya chakula/ pilipili.
Mafunzo yakiendelea.
Maandalizi ya kuandaa pilipili ya kupika.
Afisa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa Mwanza, Giliard Abel akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.
Mkaguzi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mkoa Mwanza, Nelson Mugema akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.
Afisa Ustawi kutika Shirika la WoteSawa, Demitila Faustine akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post