TPDC YAPAA KIUTENDAJI, YAJIENDESHA KWA FAIDA



*Yaanika mikakati yake, sasa mafuta, gesi kuwa ya uhakika

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeimarika kifedha kwa kupata faida ya Sh bilioni 97.78 mwaka 2021/22 ukilinganisha na Sh bilioni 22.92 kwa mwaka 2020/21.

Aidha mizania ya fedha imekuwa imara zaidi kutoka Sh trilioni 3.17 mwaka 2018/2019 hadi Sh trilioni 4.21 mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la Sh trilioni 1.042 katika kipindi cha miaka minne.

Takwimu za mafanikio hayo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC , Mussa M. Makame wakati akieleza mafanikio ya shirika katika utekelezaji wa majukumu yake kwa wahariri na waandishi wa habari Dar es Salaam leo.

Alisema katika utekelezaji wa majukumu yake kadiri ya malengo ya kuanzishwa kwake, TPDC imekuwa na mafanikio makubwa yanayogawanyika katika maeneo sita.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni uhakika wa upatikanaji wa nishati , usambazaji wa nishati safi, mafanikio ya kiutendaji na kifedha, utekelezaji wa miradi ya kielelezo ya Taifa,utekelezaji wa miradi na uwajibikaji kwa jamii.

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi, William Chiume alisema Mwaka wa fedha 2021/22 Shirika lilifanikiwa kulipa Serikali Sh bilioni 62.84 katika Mfuko wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi, na kuipa gawio la Sh bilioni 2.7.

Aidha, alisema Shirika limelipa kodi mbalimbali Sh bilioni 57.85 huku likiendelea kutekeleza dira yake ya kuwa Kampuni kubwa ya mafuta inayojiendesha kibiashara.

TPDC ni mkono wa Serikali katika usimamizi wa masuala yote yanayohusiana na utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa nishati za mafuta na gesi asilia.

TPDC iliyoanzishwa kwa Tamko la Rais Na. 140 la Mei 30, 1969 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Na. 17 ya Mwaka 1969 na baadae, kupitia Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015 TPDC na kupewa hadhi ya kuwa Shirika la Mafuta la Taifa ambalo linapaswa kujiendesha kibiashara, moja ya kazi yake ni kuhakikisha uhakika wa nishati.

"TPDC imeendelea kuwa mhimili wa upatikanaji wa nishati nchini kwa kuhakikisha uwepo wa gesi asilia ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na kukuza uchumi kupitia matumizi ya gesi kama nishati viwandani, kupikia majumbani na nishati ya kuendeshea magari.

"Aidha TPDC inatekeleza jukumu la kuhakikisha pia uhakika wa upatikanaji wa nishati ya mafuta kupitia ushiriki wake katika zabuni za uagizaji wa mafuta na usambazaji wake nchini," alisema Makame.

Ikiwa na kampuni tanzu mbili ambazo ni Gas Supply Company (GASCO) na TANOIL Investments Limited (TANOIL) imesema inaendelea kujitanua katika matumizi ya gesi asilia kwa kuhakikisha inajenga au kuvutia wawekezaji binafsi kwa vituo vya CNG kwa ajili ya vyombo vya moto na pia kusambaza majumbani.

Naye Mkurugenzi wa Utafutaji na Uendelezaji wa Gesi na Mafuta wa TPDC, Kenneth Mutaonga akizungumzia usambazaji wa nishati safi ya kupikia na kuendeshea magari kupitia mfumo wa CNG alisema wateja waliounganishwa kwa sasa ni wale wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.

"Jumla ya nyumba 1,511 na Taasisi saba zimeunganishwa kwenye mtandao wa gesi asilia hapa nchini na magari takriban 2,000 yanatumia gesi asilia kama mbadala wa mafuta" alisema Mutaonga.

Huku likiwa limepunguza utegemezi wa fedha kutoka Serikalini kufikia asilimia moja kwa sasa imejipanga vyema kutekeleza Miradi ya Kielelezo ya Taifa, ukiwemo Mradi wa LNG wenye gharama ya Dola za Marekani bilioni 42 na Mradi wa EACOP wa Dola za Marekani Bilioni 5.

Kuhusu urejeshaji wa faida kwa umma ambao umelenga kwenye Elimu, Afya, Maji na Utawala Bora hadi Mwaka 2021/22 kiasi cha Sh bilioni 2 zimetumika

Akizungumzia Mkakati ya Shirika kwa Miaka Mitano ijayo alisema baada ya kuwa na mizania mizuri ya fedha, alisema wamepania kutafuta wabia wa kimkakati kutekeleza miradi mbalimbali na kuendelea na uwekezaji kwenye miradi mbalimbali kwa faida za biashara.

Aidha, alisema watatanua soko la gesi nchini na kwenda nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kwa kuongeza mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwa njia ya mabomba na gesi iliyoshindiliwa (CNG) ili kupunguza uagizaji wa mafuta nchini.

Pia watajenga maghala ya kuhifadhi mafuta na kuanzisha hifadhi ya kimkakati ya mafuta na kuhakikisha mitambo ya kuchakata na kusafirisha gesi inafanya kazi muda wote kwa asilimia 100 bila kuwa na matukio makubwa ya ajali



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post