TANZANIA YABAINISHA HATUA INAZOCHUKUA KUELEKEA USAWA WA KIJINSIA


Na WMJJWM, Kigali, Rwanda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameshiriki mdahalo wa hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la kizazi chenye usawa.

Katika Mjadala uliofanyika Julai 18, 2023 jijini Kigali, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Women Deliver, Mhe. Dkt. Gwajima amebainisha maeneo makuu ya vipaumbele, ili kutekeleza ahadi hizo ikiwa ni pamoja na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia, uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi, Ushiriki wa Wanawake katika kufanya maamuzi, na uingizaji wa Jinsia katika Sera za Kisekta.

Aidha, ameelezea jinsi gani Tanzania inaendelea kuhakikisha wanawake wanainuliwa kiuchumi ambapo, imehamasisha na kuratibu kuundwa kwa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya taifa, mikoa, wilaya na hadi kata na vijiji.

Ameelezea pia jinsi gani Tanzania iko mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kwenye kushika nafasi za uongozi wa juu akitoa mifano kadhaa ya viongozi wa kitaifa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzbar na Tanzania Bara.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Gwajima ameeleza jinsi Tanzania inavyoendelea kutumia mabaraza ya watoto kama mojawapo ya chombo cha kufanya sauti za watoto wa shule za msingi na sekondari kusikika na kusikilizwa.

Akiwasilisha mada kwenye mjadala uliohusu umuhimu wa wasichana kushiriki kwenye mijadala ya maamuzi ya kisera, Mhe. Dkt. Gwajima amebainisha kuwa, matokeo ya sauti hizo ni kuanzishwa kwa Madawati ya ulinzi wa watoto katika Shule za msingi na sekondari nchini.

Aidha, ametoa wito kwa Wadau mbalimbali kuja kushirikiana na Tanzania kwenye mipango hii. Ameishukuru taasisi ya BRAC kwa ushirikiano wao kwenye mpango wa kufikia vijana takribani 500000 (laki tano) kupitia mkataba wa mashirikiano na Wizara.

Katika Mijadala hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe, ameshiriki pamoja na viongozi wengine kutoka Tanzania akiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufic.

Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Abeida Rashid Abdallah pamoja Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post