RAIS SAMIA MGENI RASMI KILELE CHA SIKU YA MASHUJAAMkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemarie Senyamule akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya mashujaa.


Na Dotto Kwilasa,DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa ifikapo tarehe 25 Julai ya mwaka huu Jijini hapa.

Aidha maadhimisho hayo yataadhimishwa tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma, ambapo  yalikuwa yanafanyika katika Viwanja vya Jamatin vilivyopo katikati ya Mji wa Dodoma, mwaka huu Kilele cha Maadhimisho haya kitafanyika katika Uwanja mpya wa kudumu wa Mashujaa uliopo katika eneo la Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 20,2023 Jijini Dodoma,Mkuu wa mkoa huu Rosemary Senyamule amesema Tanzania huwa inaadhimisha kumbukumbu ya siku ya Mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda Uhuru wa Nchi yetu.  

Amesema Siku hiyo ni muhimu kwa sababu inawakumbusha watanzania Kwa ujumla kuhusu wajibu wao wa kutunza historia ya Mashujaa waliopigania, kutetea na kulinda Uhuru wa nchi ikiwa ni pamoja na kuitunza na kuihifadhi vema ili kurithisha vizazi vijavyo.

"Ni mumuhimu Kwa watanzania kutumia historia hii kukuza na kuendeleza amani na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti mbalimbali, ikiwemo za kikabila, kidini na  itikadi za kisiasa, historia hii inatupa deni kwetu la kuutafsiri na kuutumia ujasiri wa Mashujaa wetu kufanya maamuzi ya kiujasiri yanayojielekeza katika kuleta mageuzi ya kiuchumi ili kizazi cha sasa na kijacho kifaidike na vitendo vya kijasiri vilivyofanywa na Mashujaa hao,"amesema

Amefafanua kuwa  shughuli za Mashujaa zitatanguliwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 Usiku wa tarehe 24 Julai, 2023 kuamkia tarehe 25 Julai 202 na kueleza kuwa amepewa heshima ya kuuwasha Mwenge huo wa Mashujaa kwa niaba ya Watanzania na kwamba Mwenge huo utazimwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma tarehe 25 julai 2023 saa 6:00 Usiku.

"Ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan,  kwa kuibua wazo na kutoa maelekezo ya kutafuta eneo kubwa la kudumu kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa, ninampongeza pia  kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kujenga Mnara wa Mashujaa pamoja na kulisimamia wazo lake hadi limefanikiwa,"amesisitiza 

Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma ameeleza kuwa  Maandalizi ya Maadhimisho yamekamilika kwa asilimia 100 na kutumia nafasi hiyo  kuwakaribisha Viongozi na Wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na kutoka nje ya Mkoa wa Dodoma, ikiwemo Mikoa jirani ya Singida, Manyara, Iringa na Morogoro kujitokeza kwa wingi kuja kuungana na Wanadodoma katika kuadhimisha siku hiyo muhimu.

"Niwaalike pia kushirikiana nami na Meya wa Jiji la Dodoma katika hafla ya uwashaji na uzimaji wa Mwenge wa Mashujaa,tutumie Maadhimisho hayo kuimarisha umoja wa Kitaifa, Amani na Utulivu ili muda mwingi utumike katika kubuni na kutekeleza kazi za kuleta maendeleo ya Nchi yetu,

Niwaombe Wanahabari, Viongozi wa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Wakala ya Serikali, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kimila na Viongozi wa Vyama vyote vya Siasa kuwahimiza Wananchi, Watumishi wa Sekta ya Umma na Binafsi, Waumuni na Wanachama wa Vyama vya Siasa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho  haya,"amesema


Senyamule pia ametumia  fursa hiyo kuzishukuru Taasisi zote, ambazo kwa namna moja au nyingine zimeshiriki katika ujenzi wa Mnara Mpya wa Mashujaa katika Mji wa Serikali – Mtumba na kueleza kuwa hiyo ni alama ya uthibitisho bayana wa namna ya kuwaenzi Mashujaa wa Nchi yetu.5236

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments