Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati akizindua rasmi Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu nchini kuendelea kufanya mapitio ya Mitaala iliyopo kwa kuzingatia miongozo iliyopo ili kuendana na mabadiliko ya soko la Ajira.
Prof. Mkenda ametoa Rai hiyo wakati akizindua rasmi Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo Kukuza Ujuzi Nchini Kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa Uchumi Imara na Shindani.
"Kauli mbinu ya Maonesho haya inaakisi hali halisi na matarajio ya Watanzania. Sisi kama Taifa tunaendelea na mchakato wa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na Mitaala ya Elimu na Mafunzo kwa ngazi zote". Alisema Prof. Mkenda
Amesema Serikali inatambua kuwa Elimu ya Juu ni Elimu ya Kimataifa, kwa kuzingatia hilo amevisisitiza Vyuo Vikuu kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali duniani ili kujenga mahusiano yenye tija kuwawezesha Watanzania kupata maarifa na ujuzi.
"Leo tumeweka sahihi ya mashirikiano ya kielimu kati ya Tanzania na Serikali ya Hungary, ambapo kutakuwa na ufadhili wa Wanafunzi kwenda kusoma nchi hiyo, vile vile Tanzania itatoa ufadhili wa Wanafunzi wao kuja kusoma hapa nchini, ili kuvifanya Vyuo Vyetu kuwa vya Kimataifa kwa kupokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali duniani, na hatimae kutoa wahitimu wenye Ujuzi na stadi za maisha " alieleza Prof. Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda amezitaka Taasisi hizo kuhakikisha zina buni program mpya zitakazoendana na wakati pamoja na kuimarisha au kuanzisha mahusiano yenye tija baina yake na Taasisi za utafiti pamoja na sekta binafsi na kuweka utaratibu wa kuendeleza Teknolojia na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya Maendeleo ya kijamii.
Awali akizungumza kuhusu Maonesho hayo, Mkurugenzi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa amesema jumla ya Taasisi 83 za ndani na Nje ya nchi zimeshiriki ukilinganisha na Taasisi 75 zilizoshiriki Maonesho kwa mwaka uliopita.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. James Mdoe,akizungumza wakati wa Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila,akizungumza wakati wa Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa,,akizungumza wakati wa Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam