Na.Mwandishi Wetu-Manyara
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu amekagua maandalizi ya shughuli za kilele cha mbio za mwenge wa uhuru 2023 kitakachofanyika Oktoba 14, 2023 Mkoani Manyara.
Ziara hiyo imefanyika Julai 20, 2023 Mkoani humo ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Karoline Mthapula ambapo wamekagua uwanja wa Kwaraa kutakapo fanyika kilele cha maadhimisho hayo, Kanisa Catholic itakapo fanyika ibada ya Baba wa Taifa, uwanja wa stendi ya zamani itakapo fanyika wiki ya vijana na kukagua maendeleo ya vijana wa halaiki.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2023 zinaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.
Mbio za mwenge wa uhuru zilizinduliwa rasmi Aprili 2, 2023 Mkoani Mtwara na kilele chake kitafanyika Mkoani Manyara Oktoba 14, 2023, utakimbizwa katika mikoa 31 na Halmashauri 195 ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ina jukumu la kuratibu mbio za mwenge wa uhuru nchini.