KATIBU MKUU CHONGOLO ASEMA TANZANIA IKO KWENYE VITA VYA KIUCHUMI, INAHITAJI AKILI KUSHINDA


*Asisitiza umuhimu wa Watanzania kutunza amani, kutetea maslahi ya nchi.

*Asema hawatayumba wala kutolewa kwenye mstari, maadui wasipewe nafasi

Na Mwandishi Wetu, Tanga

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo amewaleza kuwa hivi sasa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani iko kwenye vita kubwa ya kiuchumi na ili kuishinda moja na mshikamano unahitajika huku akiwataka kuwa makini na wale wote wenye dhamira ovu kwa nchi yetu.

Aidha ametumia nafasi hiyo kufafanua hatua kwa hatua umuhimu wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam kama Ilani ya Uchaguzi Mkuu inavyoeleza na kwamba kuna baadhi ya watu wanataka kuutumia mjadala wa bandari kuvuruma amani ya nchi kwa kuwa wanako mahali pakukimbilia kama walivyokuwa wamekimbia miaka michache iliyopita.

Chongolo akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Korogwe na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Tanga amesema dunia iko kwenye mapambano ya vita ya kiuchumi na Tanzania nayo iko kwenye mapambano hayo hayo.

Akifafanua zaidi mbele ya wananchi hao amesema ni kweli uhuru wa nchi ulishapatikana baada ya kuondolewa kwa Wakolobi lakini kwa sasa Tanzania inapambana kujikomboa kiuchumi vita ambayo haionekani kwa macho waziwazi, hivyo akili inahitajika kukabiliana nayo na kushinda.

Aidha amesema akili, hekima na busara inahitajika huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza katika mapambano hayo nchi yetu iko imara na haitakubali kuyumbishwa na kutolewa kwenye mstari na wapinzani au maadui ambao hawalitakii mema Taifa la Tanzania.

"Hii vita ya kiuchumi ukikaa kienyeji umeenda na maji kwasababu fursa tunazopigania wote, kuzipata na kuzitumia ili kujiendeleza ni fursa za aina moja na zinapatikana kwenye maeneo yale yale.Kla mmoja anaiangalia fursa kwa jina lake, kwa jicho lake, kwa namna yake na kwa mazingira.”

Akiwa katika mkutano huo uliokuwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, likiwemo makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Dubai hasa katika uendeshaji Bandari ya Dar es Salaam Chongolo ametumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kulinda na kuitunza amani iliyopo nchini.

Chongolo amesema ni muhimu Watanzania kuilinda amani kwa kuwa hiyo ni miongoni mwa Tunu za Taifa hili na ndio imekuwa utambulisho wa Watanzania , hivyo tunu hiyo lazima ilindwe kwa nguvu zote." Wale wanaotaka kuvuruga amani yetu tusiwaonee aibu hata kidogo."

Amefafanua Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake aliwahi sema ukiulizwa Tanzania una nini, sema una amani huku ukijidai. "Amani hii si amani rahisi, si amani ya lelemama, kuna watu wametoka jasho na wanatoa jasho ili hii amani iwepo. Tusiache amani hii ipotee kwa sababu ya wajanja wachache wenye dhamira ovu kwa nchi yetu."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post