SERIKALI MBIONI KUANZISHA MINADA YA MADINI YA VITO




*Dkt. Biteko akagua Maendeleo ya Kitalu C na ujenzi wa Tanzanite Centre

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imekuja na utaratibu mpya wa kuanzisha minada ya madini kwa lengo la kupata wanunuzi wakubwa wakimataifa ili kuja kununua madini hayo kwa bei kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. 

Hayo yamebainishwa na Dkt. Biteko wakati akikagua maendeleo ya Kitalu C na ujenzi wa Tanzanite Centre katika eneo la Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

"Mheshimiwa Rais amekubali tuanzishe utaratibu wa kutafuta wanunuzi wakubwa wa madini waje ili mawe kidogo mnayopata yapate thamani kubwa kuliko  ilivyo sasa na tumepata mwekezaji mpya anaitwa Franone  ambapo kwa kipindi cha miezi sita amezalisha ajira 328," amesema Dkt. Biteko.

"Amesema utaratibu wa kufanya biashara ya madini ndani ya ukuta ni biashara huru na kuwataka wafanyabiashara wa madini ndani ya ukuta kuuza mawe yao kwa mtu wanayemtaka bila kusumbuliwa lakini pia jiwe linalotoka ndani ya ukuta lazima lihesabiwe na kujulikana thamani yake na sehemu linapokwenda," amesisitiza Dkt. Biteko.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopha Ole Sendeka, amempongeza Dkt. Biteko kwa kuleta utulivu   kwenye Sekta ya Madini na kumuomba aendelee kuwa balozi katika kuendeleza utulivu kwenye sekta hiyo. 

Pia, Ole Sendeka amesema kuwa katika Eneo Tengefu la Mirerani kuna changamoto kubwa ya barabara ya ndani ya ukuta ambayo inasababisha adha kubwa kwa wachimbaji wanao ingia kwenye migodi mbalimbali iliyopo ndani ya ukuta, na pia amemuomba Dkt. Biteko kusaidia upatikanaji wa maji ndani  ya ukuta wa Magufuli.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mirerani Bernard Msengi, amesema kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 ofisi yake imekusanya kiasi cha ha shilingi bilioni 2.6 sawa na asilimia 52 .2 3 ya lengo la makusanyo huku akieleza sababu zilizosababisha baadhi ya malengo kutofikiwa  ni pamoja na hali ya kijiolojia ya mashapo kuwa katika kina kirefu hivyo migodi mingi kutumia muda mrefu kufanya utanuzi na uwekezaji wa migodi pamoja na ukosefu wa teknolojia za kisasa kwa wachimbaji wadogo ndani ya eneo la ukuta. 

Pia amebainisha changamoto zilizopo katika eneo hilo la Mirerani kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma za kijamii yaani maji Safi na salama, umeme na  ukosefu wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya uchimbaji.

Aidha ameeleza mikakati waliojiwekea  ni kuongeza vituo vya madini ujenzi kwa ajili ya kupata wadau wengi  wanaofanya biashara ya madini ujenzi hasa ya mchanga na kokoto na ufuatiliaji wa karibu wa miradi inayorajiwa kuanzishwa muda si mrefu wa madini ya Kinywe yaliopo karibu la eneo la Mirerani.
 
Katika ziara hyo viongozi walioshiriki ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt. Suleiman Selela,  Afisa Tawala wa Mkoa wa Manyara Carolina Mithapula, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendekaka, Kamishna wa Madini Abdulrahman Mwanga , Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mmiliki wa mgodi  Kitalu C  Onesmo Mbise .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post