MBUNGE MTATURU MGUU KWA MGUU JIMBONINa Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameanza ziara yake katika Kijiji cha Nkuhi kwa lengo la kurudisha mrejesho baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 11,wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara Kijijini hapo Mtaturu amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka Shilingi Milioni 544 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari.

“Ahsante sana wananchi wenzangu wa Kijiji hiki kwa mapokezi yenu na kuupokea mradi wa ujenzi wa sekondari,tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hii mpya,niwaombe wananchi wenzangu tuunge mkono jitihada hizi na kamwe tusimuangushe,”amesema.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Issuna Stephano Missai amemshukuru Mbunge kwa kuwasemea na hatimaye Nkuhi wanaenda kupata shule mpya ya sekondari itakayoondoa changamoto ya watoto kutembea umbali wa zaidi ya km 13 kufuata shule.

"Mh Mbunge ahsante sana,hatua hii sio tu itawaondolea adha watoto wetu ya kutembea umbali mrefu,pia itaondoa utoro na mimba zisizotarajiwa kwa watoto wa kike,hapa tumetenga eneo lenye hekta 100 kwa ajili ya ujenzi huu na wananchi wameanza kusafisha na wapo tayari kutoa nguvu zao ili ujenzi ukamilike mapema,"ameeleza.

Nae Afisa Elimu wilaya Mwalimu Ngwano Ngwano amemshukuru mbunge kwa kuendelea kuibeba sekta ya elimu muda wote.

"Tulishajengewa shule mpya MosiMatongo na madarasa mengi kila shule,na hivi karibuni tumepokea Mil 110 ya kujenga nyumba 2 za walimu shule ya sekondari MosiMatongo,"amesema.

Amesema baada ya mapokezi ya fedha kwa ajili ya shule hiyo mpya Nkuhi halmashauri imetoa maelekezo tayari kuunda kamati za ujenzi na wataalam wa idara ya Elimu,Ardhi na Ujenzi wapo tayari kushirikiana na kamati zilizoundwa hapo kijijni ili kuwe na uwazi kwenye utekelezaji wa mradi huo lengo likiwa ifikapo October 30 mwaka huu ujenzi uwe umekamilika tayari kuanza shule rasmi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post