MGEJA ASHITUKIA MCHEZO MCHAFU WA KUITAKA KUICHAFUA SERIKALI


Khamis Mgeja

Na Mwandishi wetu -Kahama

KHAMIS MGEJA ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga amewatahadharisha wanachama wenzake wa CCM kutahadhari na michezo michafu inayofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi ya Tanzania.

Mgeja ametoa kauli hiyo juzi kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi ya kisasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ukumbi wa mikutano ya kijiji cha Wame kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambapo yeye binafsi alichangia matofali 200 na fedha taslimu shilingi 100,000.

“Niwapongeze viongozi wetu wa CCM wa Tawi hili la Wame, kwa kweli wameona mbali kuitisha harambee hii, maana Tawi hili limo ndani ya kata ya Kilago ambayo mimi ndiye mwakilishi wake katika mkutano mkuu wa CCM wa mkoa, hivyo lazima Ofisi zetu za chama ziwe ni zile zenye ubora, na iwe mfano kwa wengine,” alieleza.

Akizungumzia kuhusu upotoshaji wa baadhi ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali Mgeja alisema ni ukweli usiopingika kwamba Serikali ya awamu ya sita ina nia njema ya kuwaletea wananchi wake maendeleo lakini bado kuna kundi la watu wachache wanaopotosha ukweli wa mambo yanayotekelezwa.

Akitoa mfano kuhusu upotoshaji huo alisema ni suala la Bandari linakuzwa na kupotoshwa ukweli wake huku ikidaiwa kwamba Bandari ya Dar es Salaam imeuzwa lakini siyo kweli, na kwamba hakuna Serikali yoyote duniani inayoweza kuuza ardhi ya wananchi wake kwa watu wengine lengo ikiwa ni kuichafua Serikali na ichukiwe na wananchi wake.

Mgeja ambaye ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga alisema yeye binafsi amebaini kuwepo kwa mchezo mchafu ambao umelenga zaidi kutaka kuwagombanisha watanzania na Serikali yao kwa kusambaza uongo ili wananchi waone hakuna kinachofanyika.

Alisema wanaosambaza habari za uongo mfano huo wa Bandari lengo lao ni kuwatoa watanzania katika kufikiria mambo muhimu ya kimaendeleo yanayotekelezwa na Serikali hivi sasa na badala yake wabaki wakiishutumu Serikali kwa madai haina jambo lolote la maana inalolitekeleza katika kuwaletea maendeleo tarajiwa.

“Nichukue nafasi hii kuwaomba na kuwatahadharisha watanzania wenzangu na wana CCM kwa ujumla, kwa sasa tunapita kwenye kipindi kigumu sana, hivyo lazima tuwe makini tuwaepuka na kuwaogopa kama ukoma wale wanaotutengenezea michezo michafu kwa lengo la kutaka kuichafua Serikali iliyoko madarakani hivi sasa,”

“Yapo baadhi ya mambo yanapotoshwa sana, mfano suala hili la bandari, limekuzwa ili tu lionekane halifai na Serikali imefanya “kituko” kikubwa kutaka kuibinafsisha, hadi watu wamefikia hatua ya kutoa lugha zisizokuwa za staha, kwa mfano kudai suala la bandari watu walitumia akili za matope, hii haikubaliki,” alieleza Mgeja.

Alisema kitendo cha kuendeleza mashambulizi dhidi ya Serikali na Bunge ni kutaka kumchafua Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mhimili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku wakijitahidi kuhamisha mawazo ya watanzania wajikite zaidi kwenye malumbano yasiyokuwa na maana badala ya kuwaza maendeleo.

“Sasa ndugu zangu niwaulize jambo moja hivi kweli kuna Serikali yoyote duniani inayoweza kudiriki kuuza nchi yake? Inashangaza kabisa wenzetu hawa suala la bandari ndiyo wamelivalia njuga, wanapiga kelele wakidai eti bandari imeuzwa, bandari imeuzwaaa, niwaombe watanzania na wana CCM wote wenye nia njema wapuuze kauli hizi za upotoshaji,”

“Haiwezekani wala haitatokea, Serikali hii ya CCM kuamua kuuza hata kipande kimoja cha ukubwa wa sentimeta moja ya ardhi kwa mtu ye yote asiyekuwa mtanzania, zipuuzeni hizi kelele za bandari imeuzwa, siyo kweli, na Serikali imetoa ruhusa kwa ye yote mwenye mawazo zaidi ya kuiendesha vizuri basi ajitokeza na apeleke ushauri wake,” alieleza Mgeja.

Aliwaomba watanzania wote wenye nia njema na nchi yao waendelee kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ili iendelee kuwaletea maendeleo badala ya kuiwekea vikwazo mbalimbali huku wakiikosoa pasipo utaratibu kwa kutumia maneno yasiyokuwa na staha dhidi ya viongozi wake wa Chama na Serikali.

Mgeja alitoa wito kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini kote wawe mabalozi wazuri wa kuwaelimisha watanzania kuhusu mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali ya Rais Samia na kwamba suala la bandari linazungumzika na kila mwenye ushauri mzuri wa jinsi ya kuiendesha au kuingia mikataba mizuri na wawekeza amekaribishwa kutoa maoni yake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post