TANZANIA, KENYA ZASAINI MAKUBALIANO KUENDELEA NA UIMARISHAJI MPAKA WA KIMATAIFA


Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Hamdouny Mansoor (Kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa Kenya Juster Nkoroi (Kulia) wakisaini hati ya Makubaliano ya Mpango kazi wa utekelezaji wa kuendelea na awamu ya tatu ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo kutoka Namanga Arusha hadi Tarekea Kilimanjaro mwishoni mwa wiki jijini Arusha.

*************

Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA

Tanzania na Kenya zimesaini Hati ya Makubaliano Mpango Kazi wa utekelezaji wa kuendelea na kazi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo kipande cha awamu ya tatu kutoka Namanga mkoani Arusha hadi Tarakea, Kilimanjaro wenye urefu wa km 110.

Hatua hiyo inafuatia kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kilichokaa kwa siku tano jijini Arusha kuanzia tarehe 29 Mei 2023 hadi Juni 2, 2023 kupokea taarifa ya ukaguzi wa kipande cha awamu ya tatu, kufanya ukaguzi eneo linaloimarishwa pamoja na kuandaa mpango kazi wa awamu zinazofuta.

Utiaji saini makubaliano ya mpango kazi baina ya pande hizo mbili ulifanyika mwishoni mwa wiki mkoani Arusha kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor na Juster Nkoroi, Afisa Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO) na kushuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Lucy Kabyemera.

Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa ni kuendelea na uimarishaji mpaka awamu ya tatu kipande cha km 110 (Namanga-Tarakea), Kuwa na kikao Cha Kamati ya Wataalam (JTC) mwezi Septemba 2023 ili kupokea taarifa ya kazi ya uwandani pamoja na timu za wataalamu kukutana na kuandaa taarifa na rasimu ya Mpaka ulioimarishwa.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera amesifu kazi iliyofanywa na wataalamu wa pande hizo mbili hadi kufikia muafaka wa kuendelea na kazi ya awamu ya tatu na kuahidi kuwa, serikali ya Tanzania iko bega kwa bega kuhakikisha zoezi linafanikiwa.

"Nichukue fursa hii kuwahakikishia wataalamu wa pande zote kuwa, serikali iko committed kuhakikisha kazi hii inakamilika kama tulivyokubaliana" alisema Lucy Kabyemera.

Kwa upande wake Balozi Mdogo wa Kenya mwenye makazi yake jijini Arusha, Tanzania Balozi Dennis Mburu amesema, makubaliano yaliyofikiwa yanaonesha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizo mbili na ni imani yake uhusiano huo utaendelea kudumu.

"Zoezi linaloendelea la uimarishaji mpaka ni ishara ya mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili na Kenya inaunga mkono zoezi hili kwa manufaa ya nchi zetu" alisema Balozi Mburu

Awali katika siku yake ya pili ya kikao, Kamati ya Pamoja ya Wataalamu wa nchi hizo mbili ilitembelea eneo la mpaka wa kimataifa lililopo mto Losoyai mkoani Kilimanjaro unaoungana na Ruvu kuingia ziwa Jipe na kufuatiwa na mpaka wa nchi kavu hadi Pangani kwa lengo la kujiridhisha.

Wakiwa katika eneo hilo, Kamati hiyo ya wataalamu ikioongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Mansoor na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa ya Kenya (KIBO) Juster Nkoroi walijionea uhalisia wa mpaka pamoja na changamoto za eneo hilo.

kikao cha siku tano kilichofikia makubaliano ya kuendelea na kazi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa awamu ya tatu kimepokea taarifa ya awali ya ukamilishaji kazi zote za awamu ya kwanza na ile ya pili yenye jumla ya km 348 ambazo tayari zimeimarishwa.

Aidha, kikao hicho pia kimeandaa mpango kazi kwa awamu zinazofuata za nne na tano kuanzia eneo la Tarakea mkoani Kilimanjaro hadi Jasini wilayani Mkinga mkoa wa Tanga eneo lililopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi linalokamilisha jumla ya kilomita 758 za nchi kavu za mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Hamdouny Mansoor (Kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa Kenya Juster Nkoroi (Kulia) wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Kuendelea na Awamu ya Tatu ya Uimarishaji Mpaka wa kimataifa kati ya ya nchi hizo kutoka Namanga Arusha hadi Tarekea Kilimanjaro mwishoni mwa wiki mkoani Arusha.


Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Hamdouny Mansoor (Kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa Kenya Juster Nkoroi (Kulia) wakionesha Hati ya Makubaliano ya Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Kuendelea na Awamu ya Tatu ya Uimarishaji Mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo kutoka Namanga Arusha hadi Tarekea Kilimanjaro mara baada ya kusaini mwishoni mwa wiki jijini Arusha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera akifunga kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) baina ya Tanzania na Kenya kilichofanyika mwishoni mwa wiki mkoani Arusha.
Sehemu ya Washiriki wa kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kati ya Tanzania na Kenya kilichomalizika mwishoni mwa wiki jijini Arusha. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post