SERIKALI KUFANYIA TATHMINI UTENDAJI WAKE


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza wakati akifungua kikao cha Wadau wa Maendeleo kuhusu kuimarisha Ufuatiliaji na Tathimini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali


Na; Mwandishi Wetu - DODOMA

IDARA ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji, Serikali Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu,  ina jukumu kubwa la kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa sera, mipango, programu, miradi na mikakati mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Serikali.

Hayo yamesemwa leo 9 June 2023, na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga alipofungua mkutano wa wadau wa maendeleo ambao pamoja na mambo mengine, ulijadili swala zima la tathmini na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali pamoja na kongamsno la wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini  na mafunzo itakayofanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu.

Mhe. Nderianaga alisema, baada ya Serikali kufanya maboresho ya Muundo wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) 2022/23,  Idara hiyo  mpya iliyoanzishwa, ndiyo inahusika moja kwa moja na kuandaa taarifa za utendaji wa Serikali za kila robo mwaka, nusu mwaka na taarifa za mwaka ikiwemo taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa ndani ya Taasisi za Umma na utekelezaji wa Malengo ya kimataifa na kikanda  na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika. 

“Taarifa hizi, zitaonesha mwenendo na mwelekeo katika utendaji wa majukumu ya taasisi zote za Umma zikiwemo Wizara, Idara za Serikali zinazojitengemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa”. Alisisistiza Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri aliendela kusema kuwa ,Taarifa ya mwaka ya utendaji wa Serikali itakuwa ikisomwa Bungeni kuanzia mwaka ujao wa fedha (2023/24) ili kutoa taswira halisi ya uwazi na uwajibikaji wa Taasisi zote za Serikali kwa Wananchi.

 “ili kuwezesha Ofisi kupata taarifa hizi, itakuwa inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa viashiria vya utendaji kazi na kutoa taarifa katika ngazi mbalimbali.” Alifafanua

Awali, Naibu Waziri Nderiananga alisema kuwa Ofisi hiyo ipo maandalizi ya Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 12 – 15 Septemba, 2023 Mkoani Arusha, Kongamano ambalo  litawaleta  pamoja, wadau wa maendeleo wa ufuatiliaji na tathmini ya Utendaji kazi ili kupashana habari na kupeana uzoefu wa namna ya kusimamia utekelezaji wa mipango, programu na miradi mbalimbali na kuonesha namna inavyosaidia jamii. 
.

Baadhi ya Wajumbe wakifuatilia kikao hicho

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post