RITA KUTOA HUDUMA ZA MAFUNZO YA UANDISHI,UTUNZAJI WOSIA


Na Dotto Kwilasa,Dodoma.

Ili kupunguza ongezeko la migogoro ya familia ambayo mara nyingi hupelekea vifo,Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umeanzisha huduma ya kutoa mafunzo ya uandishi na utunzaji wa wosia.

Msajili wa RITA, Emmy Masunga, ameeleza hayo jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo kwenye maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili mkuu wa Serikali.

Kutokana na hayo amewataka Watanzania kujenga tabia ya kuandika wosia wanapokuwa hai ili kuwaondolea shida wategemezi wao pindi wanapo fariki dunia.

Msajili huyo pia amewataka Watanzania kuondokana na imani potofu kuwa mtu akiandika wosia anajitabiria kifo bali watumie fursa hiyo kwa ajili ya manufaa ya familia zao kupata kile wanacho stahili wakati wanapokuwa hawapo Duniani kwakuwa mtoa wosia anayonafasi ya kufanya marekebisho kila mara anapohitaji.

Amesema, wakala huo ulianzisha huduma ya ushauri, kuandika na kuhifadhi wosia mara baada ya kubaini kuongezeka kwa tatizo la wajane na watoto kupoteza mali za marehemu ambaye hakuacha wosia.

"Mzazi au mlezi anaposhindwa kuandika Wosia husababisha watoto wengine kushindwa kuendelea na masomo na familia kushindwa kupata mahitaji muhimu,Kuna wakati ugomvi wa kifamilia unakuwa mkubwa na kupelekea vifo”amesema Masunga na kuongeza;

Tunataka jamii kuona umuhimu wa kuandika wosia wanapokuwa hai ili kuwasaidia watoto wao kupata haki zao tofauti na ilivyo sasa ambapo pamekuwa na matukio mengi ya familia kupotea haki zao kutokana na ndugu kupokonya mali za wajane na watoto wa marehemu”anasema

Akieleza faida za kuandika wosia amesema ni pamoja na kuepusha watoto au mke/mme kunyang’anywa mali na kumwezesha mwandishi kumchagua msimamizi wa mirathi.

“Pia inaepusha migogoro katika familia ndugu au jamaa, unakupa uhakika wa maisha bora ya baadaye ya warithi wako kulingana na mali ulizonazo, kupunguza usumbufu na gharama wakati wa kuendesha mirathi”anafafanua

Ameeleza kuwa  taarifa zinazopaswa kuandikwa kwenye wosia ni pamoja na msimamizi wa mirathi,wapi mtoa wosia angependa azikwe,idadi ya mali za marehemu na mgawanyo wa mali za marehemu.

Masunga amesema zipo aina mbili za wosia ambazo ni wosia wa maandishi na wosia wa matamshi/mdomo na anayetakiwa kuandika wosia ni mwananchi yeyote awe na umri wa miaka 18 na kuendelea, awe na akili timamu na wosia uwe wa maandishi au matamishi.

"Lazima Wosia ushuhudiwe na watu wanne ukiwa ni wa matamshi, wosia usimnyime mrithi halali wa mali bila sababu zinazotambulika kisheria na uwe umeshuhudiwa na mwanasheria”amesema

Hata hivyo, alisema RITA imeanzisha mfumo wa kutoa huduma kidijitali unaofahamika kama eRITA ambao unamwezesha mtu yeyote kupata huduma sehemu yoyote kwa kutumia simu yake ya mkononi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post