MZIMU WA SEIF WAZIDI KUITAFUNA CWT

 
Wakili wa Chama cha walimu nchini (CWT) Paschal Msafiri akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati tendaji ya CWT-TAIFA Mwalimu Tobias Sanga akizungumza leo June 6,2023 na na Waandishi wa habari  kuhusu sakata la ukiukwaji wa miongozo ya Chama hicho.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

HIVI ndivyo unaweza ukasema!!Mzimu wa aliyekuwa Katibu mkuu wa CWT-Taifa Deus Seif bado unakitesa Chama hícho kutokana na migogoro ya hapa na pale Hali iliyopelekea leo June 6,2023 Kamati tendaji ya Chama hicho kuibuka na kuazimia kwa pamoja kuweka zuio kwa Katibu Mkuu wao Japhet Maganga kuendesha shughuli zozote katika masuala ya fedha na utawala.


Hatua hiyo ni kufuatia kuwepo kwa madai ya uongozi wa Juu kuvunja Katiba ya CWT hivyo Kamati hiyo kuelekeza shughuli zote za CWT kufanywa na Naibu Katibu Mkuu Joseph Msalaba mazimio yaliyofanywa na Wajumbe wa Kamati 18 toka mikoa 18 nchini.


Wakiongea mbele ya Waandishi wa Habari Jijini hapa mara baada ya kukutana nje ofisi za chama hicho kwa zuio la kutotakiwa kuingia ndani,wamesema wamejiridhisha kuwa uongozi uliopo madarakani unavunja Katiba na kanuni zake.


Akizungumza kwa niaba ya wengine Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo na mwakilishi wa walimu wa Mkoa wa Njombe Mwl.Tobias Sanga alisema kikao hicho kimeridhia kumzuia Katibu Mkuu wa CWT kutoendesha shughuli za Chama hicho Kutokana na uonevu anaoufanya kwa wanachama wake.


Amefafanua kuwa moja ya ajenda ya kikao hicho ni uhamisho holela wa wafanyakazi, kuhusu matumizi holela ya michango ya walimu pamoja kutaka mkutano Mkuu wa dharula bila mafanikio .


"Tumejiridhisha na tumeona utendaji kazi wa Katibu huyu hauko sawa,tumepitia miongozo yetu tumejiridhisha,tunachukizwa kuona fedha za 2% za walimu zinatumika bila utaratibu,tukihoji hatupewi Ushirikiano,"alisema Mwalimu huyo.


Pamoja na mambo mengine Sanga amesema,"Kwa Mamlaka tuliyonayo tumekubaliana kazi zetu zitafanywa na Naibu Katibu mkuu ambaye atasimamia masuala yote ya utawala na fedha,"alisisitiza.


Alifafanua kuwa,"Naomba nieleweke wazi kuwa hatuna shida na Katibu Mkuu ila tunachotaka ni mfumo wa utendaji,tunataka walimu tunao wawakilisha wapate haki zao na sio unyanyasaji unaoendelea,"amesema


Naye Naibu Katibu Mkuu wa CWT-Taifa Joseph Msalaba ambaye ndiye amepewa Mamlaka ya utendaji amesema kuwa amelipokea suala hilo na kueleza kuwa kikao hicho kimefanyika kwa amani kama ilivyotarajiwa.


Anasema "nimepokea uwepo wa ujio wa Wajumbe hawa 18 wa Kamati ya utendaji Taifa japo walitakiwa kuwa 38 lakini hakuna kilicho haribika,"amesema


Naye Mwalimu Sabina Lipukila ambaye ni mwakilishi wa walimu wa Ruvuma alisema mgogoro uliopo unasababisha utendaji kazi wa walimu kushuka na kusisitiza kuwa kwa ujumla Katiba yao haiendi wanavyotaka.


Anasema uhamisho wa Makatibu unafanywa kiholela bila wao kushirikishwa na kueleza kuwa jambo hilo linashusha ari ya kufanya kazi kwa weledi Kutokana na hofu ya uhamisho.


"Hakuna asiyefahamu kuwa sisi ni chombo cha ajira,kuna vitu vingi tunavifuatilia haviendi sawa,kwa muda mrefu sasa tumekuwa tunaomba kikao lakini tumenyimwa,tungekubaliwa vikao haya yote tungezungumza na kuyamaliza kule,"amefafanua


Hata hivyo kabla ya kuanza kikao hicho baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya utendaji walizuiwa kuingia ndani ya Ofisi za chama hicho Kwa masaa sita jambo ambalo walinzi katika Ofisi hizo kwa madai kuwa ni maelekezo toka juu.

Kutokana na hayo Wakili wa kujitegemea na mwanasheria wa CWT-TAIFA Pasco Msafiri amesema kuwa kitendo hicho ni uvunjwaji wa Katiba na kwamba hakikubaliki.


Amesena,"kinachoendelea Katika chama Hiki ni uvunjwaji wa kikatiba ya Sheria ya chama Cha walimu Tanzania, kwa mujibu wa katiba wajumbe wa kamati taifa Wana vikao viwili January na July hivyo kinachofanyika Si sahihi,"amefafanua


Pia ameongeza kwa kusema kuwa katiba ya Sheria imempa mamlaka katibu mkuu kumuhamisha mtendaji mkuu yoyote kuamia sehemu ingine kiutendaji .


Mwisho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post