TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2022 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2023/24Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024, bungeni jijini Dodoma.

 

  


 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

 

 

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO,

MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA

HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2022 NA 

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2023/24

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

DODOMA                                                           15, JUNI, 2023 UTANGULIZI

 

1.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa

Mwaka 2023/24. Pamoja na hotuba hii, nawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24. Taarifa zilizopo katika vitabu hivi, ndiyo msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 nitakayoiwasilisha katika Bunge lako

Tukufu leo alasiri.

 

2.         Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kukutana tena kwa mara nyingine katika Bunge hili baada ya majadiliano ya bajeti za mafungu mbalimbali. 

 

3.         Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa, nitoe pongezi zangu za dhati; kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti aliouonesha tangu alipoingia madarakani. Kupitia uongozi wake mahiri, tumeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali ikijumuisha sekta za uzalishaji, huduma za jamii na miundombinu wezeshi. Aidha, Mheshimiwa Rais amefanikiwa kuimarisha hali ya kisiasa nchini na mahusiano ya kimataifa. Hakika nchi yetu imebarikiwa kuwa na Rais mwenye maono makubwa katika kuboresha ustawi wa maendeleo wa nchi pamoja na watu wake. HAKIKA MAMA HANA BAYA.

4.         Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri na jitihada zao katika kuhakikisha Taifa letu linakuwa na maendeleo endelevu. 

 

5.         Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya

Tanzania na mhimili mzima wa utoaji wa haki kwa kazi nzuri wanayoifanya. Aidha, pongezi za pekee ziwaendee Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kusimamia ulinzi na usalama wa nchi na hivyo kuwezesha shughuli za kiuchumi nchini kufanyika kwa amani, usalama na utulivu.

 

6.         Mheshimiwa Spika, vile vile naomba nikupongeze wewe binafsi, na Mheshimiwa Mussa Azan Zungu (Mb.), Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb), Mheshimiwa Sillo Daniel Baran (Mb) na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb) kwa kuliongoza Bunge letu Tukufu kwa weledi mkubwa. Aidha, napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mheshimiwa Sillo Daniel Baran (Mb) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua (Mb.) kwa ushauri wao mahiri wakati wa uandaaji wa taarifa nilizowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu leo hii. Maoni na ushauri wao umezingatiwa kikamilifu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/24 ambao utekelezaji wake utaanza tarehe 01 Julai, 2023. 

7.         Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuhudumu katika nafasi ya Waziri wa Fedha na Mipango. Ninamuahidi kuwa nitaendelea kutekeleza wajibu wangu na kufanya kazi kwa uaminifu, ufanisi na weledi mkubwa ili kutimiza matarajio yake aliyonayo kwangu na Wizara ya Fedha na Mipango. Ninawashukuru pia, wanachama wenzangu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna tunavyoendelea kushirikiana katika kukiimarisha zaidi chama chetu na kuhakikisha tunatekeleza yale yote yaliyokusudiwa katika Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2021/22 – 2025/26 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Aidha, kipekee napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Iramba Magharibi kwa kuzidi kunitia moyo na kushirikiana nami katika utekelezaji wa majukumu yangu ya kila siku.

 

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2022

 

Uchumi wa Dunia

 

8. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2023 inaonesha kuwa, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imepungua kutoka asilimia 6.3 mwaka 2021 hadi asilimia 3.4 mwaka 2022. Upungufu huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi wa China na India; madhara ya janga la UVIKO-19; vita kati ya Urusi na Ukraine; na sera za kupunguza ukwasi katika chumi za Ulaya ili kukabiliana na mfumuko wa bei.

Aidha, Uchumi wa dunia unatarajiwa kupungua zaidi na kufikia ukuaji wa asilimia 2.8 mwaka 2023 kutokana na kuendelea kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, mabadiliko ya Tabia Nchi na Sera za Marekani kuongeza riba.

 

Uchumi wa Afrika na Kikanda

 

9. Mheshimiwa Spika,  ukuaji wa uchumi kwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ulipungua kufikia wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2021. Aidha, ukuaji wa Pato la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ulikua kwa wastani  wa asilimia 4.1 ikilinganishwa na  ukuaji wa wastani wa asilimia 5.3 mwaka 2021. Vile vile, wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikuwa ni asilimia 5.3 mwaka 2022 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2021. Upungufu huo ulitokana na madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine uliyosababisha mfumuko wa bei za nishati ya mafuta na vyakula. 

 

Uchumi wa Taifa

 

Pato la Taifa

 

10.      Mheshimiwa Spika,  Mwaka 2022, thamani halisi ya Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2015 lilifikia shilingi trilioni 141.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 135.5  mwaka 2021.  Aidha, kiwango halisi cha ukuaji wa pato la Taifa kilifikia asilimia 4.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2021. Kiwango hicho cha ukuaji kilitokana na: mikakati iliyochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za vita nchini Ukraine; uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini; kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi; na kuongezeka kwa shughuli za utalii. Sekta zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji kwa mwaka 2022 ni pamoja na: sanaa na burudani (asilimia 19.0); madini (asilimia 10.9); fedha na bima (asilimia 9.2); malazi na huduma ya chakula (asilimia 9.0); na umeme (asilimia 7.6). Aidha, kutokana na hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali thamani ya Pato ghafi la Taifa linatarajiwa kufikia dola za Marekani bilioni

85.42 mwaka 2023/24.

 

11.      Mheshimiwa Spika, Mwaka 2022, Pato ghafi la Taifa (kwa bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi trilioni 170.3 (sawa na Dola za Marekeni bilioni 77.6) ikilinganishwa na shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021 (sawa na Dola za Marekani billioni 69.94). Aidha, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa 59,851,347 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu 57,724,380 mwaka 2021. Hivyo, Pato la Taifa kwa Mtu (GDP per capita) kwa mwaka 2022 lilikuwa shilingi 2,844,641 ikilinganishwa na shilingi 2,708,999 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 5.0. Kiasi hicho ni sawa na dola za Marekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani 1,173.3 mwaka 2021. Hali hii inaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini.

 

 

Mwenendo wa Mfumuko wa Bei

 

12. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nchini umeendelea kuwa ndani ya lengo la wigo wa kuwa chini ya asilimia 5. Mwaka 2022, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 4.3 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2021. Aidha, mfumuko wa bei hadi mwezi Mei, 2023 umebaki kama ilivyokuwa katika kipindi hicho hicho mwaka 2022 ikiwa ni wastani wa asilimia 4.0. Hali hii imesababishwa na kuongezeka kwa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma; na kuongezeka kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya maeneo nchini na nchi jirani kulikosababishwa na upatikanaji wa mvua katika maeneo yanayotegemea mvua.

 

Ujazi wa Fedha

 

13. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kukabiliana na hatari ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei linalotokana na mitikisiko ya kiuchumi duniani bila kuathiri kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Kutokana na utekelezaji wa sera hiyo, ukuaji wa ujazi wa fedha ulikuwa ndani ya malengo ambapo katika kipindi kilichoishia Aprili 2023, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa asilimia 17.2 na kufikia shilingi bilioni 39,961.5 kutoka shilingi bilioni 34,087.8 mwezi Aprili 2022. Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) ulikua kwa asilimia 15.6 hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 31,048.8 mwezi Aprili 2023 kutoka shilingi bilioni 26,861.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Mwenendo wa Viwango vya Riba

14. Mheshimiwa Spika, viwango vya riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi kwa mwaka 2023 vimeendelea kupungua na kufikia wastani wa asilimia 15.91 mwezi Aprili 2023 ikilinganishwa na asilimia 16.31 Aprili 2022. Vilevile, wastani wa viwango vya riba za amana za muda maalumu na za mwaka mmoja ulipungua hadi asilimia 6.79 kutoka asilimia 6.81 mwaka 2022. Mwenendo huu ulichagizwa na utekelezaji madhubuti wa sera wezeshi ya Fedha.  

 

Sekta ya Nje 

 

15.      Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023, urari wa malipo yote ya nje ulikuwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 4,414.2. ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 2,516.1 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022. Hii ilichangiwa na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kutokana na athari hasi za kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na ugavi wa bidhaa duniani ikilinganishwa na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Urari wa biashara ya bidhaa ulikuwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 6,065.6 kwa kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 3,556.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

 

16.      Mheshimiwa Spika urari wa biashara ya huduma ulikuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 2,198.7  kwa kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni 1,585.1 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022, sawa na ongezeko la  asilimia 38.7. Hii ilitokana na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii na usafirishaji kulikosababishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia kutokana na kupungua kwa athari za UVIKO-19. Vile vile, urari wa biashara ya bidhaa na huduma ulikuwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 3,866.9 kwa kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 1,971.7 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

 

Akiba ya Fedha za Kigeni

 

17. Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Hadi kufikia Aprili 2023, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 4.88 ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi 4.4. Mahitaji ya nchi kisheria ni kuwa na kiasi cha fedha za kigeni kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa muda usiopungua miezi 4.0.

 

Mwenendo wa Thamani ya Shilingi

 

18. Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za nchi washirika wakuu wa kibiashara imeendelea kuwa tulivu, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiuchumi duniani hususan ongezeko la bei za bidhaa. Hali hii imetokana na utulivu wa mfumuko wa bei nchini ukilinganishwa na nchi washirika wetu wa kibiashara, utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na uwepo wa chakula cha kutosha nchini. Katika mwezi Aprili, 2023 dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,324.07 ikilinganishwa na shilingi 2,322.16 kipindi kama hicho mwaka 2022. Aidha, katika kipindi cha kuanzia Aprili 2022 hadi Aprili 2023 dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,310.14.

Mwenendo wa Sekta ya Kibenki

19.      Mheshimiwa Spikasekta ya benki nchini imeendelea kubaki imara, himilivu na yenye kutengeneza faida ikiwa na mtaji na ukwasi wa kutosha katika kutoa mikopo kwa sekta za uchumi na kupunguza umaskini. Mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kufikia shilingi bilioni 28,702.95 kwa mwaka ulioishia Aprili 2023 kutoka shilingi bilioni 23,422.5 Aprili 2022 sawa na ongezeko la asilimia 22.5. Aidha, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulifikia wastani wa asilimia 15.8 katika kipindi cha Aprili 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 9.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2022 na lengo la asilimia 10.7 kwa mwaka 2022/23.  Ukuaji huu umechochewa na utekelezaji wa sera wezeshi za fedha na bajeti, pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo ulipaji wa malimbikizo ya madai na  jitihada nyingine za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hali iliyochochea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini. Aidha, kiwango cha mikopo chechefu kiliendelea kupungua na kufikia wastani wa asilimia 5.5 Aprili, 2023 kutoka asilimia 8.3 Aprili, 2022.

20.      Mheshimiwa Spika, utendaji wa sekta ndogo ya bima ulikuwa wa kuridhisha ambapo hadi kufikia Machi 2023, iliandikisha na kutoa leseni 1,196 zikijumuisha kampuni za bima, kampuni za uwakala na wadau wote wanaohusika na biashara ya bima nchini. Aidha, kwa upande wa sekta ndogo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, mtaji wa soko la hisa kwa kampuni za ndani, uliongezeka kwa asilimia 16.97 Machi 2023 na kufikia shilingi trilioni 10.82 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.25 katika kipindi kilichoishia Machi 2022. Vilevile, uwekezaji  kwenye Mifuko ya  UTT AMIS uliongezeka na kufikia shilingi trilioni 1.44 katika kipindi kilichoishia Machi 2023, ikilinganishwa na shilingi bilioni 852.21 katika kipindi kilichoishia Machi 2022 sawa na ongezeko la asilimia 69.17.

 

21.      Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha ambapo hadi kufikia Machi, 2023, ilitoa jumla ya leseni 1,187 kwa Watoa huduma daraja la pili ikilinganishwa na jumla ya leseni 736 zilizotolewa Machi 2022, leseni 780 kwa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo ikilinganishwa na leseni 615 zilizotolewa machi 2022 nakusajili vikundi 37,937 vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ikilinganishwa na vikundi 24,835 vilivyokuwepo Machi 2022. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa mafunzo kwa waratibu 115 wa biashara ya huduma ndogo za fedha kutoka katika mikoa 13 mwezi Mei, 2023. Vilevile, watoa huduma ndogo za fedha Daraja la Pili walikopeshwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 870 kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.

 

 

Deni la Serikali

 

22.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2023, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 79,100.19 sawa na ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 69,440.01 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi bilioni 51,162.60 na deni la ndani ni Shilingi bilioni 27,937.59. Ongezeko la deni limetokana na: kupokewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya. Aidha, Tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba, 2022 imeonesha kuwa deni ni himilivu na viashiria vya deni viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

 

23.      Mheshimiwa Spika, mnamo Machi 2023, kampuni za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service zilianza zoezi la kuifanyia nchi tathmini ya kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa. Zoezi hilo lilikamilika ambapo kampuni ya Moody’s Investors Service ilichapisha matokeo ya tathmini hiyo mwezi Mei 2023 na kampuni ya Fitch Ratings mwezi Juni 2023. Kwa mujibu wa matokeo hayo, Tanzania imewekwa katika daraja la B2 POSITIVE na Kampuni ya Moody’s Investors Service na daraja la B POSITIVE na Kampuni ya Fitch Ratings ambayo yanaashiria taswira chanya kwa nchi kimataifa. Pamoja na mambo mengine, matokeo hayo yamechangiwa na mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi, usimamizi makini wa deni la Taifa, kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na kuleta maridhiano ya kisiasa ndani ya nchi. Kukamilika kwa zoezi hilo,  kutaiwezesha nchi kutambulika katika masoko ya fedha ya kimataifa na hivyo, kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa Serikali na sekta binafsi.

 

24.      Mheshimiwa Spikamaelezo ya kina kuhusu taarifa ya hali ya uchumi yanapatikana katika Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022.

 

MAFANIKIO         YA   UTEKELEZAJI         WA MPANGO        WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2022/23

 

25. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu Serikali imekuwa ikitekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 ambao ni wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.  Utekelezaji wa Mpango huu umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na uongozi mahiri wa Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023 katika sekta mbalimbali ni pamoja na:

 

(i)           Miundombinu ya Reli: Kuendelea na ujenzi wa njia ya Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa ambapo kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) utekelezaji umefikia asilimia 98.14; kipande cha Morogoro

– Makutupora (km 422) utekelezaji umefikia asilimia

93.83; kipande cha Makutupora - Tabora (km 371) asilimia 7.0; kuanza kwa ujenzi wa kipande cha Tabora - Isaka (km 165) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 2.39; na ujenzi wa kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) umefikia asilimia 31.07. Aidha, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ununuzi wa mabehewa 22 ya abiria kwa ajili ya reli ya kati; kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa 52 ya mizigo na mabehewa sita (6) ya abiria na kuanza kutoa huduma katika reli ya kati; na  kukamilika kwa uboreshaji wa mfumo wa mawasiliano na umeme katika njia ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

 

(ii)          Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia asilimia 86.89 ambapo ujenzi wa handaki la kuchepusha maji (diversion tunnel) na ujenzi wa kingo ndogo za juu na chini umekamilika. Aidha, ujenzi wa ukuta wa bwawa kuu umefikia asilimia 94.85, handaki la kupeleka maji kwenye mitambo (power waterway) (asilimia 99.08), jengo la mitambo (power house) (asilimia 68.30), kituo cha kupokea na kusafirishia umeme (switchyard) (asilimia

98.87), kingo saidizi za kuzuia maji yasitoroke (asilimia 84.47). Vile vile, zoezi la ujazaji maji katika bwawa linaendelea ambapo hadi tarehe 23 Mei, 2023, kimo cha maji ya bwawa kimefikia mita 160.51 ambapo ili kuweza kuzalisha umeme, kiwango cha chini cha maji kinatakiwa kufikia mita 163 kutoka usawa wa bahari.

 

(iii)        Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania: Kufanyika kwa sehemu ya malipo ya ununuzi wa ndege nne (4) ambazo ni ndege moja (1) aina ya Boeing 767-300F ya mizigo iliyowasili tarehe 03 Juni, 2023, ndege mbili (2) aina ya Boeing 737-9 Max zinazotarajiwa kuwasili Agosti 2023 na Desemba 2023 na ndege moja (1) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner inayotarajiwa kuwasili Februari, 2024; na kuendelea na ukarabati wa miundombinu katika karakana ya KIMAFA katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KIA) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 85.0. Aidha, ATCL imeendelea kutoa huduma ya usafiri wa anga katika vituo 24 ambapo vituo 14 ni vya ndani ya nchi na vituo 10 ni vya nje ya nchi. Vituo vya ndani ya nchi ni Arusha; Bukoba; Dar es Salaam; Dodoma; Geita; Kilimanjaro; Kigoma; Songwe; Mpanda; Mtwara; Mwanza; Songea; Tabora na Zanzibar na vituo vya nje ya nchi ni: Bujumbura; Entebbe, Hahaya; Guangzhou; Harare; Lubumbashi; Lusaka; Mumbai; Nairobi na Ndola.

 

(iv)       Miradi ya Umeme: Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme. Sekta hii ni wezeshi katika uzalishaji viwandani, kukuza biashara na kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini. Hadi Mei 2023 uwezo wa mitambo ya kuzalisha  umeme iliyounganishwa katika Gridi ya Taifa ulifikia MW 1,872.05, sawa na ongezeko la asilimia 10.5 ikilinganishwa na MW 1,694.55 zilizokuwepo mwaka 2021/22. Aidha, hatua zilizofikiwa katika utelekezaji wa  baadhi ya miradi

ya umeme ni pamoja na: kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I Extension – MW 185 ambapo mitambo yote minne (4) yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 185 imewashwa na umeme huo kuingizwa katika Gridi ya Taifa; na kufikia asilimia 99 ya utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa maji Rusumo (MW 80). Kwa upande wa miradi ya ujenzi wa njia za kusafirisha na kusambaza umeme, Serikali imeunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kutokea kituo cha Nyakanazi na imeunganisha Wilaya za Ngara na Biharamulo kwenye kituo cha gridi ya Taifa cha Nyakanazi. Aidha, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze umefikia asilimia 93.5 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze umefikia asilimia 64. Vile vile, hadi Mei, 2023 jumla ya vijiji 10,127 kati ya vijiji 12,318 vya Tanzania Bara sawa na asilimia

82.21 vimeunganishwa na huduma ya umeme.

 

(v)         Ujenzi na Ukarabati wa Viwanja vya Ndege: Kukamilika kwa upanuzi wa maegesho ya ndege, uzio wa kiwanja, maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege Mwanza; kukamilika kwa upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara na Songea; Kukamilika kwa upanuzi wa njia ya kutua na kuruka ndege na kufungwa kwa mfumo wa kuongozea ndege katika kiwanja cha Ndege Dodoma; na kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja cha Ndege cha Geita. Shughuli zinazoendelea ni pamoja na: ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato Awamu ya Kwanza inayohusisha ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na jengo la abiria ambapo utekelezaji umefikia asilimia 18; Kiwanja cha Ndege Iringa (asilimia 50), Songwe (asilimia 98) na Musoma (asilimia 47). Aidha, kazi nyingine zilizofanyika ni kuanza maaandalizi ya ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga.

 

(vi)       Uendelezaji wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: kuendelea na zoezi la uchimbaji na upanuzi wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli hadi kufikia kina cha mita 15.5 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 96. Bandari ya Tanga: kuendelea na uboreshaji wa Bandari katika awamu ya pili ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 99. Bandari za Maziwa Makuu: Ziwa Victoria: Kuendelea na maandalizi ya awali ya ujenzi wa Bandari za Bukoba na Kemondo Bay; na kuendelea na hatua za mwisho za kufanya usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mwanza North ikijumuisha miundombinu ya Reli (SGR). Ziwa Tanganyika: kukamilika kwa ujenzi wa Gati katika Bandari mpya ya Karema; na kuendelea na usanifu wa ujenzi wa jengo la abiria (Passenger Lounge) na ukuta wa mizigo wa Lighter Quay katika Bandari ya Kibirizi na gati la Bandari ya Ujiji ambapo utekelezaji umefikia asilimia 69. Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa sakafu ngumu katika bandari ya Kiwira na Itungi; kuendelea na ujenzi wa sehemu ya kuegesha meli (ramp) katika bandari ya Kiwira; na kukamilika kwa ujenzi wa sehemu ya kuegesha meli katika bandari ya Ndumbi.

 

 

(vii) Kuboresha Huduma za Usafiri na Usafirishaji wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu

Kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambapo utekelezaji umefikia asilimia 83; kuendelea na ukarabati wa meli ya MV Umoja na MT Sangara ambapo utekelezaji umefikia asilimia 75.8 na 90.7 mtawalia; kukamilisha taratibu za kupata Mkandarasi wa ujenzi wa meli mpya tatu (3) pamoja na chelezo ambapo meli mbili (2) zitajengwa katika Ziwa Tanganyika, meli moja (1) Ziwa Victoria na Chelezo Ziwa Tanganyika.

 

(viii)    Barabara na Madaraja Makubwa: Kuendelea kuboresha mtandao wa barabara nchini kwa kujenga barabara za mikoa na barabara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na barabara za mijini na vijijini. Miradi ya barabara iliyokamilika ni pamoja na: ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege sehemu za Lusitu – Mawengi (km 50); Moronga – Makete (km 53.5); na Kisorya - Bulamba (km 51). Aidha, ujenzi wa madaraja ya Tanzanite (Dar es Salaam), Wami (Pwani), Kiyegeya (Morogoro) na Kitengule (Kagera) umekamilika. Vile vile, ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa km 3.2 unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 72. 

 

Kwa upande wa barabara za vijijini na mijini zinazosimamiwa na TARURA, jumla ya kilometa 163.83 za lami, kilometa 4,724.15 za changarawe madaraja 75 na makalvati 95 yamejengwa. Aidha, barabara zenye urefu wa kilometa 14,826.35 zimefanyiwa matengenezo.

(ix)       Huduma za Afya: Serikali imeendelea kuboresha huduma za kibingwa nchini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wake ambapo jumla ya wagonjwa 25 wamepatiwa huduma ya upandikizaji wa uroto katika hospitali za Muhimbili na Benjamin Mkapa. Upatikanaji wa huduma hii hapa nchini umepunguza gharama za kupata huduma nje ya nchi kutoka shilingi milioni 250 hadi kufikia milioni

70 sawa na punguzo la asilimia 72 ya gharama zilizohitajika; kuanza kutoa huduma za kibingwa ya kibobezi ya kupunguza uzito kwa kuweka puto

(Intragastric ballon) katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila ambapo jumla ya wagonjwa 87 wamepatiwa huduma hiyo; na  kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha upandikizaji viungo na ukarabati wa wodi za watoto mahututi (NICU) katika hospitali ya Muhimbili – Mloganzila.  

 

Kwa upande wa hospitali za rufaa za kanda mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa majengo ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Bugando; kuendelea na ujenzi wa jengo la huduma za tiba - mionzi kwa magonjwa ya saratani katika hospitali ya KCMC; na kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU), jengo la huduma za dharura (EMD), chumba cha tiba mtandao, katika hospitali ya rufaa Mbeya.  

 

Kwa upande wa hospitali za rufaa za mikoa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya OPD, afya ya uzazi, EMD, ICU, upasuaji, mifupa, wodi, sehemu ya kufulia, damu salama na kichomea taka katika hospitali ya Njombe; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za afya ya uzazi na kuendelea na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (asilimia 94) katika hospitali ya Simiyu; na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la afya ya uzazi na kuendelea na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi katika hospitali ya Geita ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98. 

 

Aidha, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kufikia ngazi za chini ambapo inaendelea na: ujenzi wa hospitali 59 na ukarabati wa hospitali kongwe 19 za Halmashauri; ukamilishaji wa zahanati 300 katika halmashauri 184; na ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya 150, zahanati 300, na hospitali za Halmashauri

71.

 

Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za bima za afya, idadi ya watanzania wanaopata huduma za bima ya afya imeongezeka kutoka asilimia 21.2 mwaka 2019/20 hadi asilimia 30.6 mwaka 2021/22.

 

(x)         Elimu: Kuendelea na utekelezaji wa programu ya Elimumsingi na Sekondari Bila Ada ambapo jumla ya shilingi 295.3 zimetolewa; kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 652.1 kwa wanafunzi 202,877 wa elimu ya juu; kukamilika kwa ujenzi wa madarasa 8,000 ya shule za sekondari katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara; kuendelea na ukamilishaji wa madarasa 1,072 ya shule kongwe za msingi; kuendelea na ukamilishaji wa maboma 809 ya madarasa ya shule za msingi; kuendelea na ukamilishaji wa vyumba  271 vya maabara za Sayansi katika Shule za sekondari; na kuendelea na ukarabati na ujenzi wa vyuo 14 vya maendeleo ya wananchi (FDCs) na vyuo vikuu.

 

(xi)       Maji Mijini na Vijijini: Hali ya upatikanaji wa maji nchini inaendelea kuimarika ambapo kwa upande wa vijijini wastani wa upatikanaji wa maji umefikia asilimia 77.0 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 70.1 mwaka 2020. Aidha, kwa upande wa mijini hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi imeongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2020 hadi asilimia 88.0 mwaka 2022. Vile vile, jumla ya miradi 586 yenye vituo 5,748 vya kuchotea maji vinavyonufaisha wananchi wapatao 4,086,442 kwenye vijiji 1,293 imekamilika. Kadhalika, uchimbaji wa visima vitano (5) katika jiji la Dodoma, ujenzi wa choteo jipya katika mradi wa maji na usafi wa mazingira mji wa Kigoma, awamu ya kwanza ya mradi wa uboreshaji maji katika miji ya Tinde na Shelui, ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni 15 katika eneo la Kisarawe II na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji katika eneo la Kimbiji umekamilika. Ujenzi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira Arusha unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 92.67; Mugango – Kiabakari - Butiama (asilimia 79); na mradi wa majisafi na usafi wa mazingira katika mji wa Lindi (asilimia 71). 

 

(xii) Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Kilimo: kuzalishwa na kusambazwa kwa tani 1,004 za mbegu bora za ruzuku za Alizeti kwa wakulima katika wilaya 39 za mikoa ya Dodoma, Kagera, Mbeya, Mwanza na Singida; kuzalishwa na kusambazwa kwa tani 80 za mbegu bora za ruzuku za ngano katika halmashauri ya wilaya ya Makete; kutolewa na kusambazwa kwa tani 449,795 za mbolea ya ruzuku kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini; kubainisha mashamba makubwa (Block farms) yenye ukubwa wa ekari 264,841.50 kwa ajili ya vijana katika mikoa ya Kigoma (ekari 36,719.75) Mbeya (ekari 52,165), Njombe (ekari 87,000), Dodoma (ekari 33,4543), Singida (ekari 50,000) na Kagera (ekari 5,503.75); kununuliwa kwa viuatilifu lita 106,000 za kudhibiti visumbufu vya milipuko ya viwavijeshi na  lita 82,124 zimesambazwa katika Halmashauri 58 za Mikoa ya Manyara, Singida, Tabora, Katavi, Tanga, Geita, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma; kukamilika kwa ujenzi wa vihenge 20 na maghala manne (4) katika Wilaya za Babati, Mpanda na Sumbawanga; kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula - NFRA kununua mahindi tani 17,257.857 na mtama tani 1,036.457 na Bodi ya Mazao Mchanganyiko – CPB  kununua mahindi tani 34,484, alizeti tani 2,776, mafuta ghafi tani 85.82, mchele tani 1,797, ngano tani 277, maharage tani 406, mtama tani 3,035.06, maharage ya soya tani 393, maharage ya njano tani 30, korosho ghafi tani 523, na mpunga tani 7,065; kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha TANECU (Newala) cha kubangua korosho chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 za korosho kwa mwaka; na kuendelea na ujenzi wa skimu mpya za umwagiliaji 19 kati ya 25 zenye ukubwa wa hekta 45,564. 

Mifugo: Kukamilika kwa ujenzi wa majosho 97 na kuendelea na ujenzi wa majosho 160 kwenye mamlaka 83 za serikali za mitaa; kununuliwa kwa lita 52,560 za dawa ya kuogesha mifugo kwa ajili ya majosho 2,644 na kusambazwa kwenye mashamba ya Wizara na Taasisi zake; kuwezesha upatikanaji na usambazaji wa chanjo za mifugo dozi 679,827,610 za magonjwa mbalimbali ya kipaumbele; kununuliwa kwa mitamba 1,160 na kununuliwa kwa matrekta 3, Bailer 5, mower 5 na Hay rake 5 na kusambazwa katika mashamba ya serikali; kuhimilisha ng’ombe 60,697 kupitia kambi za uhimilishaji; kuzalishwa kwa jumla ya dozi 116,558 za mbegu za mifugo katika kituo cha NAIC kwa ajili ya uhimilishaji; kununuliwa kwa magari 13 yakiwemo Toyota Hard Top (2) na Toyota Double Cabin (11) na pikipiki 1200 kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za ugani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184; kujengwa kwa minada 19 na kukarabati minada minne (4) katika maeneo mbalilmbali nchini; kuendelea na ujenzi wa mabwawa 11 katika maeneo mbalimbali nchini; kununuliwa kwa tani 8.56 za mbegu za malisho na vipando vya miti malisho 18,025 kutoka mashamba ya Serikali na binafsi na kusambazwa kwa wafugaji; na kuanzishwa kwa vituo nane (8) vya uwekezaji vya vijana vyenye uwezo wa kuchukua jumla ya vijana 240 kwa mwaka kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata uzoefu katika kuanzisha na kuendesha miradi ya ufugaji kibiashara, ambapo jumla ya vijana 238 wamesajiliwa katika vituo Atamizi vya LITA na TALIRI.

 

Uvuvi: Kuendelea na ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko – Lindi ambapo usanifu wa kina umekamilika na kuanza uchimbaji; kuendelea na taratibu za  ununuzi wa meli mbili (2) za uvuvi wa Bahari Kuu zenye vifaa vya kisasa; kukamilika kwa ujenzi wa Maabara ya Utafiti wa Uvuvi katika kituo cha TAFIRI - Dar es Salaam; kukamilika kwa ukarabati wa mabwawa makubwa matatu (3) na madogo sita (6) katika Kituo cha Rubambagwe (Geita); kuendelea na ujenzi wa mashamba darasa sita (6) ya ufugaji wa samaki katika Halmashauri za wilaya za Kongwa, Iringa, Njombe, Songea, Tandahimba  na Ruangwa; kukamilika kwa taratibu za ununuzi wa boti za uvuvi 158 ikiwa ni awamu ya kwanza kwa ajili ya kukopesha wavuvi; kuvunwa kwa tani 426,555.46 za samaki zenye thamani ya Shilingi trilioni 2.86; kuuzwa nje ya nchi  kwa jumla ya tani 29,466.98 za mazao ya uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni 453.8 na idadi ya samaki hai wa mapambo 150,308 wenye thamani ya shilingi bilioni 1.82; na kuendelea na tafiti mbalimbali za kujua uwingi, aina, bioanuwai na mtawanyiko wa samaki kwenye Maziwa, Bahari na Mabwawa.

 

(xiii)    Madini: Kusainiwa kwa mikataba ya uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini muhimu na madini mkakati na kampuni tatu (3) kutoka Australia yenye thamani ya dola za Marekani milioni 667; ununuzi wa mawe mawili (2) makubwa ya madini ya Tanzanite yenye jumla ya uzito wa kilo 5.22 kutoka kwa mchimbaji mdogo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.24; kununuliwa na kusimikwa

(commissioning) kwa vifaa vya utafiti wa jiosayansi na

vifaa vya maabara na uchunguzi; ununuzi wa mitambo mitano (5) ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo; ununuzi wa mitambo miwili (2) ya uzalishaji wa mkaa mbadala na utengenezaji wa mkaa unaotokana na makaa ya mawe;   na kuendelea na ujenzi wa jengo la kuhifadhia sampuli za miamba choronge (core shade) eneo la Kizota - Dodoma ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 75. 

 

(xiv)   Habari, Mawasiliano na TEHAMA: Kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi mpya wa Kilomita  1,600 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vituo 15 vya kutoleo huduma za Mkongo; kuendelea na ujenzi wa njia mpya za mkongo wa Taifa wa mawasiliano wenye jumla ya kilomita 4,442; kukamilika kwa uboreshaji wa programu ya Mfumo wa Kidijitali wa Anwani za Makazi; na  kukamilika kwa uhakiki wa taarifa za miundombinu ya Anwani za Makazi pamoja na taarifa za makazi zilizokusanywa katika Operesheni Anwani za Makazi kwenye Halmashauri 23.   

 

Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kuongeza upanuzi na usikivu wa shirika la utangazaji TBC ambapo shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na: kukamilika kwa taratibu za ununuzi za kuwapata wazabuni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa usikivu redio zinazomilikiwa na TBC katika maeneo tisa (9); na kuendelea na ujenzi wa makao makuu ya TBC Jijini Dodoma.

 

(xv)     Maliasili na Utalii: Kuimarisha miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi na kutangaza vivutio vya utalii kupitia programu maalum ya Tanzania - the Royal Tour imewezesha kuwepo kwa ongezeko la idadi ya watalii wa ndani na kimataifa waliotembelea maeneo ya hifadhi na Makumbusho ya Taifa kutoka watalii 1,711,625 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 3,818,180 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 123. Katika ongezeko hilo idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,454,920 mwaka 2022 sawa na asilimia 57.7 na watalii wa ndani wameongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022 sawa na asilimia 199.5. Aidha, mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,310 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 2,527.72 kwa mwaka 2022 sawa na asilimia 93. Vile vile, Serikali imeimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za maliasili kwa kudhibiti ujangili, biashara haramu ya nyara na uvunaji haramu wa mazao ya misitu.

 

(xvi)   Uwekezaji, Viwanda na Biashara: Serikali imeendelea na juhudi mbalimbali za kuhamasisha na kuvutia uwekezaji nchini kwa kufanya mapitio ya Sera mbalimbali ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya Mwaka 2022, kuendelea na uwekaji wa miundombinu wezeshi katika maeneo maalumu ya uwekezaji na kushiriki makongamano mbalimbali ya uwekezaji yanayofanyika ndani na nje ya nchi. Kutokana na juhudi hizo baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na usajili wa jumla ya miradi mipya 240 (Wazawa 89, wageni 94 na ubia 57) katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023 ikilinganishwa na miradi 206 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2021/22. Miradi hii inatarajiwa kuwekeza jumla ya Dola za Marekani milioni 4,387.17 na kuzalisha ajira 39,245.  

 

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni: Kusajiliwa kwa miradi mitano (5) katika vituo vya mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 15.6 inayotarajiwa kuchangia mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 12.6 na kuzalisha ajira 1,247; na kukamilika kwa usimikaji wa Mfumo wa Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa Wawekezaji kwa Njia ya Kielektroniki (Tanzania Electronic Investment Single Window - TeIW) awamu ya kwanza pamoja na kuunganisha taasisi saba (7). 

 

(xvii)  Utawala Bora na Utawala wa Sheria: katika kuhakikisha kuwa utawala bora na utawala wa sheria unaendelea kushamiri nchini, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo na miundombinu ya Kitaasisi na utoaji haki, uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma.  Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: Kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni; kuendelea na ujenzi wa  Mahakama za wilaya za Liwale ambapo utekelezaji umefikia asilimia 70, Kwimba (asilimia 80), na Ulanga (asilimia 35); kuendelea na ujenzi wa Mahakama za

Mwanzo tisa (9) ambapo Mahakama ya Mwanzo Madale

(Dar es Salaam) utekelezaji umefikia asilimia 75, Kinesi -

Rorya (asilimia 99), Mahenge - Kilolo (asilimia 97), Luilo – Ludewa (asilimia 80), Newala – Newala (asilimia 75), Usevya – Mlele (asilimia 95), Nyakibimbili -  Bukoba (asilimia 90);  Kabanga – Ngara (asilimia 80) na Mlimba na Mang’ula – Morogoro (asilimia 85); kukamilika kwa ukarabati wa jengo la Mahakama Kuu Tabora na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi; na kuendelea na Awamu ya Pili ya ujenzi wa majengo ya Wizara katika mji wa Serikali Mtumba ambapo ujenzi wa majengo 24 umefikia wastani wa asilimia 60 na ujenzi wa jengo moja (1) la Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) umefikia asilimia 50 kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

 

(xviii)             Utamaduni, Sanaa na Michezo: Kutolewa mikopo kwa awamu mbili (2) yenye thamani ya shilingi bilioni 1.07 kwa wasanii na wadau 45 katika tasnia za utamaduni na sanaa. Aidha, Serikali imeratibu matamasha mbalimbali yenye lengo la kudumisha urithi wa utamaduni ikiwemo: Tamasha kubwa la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika Julai, 2022 Jijini Dar es Salaam; Tamasha la tano (5) la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki, (JAMAFEST) lililofanyika Septemba, 2022 Jijini Bujumbura - Burundi; Tamasha la 41 la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa la Bagamoyo; na Tamasha la Msimu wa Utamaduni kati ya Tanzania na Afrika Kusini  mwezi Novemba, 2022; na kuandaa na kuendesha mashindano ya Kimataifa ya Urembo na Utanashati kwa viziwi (Miss and Mr. Deaf International – MMDI, 2022) ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika Barani Afrika.

 

Aidha, timu ya mpira wa miguu ya watu wenye ulemavu (Tembo Worriors) ilifanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya kombe la dunia kwa watu wenye ulemavu na kuiweka nchi kwenye orodha ya timu kumi bora za dunia; na Timu ya Taifa ya Wanawake (Serengeti Girls) kushiriki fainali za kombe la dunia nchini India na kufikia hatua ya robo fainali mwezi Oktoba, 2022. 

 

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na: Nchi kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mwaka 2022 uliofanyika Jijini Arusha na Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Michezo wa Baraza la Michezo la Afrika Kanda ya IV uliofanyika Jijini Arusha ambapo Tanzania ilichaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza hilo; na Tanzania kuwasilisha zabuni ya kuomba kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika – AFCON 2027 kwa ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda. 

 

Aidha, kwa namna ya kipekee kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuleta hamasa kwa timu zetu katika michezo ya Kimataifa kwa kununua kila goli linalofungwa na timu zetu zinapokuwa katika mashindano ya Kimataifa ambapo kutokana na juhudi hizo timu ya Simba imepata shilingi milioni 55 na Yanga shilingi milioni 135. YANGA HOYEE!!. Vile vile, napenda kutoa pongezi kwa klabu ya Simba kwa kuendelea kufanya vizuri kimataifa na kufikia hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika. Aidha, kwa kipekee kabisa napenda kuipongeza timu ya Yanga kwa kufika fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika pamoja na kutoa Mfungaji Bora (Mayele) na Kipa Bora (Diara). HAKIKA TIMU YA SIMBA MNA MENGI YA KUJIFUNZA KUTOKA TIMU YA YANGA

 

26.      Mheshimiwa Spikamaelezo ya kina kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Mpango yanapatikana katika Kitabu cha Mpango, Sura ya Pili.

 

27.      Mheshimiwa Spika, itakumbukwa mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa 2050 ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango tarehe 03 Aprili, 2023 Dodoma. Aidha, Serikali imepanga kuyafikia makundi yote ya wadau katika zoezi la ukusanyaji wa maoni ili kuhakikisha Dira inakuwa na maono jumuishi. Nitumie fursa hii, kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, maandalizi ya Dira 2050 yanahusisha tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025, ambapo matokeo ya tathmini hiyo yataweka msingi wa maandalizi ya Dira 2050. Hivyo, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa maandalizi ya Dira Bora kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo yanategemea ushiriki mkubwa na maoni ya Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote (ikijumuisha wale waishio nje kwa maana ya Diaspora) na Washirika wetu wa Maendeleo. Hivyo, usisite kutoa maoni yako pale utapohitajika kufanya hivyo.    

 

 

 

 

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2023/24

28.      Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 ni wa tatu katika utekelezaji wa Mpango wa

Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Mpango umeandaliwa kwa kuzingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26; Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24; na Sera na Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050, Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050, Agenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika na Malengo ya Maendeleo Endelevu

2030.

 

29.      Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2023/24, msisitizo mkubwa utawekwa katika sekta za uzalishaji na zinazozalisha ajira zinazowagusa wananchi wengi ambazo ni kilimo, mifugo, na uvuvi. Aidha, Mpango huu unalenga kukamilisha miradi mingi ambayo ilianza katika utekelezaji wa mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano (2021/22-2025/26), ambao ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira 2025. Vile vile, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2023/24 unatarajia kuleta matokeo chanya ikiwemo: kuimarika kwa ukuaji wa Pato la Taifa; kuimarika kwa miundombinu ya huduma za kiuchumi na kijamii hususan afya, elimu, maji na umeme; kudhibitiwa kwa kasi ya mfumuko wa bei; kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji na biashara; kuvutia ushiriki wa sekta binafsi; na kuimarika kwa maisha na ustawi wa jamii.

 

Malengo na Shabaha za Uchumi Jumla kwa Mwaka 2023/24

 

30.      Mheshimiwa Spika, malengo na shabaha za ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2023/24, ni kama ifuatavyo:

(i)       Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.2 mwaka 2023 kutoka ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka

2022; 

(ii)    Mfumuko wa bei kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa  asilimia 3.0 hadi asilimia 7.0 katika kipindi cha muda wa kati; 

(iii)  Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 kutoka matarajio ya asilimia 14.4 mwaka 2022/23

(iv)  Mapato ya kodi kufikia asilimia 12.0 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 kutoka matarajio ya asilimia 11.5

mwaka 2022/23; 

(v)    Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa chini ya asilimia 3.0 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24; na 

(vi)  Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).

 

31.      Mheshimiwa Spika, misingi itakayozingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 ni kama ifuatavyo: 

(i)       Kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara;

(ii)    Kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili; 

(iii)  Kuendelea kuhimili athari zitokanazo na kushuka kwa uchumi wa dunia na kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma katika soko la dunia;

(iv)  Kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa chakula nchini;

(v)    Uwepo wa amani, usalama, umoja na utulivu wa ndani na nchi jirani; na

(vi)  Kuendelea kuimarika kwa viashiria vya ustawi wa jamii.

 

Miradi ya Kipaumbele kwa Mwaka 2023/24

 

32.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24, Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo. Miradi hiyo inajumuisha: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway - SGR); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Kufua Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222) – Njombe; Daraja la JPM - Kigongo – Busisi (Mwanza); Ujenzi wa barabara na Madaraja Makubwa; kuendeleza Kanda Maalumu za Kiuchumi ikiwemo Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo; na Programu ya Kuendeleza Ujuzi Adimu.

 

33.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023/24 Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia maeneo matano (5) ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2021/22 – 2025/26 kama ifuatavyo:

 

(a)         Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: Katika eneo hili nguvu kubwa itaelekezwa kwenye miradi inayolenga kuboresha miundombinu, kuimarisha mifumo ya kitaasisi pamoja na miradi inayolenga kuleta mapinduzi ya TEHAMA. Utekelezaji wa miradi hiyo utaimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza utulivu wa kiuchumi. Miradi hiyo ni pamoja na:

(i)          Barabara: miradi itakayotekelezwa ni ile inayolenga kufungua fursa za kiuchumi, za kuunganisha Tanzania na nchi jirani pamoja na za kupunguza msongamano ikiwemo: Barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupilo - Malinyi – Londo – Lumecha/Songea (km 499); Barabara ya Ifakara - Kihansi - Mlimba - Madeke – Kibena (km 220); na Barabara ya Makutano – Natta – Mugumu/Loliondo – Mto wa Mbu (km

235); Handeni – Kibaya – Singida (Km 460). 

(ii)        Madaraja Makubwa: kuanza ukarabati wa daraja la Kirumi (Mara); kuendelea na ujenzi wa barabara unganishi za Daraja la Sibiti (Singida); na kuanza ujenzi wa Madaraja ya Chakwale (Morogoro), Nguyami (Morogoro) na Mbambe (Pwani).

(iii)      Usafiri wa Majini: Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu ikijumuisha: Kukamilisha ujenzi wa meli mpya ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu; kukamilisha ukarabati wa meli za MV Umoja na MT. Sangara; kuanza ujenzi wa meli mpya (Wagon ferry) katika Ziwa Victoria na meli mpya (Barge/Cargo

ship) ya kubeba shehena ya mizigo katika Ziwa Tanganyika

(iv)      Bandari: Bandari ya Dar es Salaam, kuendelea uchimbaji wa kina na upanuzi wa lango la kuingilia na kugeuzia meli na uboreshaji wa Gati Na. 8 – 11 na kuendelea na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa gati Na. 12 -15; Bandari ya Tanga, kuendelea na uboreshaji wa Bandari ya Tanga na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya gati la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga); Bandari ya Mtwara, kuendelea na maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena za mizigo; Bandari ya Bagamoyo, kuanza maandalizi ya utekelezaji wa bandari; kuendelea na uboreshaji  wa  Bandari za Bukoba,  Kemondo Bay na Mwanza North katika Ziwa Victoria; Kuendelea na ujenzi wa Access Road, Cargo Shed, Passenger Wharf and Lounge) pamoja na kuendelea na ujenzi wa Passenger Lounge na ukuta wa mizigo wa  Lighter Quay katika Bandari ya Kibirizi na gati la Bandari ya  Ujiji katika Ziwa Tanganyika.

(v)        Usafiri wa Anga: Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Msalato, Mwanza, Mtwara, Kigoma, Sumbawanga, Shinyanga, Songwe, Mpanda, Tabora, Bukoba, Geita, Iringa, Ruvuma (Songea), Simiyu, Lake Manyara, Tanga, Moshi, Lindi na Mara (Musoma), Dodoma, Manyara na Arusha.

(vi)      Nishati: Kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kufua, kusafirisha na kusambaza umeme (nishati) ikiwemo: Kufua Umeme wa Maji Kikonge (MW 300); Kufua Umeme wa Maji Malagarasi (MW 49.5); Uimarishaji wa Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization); Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi; na Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 – North – West Grid Extension (Iringa – Mbeya – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi).

(vii)    Mapinduzi ya TEHAMA: Kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya Anwani za Makazi na Tanzania ya Kidijitali; kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji wa Vifaa vya TEHAMA; na ujenzi wa Kituo Kikuu na Vituo vidogo vya  Kuendeleza Ubunifu katika TEHAMA.

 

(b)        Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Huduma: miradi itajielekeza katika kukuza sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi. Miradi hiyo ni pamoja na: programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili; mradi wa kuimarisha miundombinu ya masoko ya mifugo na mazao yake; kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga skimu mpya 25 na kukarabati skimu 30 zenye jumla ya hekta 95,005 katika mikoa mbalimbali; na kuimarisha huduma za ugani. Aidha, msukumo wa pekee utawekwa katika kuboresha Viwanda Vidogo – SIDO na Kiwanda cha Mashine na Vipuri KMTC; kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi (SEZ) na kongani za viwanda. 

(c)          Kukuza Biashara na Uwekezaji: Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za maendeleo. Kipaumbele kitakuwa katika kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Blueprint); kuboresha huduma za biashara na masoko; kuratibu programu za kuimarisha mifumo ya udhibiti wa uwekezaji inayolenga katika kupunguza gharama za uwekezaji nchini; na kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma zitolewazo kwa wawekezaji katika Kituo cha Huduma za Mahali Pamoja.

 

(d)        Kuchochea Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa imelenga kuboresha maisha ya watu pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii. Miradi hiyo ni pamoja na: miradi ya afya kwa kuimarisha huduma za afya katika  hospitali za kitaifa, hospitali za rufaa za kanda na  mikoa; hospitali za halmashauri; vituo vya afya na zahanati; kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; kugharamia elimumsingi na sekondari bila ada; utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; kuendelea na  ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya mikoa na wilaya, miji midogo na vijijini; na kuendelea kupanga, kupima na kumilikisha ardhi pamoja na kuimarisha mipaka ya kimataifa.

 

(e)         Kuendeleza Rasilimali Watu: Kuendelea na utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya kukuza ujuzi nchini ili kuongeza ajira kwa vijana kwa kutoa mafunzo ya ufundi na stadi za kazi kupitia programu mbalimbali zikiwemo:  kuimarisha programu ya Taifa ya kukuza ujuzi nchini; kuboresha mfuko wa maendeleo ya vijana; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa vituo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu; na kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Kazi za Staha.

 

34.      Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, sekta ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ilipewa jukumu la kugharamia shilingi trilioni 21 sawa na asilimia 17 ya Bajeti ya kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. Katika kutekeleza jukumu hilo la kimkakati, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na wadau wengine imeweza kubainisha jumla ya miradi 48 inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP. 

 

35.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24 miradi mikubwa ambayo ipo kwenye maandalizi ya kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP ni pamoja na:  kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua katika mikoa ya Dodoma (Zuzu MW 60) Kilimanjaro (Same MW 50) na Singida (Manyoni MW 100); Mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji wa Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222); mradi wa miundombinu ya kusambaza gesi katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara ;na mradi wa kusafirisha umeme wa Tanzania – Malawi – (TAMA) interconnection wenye urefu wa km 82. 

 

36.      Mheshimiwa Spika, Miradi mingine ni: Reli ya Dar es Salaam (Dar -Commuter Rail); Reli ya Mtwara-Bamba Bay; Uendeshaji wa Reli (Rolling stocks); Uendeshaji wa Barabara ya haraka (expressway) kutoka Igawa-Tunduma; Barabara za kupunguza msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Inner and Outer Ring Roads); Barabara za haraka kutoka KibahaChalinze-Morogoro hadi Dodoma na kuunganisha Jiji la Dodoma na Dar es Salaam kwa barabara za haraka; Bandari kavu katika eneo la Kisiwa/Mgao – Mtwara; na Kuboresha na Upanuzi wa bandari katika Ziwa Victoria - Mwanza na Nansio - Ukerewe.

 

37.      Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Umuhimu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Serikali inaendelea na hatua za mwisho za utekelezaji wa takwa la kisheria la kuanzisha Kituo cha Ubia (PPP-Center) kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa jukumu hili kubwa na la kimkakati. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2023/24, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.82 kwa ajili ya maandalizi ya miradi ya Ubia (PPP Faciliatation Fund-PPPFF) ili kuwezesha maandalizi ya maandiko ya miradi ya maendeleo yenye mvuto wa uwekezaji wa sekta binafsi nchini. Vile vile, Serikali imejipanga kukabili changamoto za kisheria, kimfumo na kiutendaji zilizochangia kuchelewa kwa  miradi ya ubia kwa zaidi ya muongo mmoja. Katika kuhakikisha hilo, Serikali iliwasilisha muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta Umma na Binafsi, Sura Na 103 ambapo tarehe 13 Juni, 2023 Bunge lako Tukufu liliuridhia na kuupitisha. Hivyo, ni rai yangu kwa Mawaziri wenzangu na watendaji wa Serikali kutumia fursa hiyo kushirikiana na Sekta Binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

 

38.      Mheshimiwa Spikamaelezo ya kina kuhusu miradi ya kipaumbele kwa mwaka 2023/24 yanapatikana katika Kitabu cha Mpango, Sura ya Tatu.

Vihatarishi vya Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2023/24 na Mikakati ya Kukabiliana Navyo

 

39.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango unaweza kuathiriwa na  vihatarishi vya ndani na nje. Vihatarishi hivyo ni pamoja na: mabadiliko ya viwango vya riba za mikopo katika soko la ndani na nje; uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za binadamu; migogoro na hali ya siasa inayojitokeza kwa nchi jirani, kikanda na kimataifa; na kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

 

40.      Mheshimiwa Spika, katika kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na vihatarishi husika, Serikali inalenga kuchukua hatua mbalimbali ikijumuisha: kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ili kupunguza utegemezi katika misaada na mikopo kutoka nje; kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira ili kudhibiti uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu; kuimarisha mikakati ya kisera ili kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi duniani; na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.

 

Ugharamiaji wa Mpango 2023/24

 

41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24 Serikali imetenga shilingi bilioni 14,077.2 kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 10,795.1 sawa na asilimia 77.0 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za ndani na shilingi bilioni 3,282.1 sawa na asilimia 23 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za nje. Fedha hizi zitakusanywa kutoka katika mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, misaada na mikopo nafuu, mikopo ya ndani na mikopo ya nje yenye masharti ya biashara. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia ushiriki wa sekta binafsi.

 

Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango 2023/24

 

42.      Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, suala la ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji limeendelea kupewa msukumo wa pekee katika shughuli za kila siku za Serikali. Katika kutekeleza hilo, mwaka 2022/23, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi 211 kati ya lengo la miradi 300 iliyopangwa kufuatiliwa katika kipindi cha mwaka 2022/23. Aidha, miradi iliyofuatiliwa ilihusisha miradi kutoka sekta za ujenzi, uchukuzi, viwanda, elimu, afya, utawala bora, kilimo, mifugo, maji na biashara inayotekelezwa na serikali pamoja na sekta binafsi.

 

43.      Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha uratibu na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 kupitia Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo wa Mwaka 2022; Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26; Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/24; Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma wa Mwaka 2022; Sheria ya Bajeti, Sura 439; Mpango Kazi na Mtiririko wa Mahitaji ya Fedha; Waraka Na. 5 wa Hazina wa Mwaka 2020/21 Kuhusu Matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo (NPMIS); na Waraka Na. 1 wa Hazina kuhusu

Utekelezaji wa Bajeti. 

 

44.      Mheshimiwa Spika, Pamoja na Sheria hizo na miongozo hiyo, Serikali pia inaendelea na maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ambapo hatua iliyofikiwa ni kukamilika ukusanyaji na uchambuzi wa maoni kutoka kwa wadau na kuanza kwa uandishi wa Taarifa ya Kizio (Baseline Report). Kukamilisha kwa uandishi wa Taarifa Kizio kutajenga msingi wa uandishi wa Sera ambayo inatarajiwa kutatua changamoto za uratibu wa shughuli za ufuatiliaji na tathmini chini. Aidha, shughuli ya ufuatiliaji na tathmini ni suala mtambuka na inahusisha wadau mbalimbali katika ngazi tofauti, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushirikiana na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na sekta binafsi katika kuratibu na kusimamia ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.

 

45.      Mheshimiwa Spika, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaelekezwa kuzingatia maelekezo yaliyoainishwa katika Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya  Miradi na Programu za Maendeleo wa Mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na: kuandaa Mpango Kazi wa mwaka wa ufuatiliaji na tathmini; kutenga rasilimali fedha zitakazowezesha shughuli za ufuatiliaji na tathmini; kuimarisha mifumo ya ndani ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mipango kazi iliyowekwa; na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi katika tasnia ya ufuatiliaji na tathmini. 

 

46.      Mheshimiwa Spika, Serikali inazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuaandaa taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo na kuziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa husika Wizara ya Fedha na Mipango.

 

MAJUMUISHO

 

47.      Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 ni wa tatu katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Utekelezaji wa Mpango utaendelea kuimarisha mahusiano ya kisiasa, ulinzi na diplomasia ya uchumi na nchi nyingine, kuendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya maendeleo, kuchochea uwekezaji viwandani hususan kwa kutumia rasilimali watu na malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini ikiwemo mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, madini, misitu na gesi asilia, kuimarisha viashiria vya uchumi jumla, kuboresha mazingira ya uwekezaji viwandani ikiwemo kuimarisha majadiliano na wawekezaji wa ndani na nje pamoja na kuendeleza mashirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

48.      Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji ili kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi, kufungua fursa zaidi za ajira na maendeleo ya watu, kuboresha upatikanaji na utoaji wa  huduma bora kwa wananchi zikiwemo huduma za afya, elimu, umeme na maji safi na salama mijini na vijijini pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi ya uwekezaji na biashara kwa ajili ya masoko ya kimataifa hususan ya nchi jirani.

 

49.      Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kukabiliana na athari za majanga mbalimbali ya asili na yasiyo ya asili yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, magonjwa na vita. Aidha, tutaendelea kuimarisha utekelezaji kwa kuweka mipango madhubuti ya kupunguza athari zitokanazo na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine ikiwemo kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa mbalimbali na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kukabiliana na Athari za UVIKO–

19.

 

 

HITIMISHO

 

50.          Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ninaomba kutumia fursa hii kuwashukuru wadau wote wa maendeleo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo,

Taasisi za Elimu na Tafiti, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Taasisi za Dini na Wananchi wote kwa namna walivyojitoa na kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha uchumi wa Taifa letu. Wadau hao wamekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Kwa msingi huo, ninawaomba na kuwasihi wadau wote waendelee kushirikiana na Serikali yetu inayoongozwa na Rais shupavu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

51.          Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa niwashukuru Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Viongozi wote wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakuu wa Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24. Aidha, hotuba hii isingeweza kukamilika bila jitihada kubwa zilizofanywa na watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango. Hivyo, kwa dhati ya nafsi yangu naomba nitoe shukrani za pekee kwa Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na watendaji  wote wa Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zilizo chini ya Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Natu El-Maamry Mwamba kwa kujitoa usiku na mchana kukamilisha kwa wakati na kwa ubora Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24.

 

52.          Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa ujumla kwa kutenga muda wao kunisikiliza. Aidha, napenda kuwataarifu wadau wote kuwa, hotuba hii pamoja na vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni www.mof.go.tz.

 

53.          Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24.

 

54.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post