VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA VYACHOCHEA VUGUVUGU LA MAENDELEO KWA WANANCHI


Deogratius Temba kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania akizungumza na baadhi ya wajumbe wa kituo cha taarifa na Maarifa cha Kijiji cha Miyuguyu kata ya Kiloleli.
Deogratius Temba kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania akizungumza na baadhi ya wajumbe wa kituo cha taarifa na Maarifa cha Kijiji cha Miyuguyu kata ya Kiloleli.
Wajumbe wa Kituo cha taarifa na maarifa cha kijiji cha Miyuguyu wakijadiliana namna ya kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia baada ya kujengewa uwezo na Mtandao wa jamii Tanzania (TGNP)
Wajumbe wa Kituo cha taarifa na maarifa cha kijiji cha Miyuguyu wakijadiliana namna ya kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia baada ya kujengewa uwezo na Mtandao wa jamii Tanzania (TGNP)
Nyumba iliyojengwa na wakazi wa kijiji cha Miyuguyu kwa ajili ya Mwalimu wa Shule ya Msingi ambaye awali alikuwa akiishi Shuleni.
Vyoo vilivyojengwa na wakazi wa kijiji cha Miyuguyu kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Miyuguyu.

***
Uwepo wa Vituo vya Taarifa na Maarifa mkoani Shinyanga vimetajwa kuwa kichocheo muhimu katika ujenzi wa Vuguvugu na mabadiliko kwenye jamii ambapo katika Kijiji cha Miyuguyu wilayani Kishapu wamefanikiwa kuhamasisha wananchi kujenga nyumba mpya ya Mwalimu na matundu 12 ya vyoo katika Shule ya Msingi Miyuguyu.

Hayo yamebainishwa katika Kikao cha Tathimini ya hali ya utendaji kazi wa kituo cha taarifa na Maarifa cha kijiji hicho, ambapo baadhi ya wajumbe wake akiwemo Agness Kwilasa katibu wa kituo hicho, amesema mafanikio hayo yamesababishwa na hamasa iliyotokana na Bunge la jamii.

Amesema kabla ya kuanzishwa kwa kituo hicho mwitikio wa jamii kushiriki shughuli za maendeleo ulikuwa mdogo lakini baada ya Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) kuwajengea uwezo kupitia Midahalo na Bunge la jamii katika kukabiliana na mila na desturi hasi zilizopitwa na wakati.

“Tuliziibua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinakikabili kijiji chetu ambapo wananchi waliazimia kujenga nyumba ya mwalimu ambaye alikuwa anaishi katika moja ya Ofisi katika Shule ya Msingi Miyuguyu kutokana na uhaba wa makazi ya walimu,”amesema Kwilasa.

Nae Hamis Mashauri Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho amesema tatizo la uhaba wa nyumba za walimu katika shule ya Msingi Miyuguyu linasababisha walimu kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ndio maana wanakijiji walihamasika na kuamua kujenga nyumba hiyo ili kuboresha mazingira bora ya kufanyia kazi.

“Shule hii ina wanafunzi 524,madarasa sita, walimu wapo sita na nyumba za walimu zipo tatu mbili zizojengwa na serikali na moja iliyojengwa na wananchi,mwalimu wa kike yupo mmoja tu na inauhaba wa walimu 11,”amesema Mashauri.

Kwa upande wake Getrude Missana Mwalimu wa shule ya Msingi Miyuguyu amesema awali kabla ya kujengewa nyumba hiyo alikuwa anaishi katika moja ya ofisi katika Shuleni hapo hali iliyokuwa inamuwia vigumu kutekeleza majukumu yake hadi alipohamia katika nyumba iliyojengwa na wakazi wa kijiji hicho.

“Tunaiomba serikali ituboreshe mazingira ya kazi ikiwemo ujenzi wa Makazi ya walimu katika vituo vya kazi ili kutimiza majukumu yetu ipasavyo,hapa mimi ni mwalimu wa kike peke yangu niliyesalia wengi wakipangiwa wanaomba uhamisho kutokana na changamoto hizi,”amesema Missana.

Edward Manyama ni diwani wa kata ya Kiloleli amesema serikali imeanza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kijiji cha Miyuguyu ikiwemo ya walimu ambapo kwa sasa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa walimu 11 na waliopo ni sita pekee.

“Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu imeahidi kuleta walimu wapya katika Shule ya Msingi Miyuguyu,niwaombe wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwao ili waweze kutimiza majumu ya kuwafundisha watoto wetu,”amesema Manyama.

Awali akizungumza wajumbe wa kituo cha taarifa na maarifa cha Kijiji cha Miyuguyu Deogratius Temba kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)amepongeza jitihada zizofanikisha kujengwa kwa nyumba ya mwalimu ambaye awali alikuwa akiishi shuleni.

“TGNP inawajengea uwezo wananchi kupitia vituo hivi ili waweze kuiziibua changamoto zinazowakabili na kuzipatia suluhisho,ujenzi wa nyumba hii na matundu ya vyoo 12 ni kielelezo kwamba Wakazi wa kijiji cha Miyuguyu wamebadilika na wameamua kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa pamoja,”amesema Temba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post