WIZARA YA AFYA YAWATAHADHARISHA WANANCHI DHIDI YA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU


Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema tatizo la ugonjwa wa shinikizo la juu la damu nchini bado ni kubwa ambapo kwa wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI)tangu ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2023 kati ya wagonjwa 619,102 waliotibiwa asilimia 66 kati yao walikuwa na shinikizo la juu la damu.

Ameeleza hayo leo Jijini hapa kwenye maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu duniani ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Mei 17 na kueleza kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa kwa kila wagonjwa 10 wanaoumwa hospitalini hapo, wagonjwa 6 wana ugonjwa wa shinikizo la damu.

Amesema katika uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha,Geita, Mtwara,Lindi, Zanzibar,Iringa na Dar Es Salaam takwimu zinaonesha watu 3 hadi 4 kati ya 10 wana shinikizo la damu la juu .

"Shinikizo la juu la damu ndio sababu kubwa ya kiharusi,shambulio la moyo,moyo kushindwa kufanya kazi,kutuna kwa kuta za mishipa ya damu ,moyo,uharibifu kwenye chujio za Figo,ganzi miguuni na mikononi,upofu na kupunguza nguvu za kiume,"amesema

Pamoja na hayo Waziri huyo wa afya amefafanua kuwa kwa takwimu za Tanzania kutoka mfumo wa ukusanyaji taarifa za afya zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya afya kwa mwaka 2017.

Amefafanua kuwa wagonjwa hao wameongezeka hadi kufikia wagonjwa 3,440,708 Kwa mwaka 2021 ambapo ongezeko hilo wako wagonjwa 905,427 Kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.4.

"Kati ya hao ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ndio ulioongoza miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambapo waliongezeka Kutoka wagonjwa 688,901 Kwa mwaka 2017,hadi kufikia wagonjwa 1,345,847 kwa mwaka sawa na ongezeko la asilimia 95.4 katika kipindi hicho;

Kwa takwimu hizo inaonyesha kwamba wagonjwa Wenye shinikizo la damu wameongezeka takribani mara mbili zaidi Kwa kipindi cha miaka mitano,"alisema Waziri Ummy 

Kutokana na hayo Waziri Ummy alisema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya afya ya mwaka 2007 ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu Kwa umahiri zaidi.

Kwa upande wake Prof. Pasco lubajo Mkurugenzi wa kinga Wizara ya afya ametumia nafasi hiyo kuhimiza wananchi kubadili mtindo wa maisha Kwa kufanya mazoezi, kuepuka tabia bwete, kupunguza ulevi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake .

Prof.Lubajo ameutaja ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kuwa unasababishwa na nguvu ya msukumo wa damu Katika mishipa kuwa kubwa kuliko kawaida Kwa muda mrefu ambapo ongezeko hilo huulazimu moyo kufanya kazi kupita kiasi.

Akieleza kipimo cha kawaida cha shinikizo la juu la damu alisema ni 100 hadi 140 milimita za zebaki upande wa kipimo Cha juu na milimita za zebaki 60 Hadi 90 upande wa kipimo cha chini.

"Kuna aina mbili za shinikizo la juu la damu ambazo ni asili na linalosababishwa na magonjwa mengine,kadiri ya asilimia 90 hadi 95 za watu wanaathiriwa na shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mengine kama Figo,kisukari,mapafu na mfumo wa homoni,"amesema

Siku ya shinikizo la juu la damu duniani huadhimishwa Kila mwaka ifikapo Mei 17 ambapo kwa Tanzania kitaifa inafanyika mkoani Manyara huku kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu ni Pima shinikizo la damu kwa usahihi,idhibiti ,ishi kwa muda mrefu .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments