WAZIRI DKT MABULA AINGIA MTAANI KUKAGUA UTEKELEZAJI MAELEKEZO YAKE

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua orodha ya wananchi waliohudumiwa katika eneo la Ndachi jijini Dodoma alipokwenda kukagua utekelezaji wa maelekezo yake ya kuzitaka idara za ardhi kwenda kuwahudumia wananchi katika maenreo yao mwishoni mwa wiki.

**************

Na Munir Shemweta, WANMN

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amefanya ukaguzi katika mtaa wa Ndachi jijini Dodoma kuangalia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa idara za ardhi nchini kuhakikisha zinawafuata wananchi angalau mara mbili kwa wiki kwa lengo la kutoa huduma za sekta ya ardhi.

Dkt Mabula alifanya ukaguzi huo mwishoni mwa wiki katika eneo hilo la Ndachi ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha huduma za sekta ya ardhi zinasogezwa karibu badala ya huduma hizo kupatikana ofisini pekee.

Mbali na juhudi hizo, kwa sasa Wizara ya Ardhi inabadilisha mifumo yake kutoka analogia kwenda digitali ambapo moja ya hatua kubwa iliyofikiwa ni utaratibu wa kuwapelekea wamiliki wa ardhi ankara za malipo kupitia ujumbe wa simu za kiganjani.

Katika ukaguzi huo, Dkt Mabula alianzia ziara yake ofisi ya Mtendaji Kata iliyopo eneo la Ndachi Boda ambapo aliwakuta watendaji wa sekta ya ardhi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Dodoma wakitoa huduma kama alivyoelekeza.

"Nimekuja kuangalia kuona maelekezo yangu kuwa badala ya wananchi kwenda kila mara ofisi za jiji kupata huduma basi ofisi hiyo ipange walau mara mbili kwa wiki kwenda katika mitaa kusikiliza changamoto za ardhi nimekuja hapa kuangalia kuona kama hilo limetekelezwa’’ alisema Dkt Mabula.

‘’Mkienda katika mitaa muende na ofisi, yaani idara zote za sekta ya ardhi kwa lengo la kusikiliza kero, kutoa hati na kama ipo haja ya kwenda eneo la mgogoro basi muende na mtoe tangazo kama mtakuwa mahala fulani’’. Alisema Waziri wa Ardhi

Hata hivyo, Waziri Dkt Mabula akiwa katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Ndachi alipata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wakidai kuna mtu aliyemilikishwa kiwanja eneo la Ndachi Mnadani kwa maelezo kuwa kimetokea kwenye shamba lake jambo walilodai siyo kweli.

Kufuatia hali hiyo, Dkt Mabula àliongozana na walalamikaji pamoja na wananchi wengine kwenda kuliona eneo la shamba hilo ambapo akiwa katika eneo hilo walalamikaji walidai mmiliki huyo alipatiwa eneo hilo kiulaghai kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa jiji.

Kufuatia madai hayo, Dkt Mabula alimpigia simu mkuu wa idara ya ardhi wa halmashauri ya jiji la Dodoma Bw. Maduhu Ilanga na kuweka sauti kubwa ili wananchi wasikie moja kwa moja ambapo mkuu huyo wa Idara alieleza utaratibu mzima uliotumika hadi mdaiwa kumilikishwa pamoja na mgogoro uliopo katika eneo hilo.

Mkazi wa Ndachi Bw. Joel Said Katala alimueleza Waziri wa Ardhi kuwa, Dodoma ina changamoto kubwa haswa halmashauri jiji la Dodoma kutokana na watendaji wake kutosimamia ukweli na kuangamiza wananchi huku wakijua ukweli ambapo aliongeza kwa kusema kuwa, watendaji hao hutengeneza uongo kwa sababu wao ni wa mwisho kuzungumza na viongozi.

Mkazi mwingine Shaban Haruna, alisema changamoto ya eneo linalolalamikiwa imetokana na serikali kutangaza uwepo mabadiliko katika eneo hilo kutoka mashamba kuwa makazi huku wananchi wakiwa tayari walishaanza kuishi. Hata hivyo, alisema mkuu wa wilaya ya Dodoma tayari ameunda kamati itakayoshughulikia umilikishaji kwenye maeneo hayo.

Naye Salum Iddy Juma ambaye ni Mwenyekiti wa shina namba moja eneo la Ndachi Mnadani alieleza kuwa, katika mchakato mzima wa utwaaji shamba alilomilikishwa mlalamikiwa, kamati inayosimamia zoezi hilo haijahusishwa jambo alilolieleza kuwa linatia shaka.

Baada ya kupata maelezo kuhusiana na mgogoro huo, Dkt Mabula aliwaeleza wananchi kuwa, pamoja na wizara yake kupitia idara ya ardhi jiji la Dodoma kuwafuata wananchi katika maeneo yao lakini migogoro ya ardhi itaisha tu iwapo wananchi watazingatia sheria kanuni na taratibu na kuacha kuwa na haraka kujenga nyumba bila kuwa na vibali.

"Sasa hivi jiji la Dodoma linakuwa kwa kasi na fursa ziko nyingi na watu wanakimbilia, kuweni na subira katika ujenzi, fuateni taratibu" alisema Dkt Mabula.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alielekeza ujenzi unaoendelea eneo linalolalamikiwa kusitishwa hadi hapo ufumbuzi wa mgogoro wa eneo hilo utakapopatikana.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisikiliza kero za baadhi ya wananchi aliowakuta eneo la Ndachi Dodoma wakati akikagua utekelezaji wa maelekezo yake ya kuzitaka idara za ardhi kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi alipokwenda eneo la Ndachi Mnadani jijini Dodoma kusikiliza mgogoro wa ardhi wakati akikagua utekelezaji wa maelekezo yake ya kuzitaka idara za ardhi kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao mwishoni mwa wiki.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili eneo la Ndachi jijini Dodoma alipokwenda akikagua utekelezaji wa maelekezo yake ya kuzitaka idara za ardhi kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao mwishoni mwa wiki. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post