WANAFUNZI WAWILI WAFA KWA AJALI YA ROLI NA WENGINE ZAIDI KUJERUHIWA


 Mmoja wa majeruhi

Na Dotto Kwilasa, DODOMA 

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma, Dk. Ernest Ibenzi amethibitisha kupokea miili ya wanafunzi wawili wa shule ya Sekondari ya Mpalanga wilayani Bahi mkoani Dodoma waliokufa katika ajali ya lori aina ya Canter lenye namba T519 DSY walilokuwa wamepanda kupinduka wakati wakiwa safarini kwenda kwenye kambi ya michezo ya Umiseta.

Akizungumza na waandishi wa habari Dk.Ibenzi pia amethibitisha kupokea majeruhi  31 wanaohusishwa na ajali hiyo na kwamba wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya rufaa.

“Majira ya saa 7:30 tulipokea majeruhi hao wanafunzi kutoka shule ya sekondari Mpalanga na wanne kati yao wamefanyiwa upasuaji na wengine walikuwa na majeraha madogo ya majeraha wanaendelea vizuri”, amesema Dk. Ibenzi

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika hospitali ya Rufaani ya mkoa wa Dodoma wameeleza chanzo Cha ajali hiyo kuwa ni  mwendokasi .

Amani Yobwa, mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Mpalanga, alisema walipanda usafiri huo kwenda kushiriki michezo ya Umiseta ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika katika kijiji cha Magaga.

“Tulipakiwa kwenye gari lile asubuhi ili kuwahi michezo ya Umiseta lakini tulipofika katika kijiji cha Chidilo kuna eneo kuna kona kali dereva alipokata kona gari likapoteza mwelekeo na kupinduka na kusababisha wenzetu wawili kufa na sisi kujeruhiwa’alisema Yobwa

Magreth Masinga mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo alisema sababu za ajali hiyo ni mwendo kasi na tatizo kubwa ni aina ya gari walilotumia ambalo siyo kwa ajili ya abiria.

“Kama tungepanda gari la abiria kusingekuwa na shida kama hii kwani alipokata kona wanafunzi waliyumba na kulala upande mmoja na kusababisha kupinduka kwa gari hivyo tunaomba magari ya mizigo yasitumike kubeba abiria”alisema Masinga

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi waliopata ajali hiyo Manase Matonya, alisema wanaiomba serika kwenye matukio mbalimbali ya wanafunzi kuacha matumizi ya magari ya mizigo kwa ajili ya kubeba abiria.

“Siku hizi hata minadani abiria hawapandi magari ya mizigo lakini tunashangaa leo watoto wetu kupanda gari la mizigo kwa ajili ya kwenda kwenye michezo ya Umiseta”alisema

Aidha,taarifa iliyotolewa na uongozi wa wilaya ya Bahi inasema kuwa ajali ya gari hilo imetokea kijiji cha Chidilo majira ya saa 5 Asubuhi Kata ya Mpalanga,Tarafa ya Chipanga.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa gari ilikuwa aina ya canter ilikuwa imebeba jumla ya wanafunzi 46 wakitokea Mpalanga Sekondari kwenda Magaga Sekondari kwenye michezo ya Umiseta.

“Wanafunzi wawili wa kike wamefariki dunia hapohapo majina yao ni Neema Yohana Hoya (17) kidato cha tatu mkazi wa Chidilo na Magreth Juma (19)  mkazi wa Nholi na wanafunzi 31 wamepelekwa hospitali ya Rufaani Dodoma kwa matibabu zaidi na wengine 14 wamepatiwa matibabu zahati ya Mpalanga”inasema sehemu ya taarifa hiyo


  


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments