TANZANIA NA KENYA ZAJADILIANA UIMARISHAJI MPAKA WA KIMATAIFA


Afisa Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa Kenya (KIBO) Juster Mkoroi (wa pili kushoto) akisisitiza jambo wakati timu ya wataalamu wa Tanzania na Kenya ilipotembelea eneo la mpaka katika mto Losoyai wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Mei 2023. Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Hamdouny Mansoor na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mwanga Abdalah Mwaipaya.

************

Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA

Tanzania na Kenya ziko katika kikao cha majadiliano ya kuendelea na kazi kuimarisha mpaka wa kimataifa wa nchi hizo mbili kipande cha awamu ya tatu cha kutoka Namanga mkoani Arusha hadi Tarakea Kilimanjaro.

Kikao hicho cha siku tano cha Kamati ya Pamoja baina ya Wataalamu wa nchi hizo mbili kilianza tarehe 29 Mei 2023 na kutarajiwa kukamilika ijumaa tarehe 2 Juni 2023 kikiwa na lengo la kupokea taarifa ya ukaguzi wa kipande cha awamu ya tatu cha km 110 kutoka Namanga mkoani Arusha hadi Tarakea, Kilimanjaro, kufanya ukaguzi wa eneo linaloimarishwa na kuandaa mpango kazi wa awamu zinazofuata.

Akifungua rasmi kikao cha Kamati hiyo ya Pamoja tarehe 31 Mei 2023 jijini Arusha kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo John Mongela, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo David Lyamongi alisema, kikao hicho kinadhihirisha umuhimu wa kazi walioyopewa wataalamu wa nchi hizo mbili kwa kuhakikisha kazi waliyopewa inakamilika katika muda uliopangwa.

‘’Ninafahamu timu ya wataalamu wa pande zote mbili zimekuwa na vikao ambapo kikao cha mwisho kilifanyika mwezi Desemba 2022 mjini Kajiado nchini Kenya na kufuatiwa na ukaguzi awamu ya tatu ya kipande cha kuanzia Namanga hadi Tarakea pamoja Tarakea hadi ziwa Jipe’’ alisema Lyamongi

‘’Tunafahamu kuwa kwa sasa timu ziko uwandani zinaendelea na ujenzi wa alama za mpaka na ni matumaini yangu zoezi linaenda vizuri na litakamilika ndani ya muda uliopangwa’’ alisema Lyamongo.

Mratibu wa zoezi la uimaishaji mpaka wa Tanzania na Kenya kwa upande wa Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi idara ya Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Joseph Ikorongo alisema, kikao hicho cha siku tano kinapokea taarifa ya awali ya ukamilishaji kazi zote za awamu ya kwanza na ile ya pili yenye jumla ya km 348 ambazo tayari zimeimarishwa.

‘’kikao hiki kinachoendelea kinapokea taarifa ya awali ya ukamilishwaji kazi zote za awamu ya kwanza na ya pili yenye jumla ya kilomita 348 ambayo tayari zimekamilishewa’’ alisema Ikorongo.

Kwa mujibu wa Ikorongo, kikao cha Kamati ya Pamoja pia kinaandaa mpango kazi kwa awamu zinazofuata za nne na tano kuanzia eneo la Tarakea mkoani Kilimanjaro hadi Jasini wilayani Mkinga mkoa wa Tanga ufukweni mwa Bahari ya Hindi zinazokamilisha jumla ya kilomita 758 za nchi kavu za mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.

Awali katika siku yake ya pili ya kikao, timu ya wataalamu wa nchi hizo mbili za Kenya na Tanzania ilitembelea eneo la mpaka wa kimataifa lililopo mto Losoyai unaoungana na Ruvu kuingia ziwa Jipe na kufuatiwa na mpaka wa nchi kavu hadi Pangani wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kujiridhisha.

Wakiwa katika eneo hilo, timu hiyo ya wataalamu ya Kamati ya Pamoja ya nchi hizo wakioongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Hamdouny Mansoor kwa upande wa Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa ya Kenya (KIBO) Juster Nkoroi walijionea uhalisia wa mpaka pamoja na changamoto za eneo hilo wakati wa ukaguzi.

Mratibu wa zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Joseph Ikorongo pamoja na wataalamu wa nchi hizo mbili wakiangalia muelekeo wa mfereji wa maji yanayotoka mto Losoyai wakati wataalamu wa nchi hizo walipotembelea eneo hilo tarehe 30 Mei 2023.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor (Kushoto) akitoa maelezo kwa timu ya wataalamu wa Tanzania na Kenya walipotembelea eneo la mto Losoyai wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Mei 2023.


Timu ya wataalamu kutoka Kenya na Tanzania ikielekea eneo la mto Losoyao kuangalia alama ya mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo tarehe 30 Mei 2023.

Ujumbe wa Kenya ukiwa katika kikao cha pamoja kati ya Tanzania na Kenya kujadili uimarishaji mpaka wa nchi hizo tarehe 31 Mei 2023.
Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika kikao cha Kamati ya pamoja kati ya Tanzania na Kenya kujadili uimarishaji mpaka wanchi hizo tarehe 31 Mei 2023.

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha David Lyamongi akizungumza wakati wa kufungua Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Kenya na Tanzania jijini Arusha tarehe 31 Mei 2023.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha David Lyamongi (Katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Kenya unaoshiriki kikao cha Kamati ya Pamoja baina ya nchi hizo jijini Arusha tarehe 31 Mei 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post