SERIKALI IKABIDHI NDEGE  ATCL- MTATURU


MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameiomba serikali kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),ili kuchochea shughuli za utalii nchini.

Mtaturu ametoa ushauri huo Mei 22,2023,wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

“Kwenye hili nitaongea mambo mawili ili kukuza utalii nchini,ukiboresha Shirika letu la ndege utachochea shughuli z utalii nchini,watalii wengi watakuja lakini ukiwa na ndege yako mwenyewe biashara zinazofanyika katika maeneo mbalimbali duniani utakuwa na uhakika nazo,

“Niombe sana Mh Mwenyekiti,tunategemea kupata ndege ya Cargo hivi karibuni ambayo itarahisha biashara za mbogamboga na maua nchi za Ulaya na Asia,niombe sana Shirika hili liangaliwe na serikali iendelee kuliwezesha ili kuhakikisha kwamba linapata faida,”amesema.

Aidha,ameeleza changamoto ya madeni inayoikabili Shirika hilo na kuishauri serikali kubeba deni la Shilingi Bilioni 100 ambalo Shirika hilo linadaiwa.

“Awali wakati Shirika halifanyi kazi lilikuwa linadaiwa karibu Bilioni 236 na wamejitahidi kulipa karibu Bilioni 136 na sasa wamebakiwa na deni la Bilioni 100,niombe serikali iangalie namna ya kulipa deni hili ili kuweza kuweka mizania sawa ya hesabu ya shirika hilo na hivyo liweze kuondokana na hasara ambayo imeweza kujitokeza,”amesema.

Changamoto nyingine aliyoitaja ni kukamatwa kwa ndege katika nchi nyingine ambazo zinaidai Tanzania,“Ndege hizi zimekuwa zinashikwa lakini sio kwamba ATCL inadaiwa bali inadaiwa serikali lakini kwa sababu Shirika la Ndege linamilikiwa na Wakala wa Ndege wa Serikali (ATGF),ndio maana deni lolote linalohusu serikali likipatikana ndege inakamatwa na hivyo kuondoa mtiririko wa usafiri,

Amesema ndege kama inaenda Mumbai au nchi nyingine ukiiondoa maana yake unapunguza mtiririko wa abiria hivyo usitegemee kupata faida.

“Leo hii CAG akienda anaona kila siku Shirika linapata hasara kwa sababu ni mpango ambao tumeuweka wenyewe ,niombe sana serikali iangalie uwezekano wa kuhakikisha ndege hizi za ATCL iweze kumilikiwa na Shirika lenyewe ili kuleta faida na kulifanya shirika liweze kufanya kazi vizuri,”amesema.

Amesema kwa sasa ATCL inalipa Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kukodisha ndege ya serikali jambo ambalo linashangaza kwa serikali kukodishana ndege ilhali ni kitu kimoja.

“Kwa mantiki hii Shirika letu haliwezi kuendelea kwa kuwa linakwama na mambo mengi,Waziri akirudi aseme ni mpango gani wa serikali umefikiwa wa kurudisha ndege hizi ATCL kuondoka kwenye wakala wa ndege wa serikali ili kuondokana na changamoto ambazo shirika inazipata,”ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post